|
|
|
|
|
|
|
Hotuba ya Waziri Kivuli wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe (MB)
Hali ya Uchumi wa Taifa na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Mfumo wa Matumizi wa Serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2007/2008
I. UTANGULIZI
- Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwa niaba ya kambi ya upinzani, napenda kutoa maoni ya kambi ya upinzani kuhusu hotuba ya hali ya uchumi wa Taifa na mpango wa maendeleo na mfumo wa matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2007/2008 kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu cha 43(5)(c) na 81(1) toleo la mwaka 2004.
- Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wa Jimbo langu la Kigoma Kaskazini, viongozi wa chama changu cha CHADEMA na wa Kambi ya Upinzani na wananchi wengine wote wapenzi wa demokrasia kwa ushirikiano wao mkubwa kwangu na kunipa moyo katika kipindi cha mwaka mmoja toka Mkutano wa Bajeti uliopita.
- Aidha, nakupongeza wewe Spika, Mhe. Samwel Sitta na Naibu wako, Mhe. Ana Makinda kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuliongoza Bunge letu katika misingi ya kidemokrasia na kuhakikisha hadhi na uhuru wa Bunge vinalindwa. Tunaipongeza pia azma yako ya kulifanya Bunge letu kuwa Bunge bora Afrika ifikapo mwaka 2011. Tunakuhakikishia ushirikiano wa Kambi ya Upinzani kutimiza lengo hilo.
- Mheshimiwa Spika, Napenda kumshukuru mwenyezi mungu kwa kutuwezesha kuwepo hapa tena leo na kutekeleza majukumu yetu ya kitaifa. Namwomba Mwenyezi Mungu atujaalie afya njema na hekima ili tuwatumikie vema Watanzania. Mungu atupe busara ili tuwatumikie Watanzania bila kujali rangi, kabila, dini, jinsia, hali ya maungo, hali ya afya na bila kujali itikadi za vyama vyetu vya siasa.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani kupitia hotuba hii na Hotuba ya Waziri Kivuli wa Fedha inachambua kwa kina hali ya uchumi wetu na kutoa maoni ya upande wa pili wa Shillingi kwa mujibu wa Kanuni zetu kama nilivyotaja hapo juu. Lengo kuu ni kutoa mchango wa Kambi ya Upinzani katika kukuza uchumi imara unaokua kwa kasi, kuimarisha jitihada za kuupiga vita umaskini miongoni mwa Wananchi wetu na kuboresha maisha ya Watanzania wote katika ujumla wao.
- Mheshimiwa Spika, Baada ya utangulizi huo, naomba sasa nijadili hali ya uchumi wa nchi na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha Mpango huo wa Taifa. Tunatoa mchango wetu tukizingatia kuwa tunaingia mwaka wa pili wa fedha toka serikali ya awamu ya nne ishike madaraka. Kambi ya Upinzani kwa upande wake imepata uzoefu wa kutosha na kupata uwezo mkubwa wa kuichambua bajeti ya Serikali na kupima uwezo na utayari wake katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu.
II. MAPITIO YA HALI YA UCHUMI KWA UJUMLA NA MAONI YA KAMBI YA UPINZANI
- Mheshimiwa Spika, malengo ya uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2006/2007 yalikuwa kama ifuatavyo:
- Pato halisi la Taifa kukua kwa asilimia 5.9 mwaka 2006. Kiwango hiki kilikadiriwa kwa kuzingatia kuwa, ukame, ukosefu wa umeme na kupanda bei ya mafuta katika soko la dunia vingeathiri uchumi wetu.
- Kiwango cha kasi ya upandaji bei kisichozidi asilimia 4.0 kufikiwa ifikapo mwezi Juni mwaka 2007.
- Mapato ya ndani kuongezeka kufikia asilimia 14.5 ya Pato la Taifa
- Kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni itakayokidhi mahitaji ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi saba.
III. MWENENDO WA UCHUMI JUMLA KATIKA MWAKA 2006/2007 Pato la Taifa
- Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Taarifa ya serikali, Pato la Taifa lilifikia takribani shs. 15 Trilioni kwa bei za mwaka 2006 ukilinganisha na Tshs 13 Trilioni mwaka 2005. Kwa takwimu hii inaonyesha kuwa Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.2 na hivyo kuvuka lengo la ukuaji wa asilimia 5.9 lililotarajiwa.
- Mheshimiwa Spika, takwimu hizi za serikali zikiangaliwa kwa uangalifu utagundua kirahisi kabisa kuwa uchumi wetu uliporomoka sana katika mwaka 2006. Taarifa ya serikali inaonyesha kuwa mwaka 2005 thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola moja ya marekani ilikuwa shs. 1128.8 na wakati huo Pato la Taifa lilikuwa takribani shs 13 Trilioni. Mwaka 2006, shilingi ya Tanzania ilikuwa na thamani ya shs.1251.9 kwa dola moja ya Marekani. Kwa bei za mwaka huo Pato la Taifa lilifikia Tshs. 15 Trilioni.
- Mheshimiwa Spika, kwa takwimu hizi za serikali, thamani ya shs ya Tanzania mwaka 2006 ilishuka kwa asilimia 10.9, hivyo thamani halisi ya Pato la Taifa 2006 kwa bei za mwaka 2005 lilikuwa ni Tshs 12.15 Trilioni tu. Tukilinganisha na Pato la Taifa la mwaka 2005 ambalo lilikuwa 13 Trilioni kwa bei za mwaka 2005, tutaona kuwa ukuaji wa Pato la Taifa uliporomoka.
- Mheshimiwa Spika, Uchumi wetu umegawanyika katika sekta tisa (9). Sekta hizi ni Kilimo, Uchimbaji Madini, Bidhaa za Viwandani, Umeme na Maji, Ujenzi, Biashara na Mahoteli, Mawasiliano na Uchukuzi, Fedha na Huduma za Biashara na Uendeshaji wa Serikali. Kwa mujibu wa Takwimu za Serikali ukuaji wa kila sekta mwaka 2006 ni kama unavyoonyeshwa na jedwali hili hapa chini.
Ukuaji wa Pato la Taifa (%) mpangilio kutokana na kasi ya ukuaji
| No. |
Sekta ya uchumi |
2005 |
2006 |
1 |
Uchimbaji Madini |
15.7 |
16.4 |
2 |
Ujenzi |
10.3 |
10.0 |
3 |
Biashara za Viwandani |
9.0 |
8.6 |
4 |
Biashara na Mahoteli |
8.2 |
8.4 |
5 |
Mawasiliano na Uchukuzi |
6.4 |
7.5 |
6 |
Fedha na Huduma za Biashara |
5.3 |
5.5 |
7 |
Uendeshaji Serikali |
5.1 |
5.1 |
8 |
Kilimo |
5.1 |
4.1 |
9 |
Umeme na Maji |
5.1 |
-1.8 |
| |
Pato la Taifa |
6.7 |
6.2 |
Source:Hali ya Uchumi wa Taifa katika Mwaka, 2006. June,2007
- Mheshimiwa Spika, ukichambua takwimu katika jedwali hili hapo juu utagundua kuwa sekta ya Kilimo ambayo inachangia sehemu kubwa ya pato la taifa ukuaji wake umeporomoka kwa 1.0. Kwa kuwa Tanzania inapima uchumi wake kutokana na thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa nchini, kushuka huku kwa ukuaji wa kilimo kunaashiria kuporomoka kwa uzalishaji katika sekta hii.
- Mheshimiwa Spika, Huu ni mwaka wa tatu wa MKUKUTA. Ukuaji wa sekta hii ambayo ndio shughuli kuu vijijini katika hali ya kusuasua kunaonesha dalili mbaya katika juhudi za kupambana na umasikini. Sababu za ukame hazitoshi kuelezea hali hii. Ni lazima sasa kama nchi tuamue maamuzi muhimu kwa ajili ya kuokoa kilimo chetu.
- Mheshimiwa Spika, Mchango wa sekta ya kilimo mwaka 2006 ulikuwa asilimia 44.7 tofauti na mwaka 2005 ambao ulikuwa asilimia 45.6. Kwa uchumi wowote unaokua, mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi unapaswa kupungua mwaka hadi mwaka kwani ukuaji wa sekta nyingine kutokana na kupanuka kwa uchumi hupunguza mchango wa sekta ya Kilimo. Hata hivyo, kwa Tanzania nadharia hii bado haifanyi kazi. Na hivyo kupungua huku kwa Tanzania si dalili njema. Mchango wa sekta ya Kilimo katika pato la Taifa unashuka kutokana na ukame na kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya Kilimo na Chakula. Hii inaonesha kuwa bado hatujafanya kazi sawa sawa katika kuleta mapinduzi ya Kilimo.
- Mheshimiwa spika, takwimu za sensa za mwaka 2002/03 zinakadiria kwamba kuna jumla ya wakulima wadogo milioni 4.8 wanaolima takriban hekta milioni 44 ukulima huu ni wa kifamilia zaidi, uzalishaji huu ni wa ubora wa chini na kwa ajili ya chakula tuu (subsistence). Asilimia 70 ya wakulima wadogo wadogo hawana kipato kingine chochote nje ya kilimo na wengi wao wanatumia walichozalisha ingawa asilimia 70 tena wanauza kidogo katika walichozalisha. Hivyo kuna uongezaji thamani mdogo sana wa bidhaa zao. Soko la bidhaa ni changamoto kubwa na vile vile kuna vikwazo vya kimmuundo kama bodi za mazao na au vyama dhaifu vya ushirika. Ni asilimia 8 tu ya wakulima wadogo wadogo ndio wanaofanya kilimo cha umwagiliji na ni aslimia 3 tu wanapata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya shughuli zao za kilimo. Mingi ya mikopo hii ni kwa ajili ya mbolea, madawa na mbegu na kiasi kidogo sana ni kwa ajili ya vifaa (machine),nguvu kazi na umwagiliaji. Huduma za ugani inafikia asilimia 35 tu ya wakulima wadogo wote.
- Mheshimiwa spika, ripoti ya umasikini na maendeleo ya binadamu ya mwaka 2005 inataarifu kwamba tutaweza tu kupunguza umasikini iwapo ukuaji wa uchumi vijijini hususani sekta ya kilimo utakua kati ya asilimia 6 mpaka 8 kwa mwaka. Kwa hali ya sasa ilivyo ya uzalishaji katika kilimo hatutaweza kufikia malengo ya MKUKUTA.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani bungeni inapendekeza hatua zifuatazo kuchukuliwa ili kuongeza uzalishaji katika kilimo na kuongeza ubora wa mazao ya kilimo:-
- Kuongeza ukuaji wa uchumi vijijini kwa kuhamasisha utangamano wa skimu za uzalishaji (integrated production schemes) ambazo zinahusisha upatikanaji wa pembejeo, teknolojia, huduma za ugani, usafirishaji na masoko.
- Kuhamasisha uanzishwaji wa umoja wa wazalishaji wa mazao ili kuwapa sauti kubwa wakulima katika kutetea haki zao.
- Kutoa vivutio (incentives) kwa taasisi za kifedha zitakazotoa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji mkubwa katika kilimo.
- Kutenga rasilimali nyingi zaidi kutoka katika bajeti ya nchi kwa ajili ya kilimo na shughuli zinazohusiana na kilimo. Waziri kivuli wa fedha na Waziri Kivuli wa Kilimo watawasilisha makadirio ya rasilimali kwenda kilimo kwa undani zaidi.
-
Mheshimiwa Spika, sekta ya madini ilikua kwa asilimia 16.4 mwaka 2006. Mwaka 2005 sekta hii ilikua kwa asilimia 15.7. Hata hivyo, ukuaji wa sekta ya madini hauendani na ukuaji wa ajira na kupungua kwa umasikini. Kama nilivyosema mwaka jana Taarifa ya hali ya umasikini nchini inaonesha kuwa, sekta ya madini inachangia ajira chini ya asilimia moja. Yaani katika kila ajira 100 zinazotengenezwa nchini katika mwaka, sekta ya madini inachangia chini ya mtu mmoja katika ajira. Mheshimiwa Spika, Hii inasababishwa na sababu moja kubwa, kuwa sekta ya madini na Migodi haina mahusiano na sekta nyingine za uchumi yaani ‘forward and backward linkages’.
- Mheshimiwa Spika, licha ya kwamba mgodi mpya wa kabanga wa Nickel ni moja ya miradi mikubwa sana duniani lakini ulioko eneo la mbali na lisilo na miundombinu. Serikali bado haijaonyesha juhudi yeyote katika bajeti ya mwaka huu ya kufungua miundo mbinu kwa mikoa ya magharibi ili kuwezesha Nickel itakayochimbwa kufika bandarini Dar es Salaam na Tanga. Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Economists Intelligence Unit (EIU) ya mwezi Machi mwaka 2007 (Tanzania at a Glance 2007-2008), wawekezaji wa mradi huo kampuni za Barick Gold ya Kanada na Xstrata ya Uingereza na Uswizi walitangaza katikati ya mwezi Februari kuwekeza dola milioni 95 zaidi ili kufanikisha mradi huo. Uwekezaji huu ni muhimu sana kwa Tanzania kwani utatuondolea utegemezi wa dhahabu kwa kiasi kikubwa katika mauzo yetu ya nje. Hata hivyo, Kambi ya Upinzani inaishauri serikali kuhakikisha kuwa mkataba wa wawekezaji hawa wa mgodi wa Nickel unazingatia kwa kiasi kikubwa maslahi ya Tanzania na kuepuka makosa yaliyofanywa katika migodi mengine.
- Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji Kambi ya Upinzani inasikitika kuwa haijazungumzia kabisa Sekta ya mafuta na gesi asilia kwa kina. Mwaka jana kampuni ya Kifaransa inayoitwa Maurel & PROM ilitangaza kugundua Gesi yenye takriban ujazo wa C. futi 5 trillioni katika wilaya ya Mkuranga. Gesi hii ingekuwa ni sababu tosha kabisa kiuchumi kugeuza IPTL kutoka kwenye matumizi ya mafuta kwenda kwenye matumizi ya gesi na hivyo kupunguza gharama za umeme na pia kupunguza matumizi makubwa ya serikali katika sekta hiyo.
- Mheshimiwa Spika, vile vile, bado kuna makampuni mengi sana yanaendelea kutafuta mafuta katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Yako Makampuni ambayo tayari mikataba yake ya uzalishaji (Production Sharing Agreement (PSA)) imesainiwa na mengine ndio kwanza yameomba kufanya utafiti, tena katika maeneo ambayo hata hatukutegemea. Kwa mfano, kampuni ya TULLOW Oil kutoka nchini Ireland imeomba kutafuta mafuta katika eneo la kaskazini mwa ziwa Tanganyika (Lake Tanganyika- East Block A) na kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya shirika la petroli nchini, mkataba wa uzalishaji (PSA) ulipaswa kusainiwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2007. Taarifa kama hizi ni muhimu kutolewa bungeni katika taarifa ya hali ya uchumi ikitaja angalau maombi ya kutafuta mafuta nchini yako kiasi gani, na utafutaji unaendeleaje. Hii itasaidia sana kutuondolea matatizo huko baadae kuhusiana na mikataba na wawekezaji hao. Na vile vile ingetusaidia kushirikisha wananchi wa maeneo husika katika kuandika mikataba ambayo itakuwa na faida kwao. Hata hivyo naipongeza kampuni ya TULLOW na shirika letu la TPDC kwa kuamua kutafuta mafuta katika mkoa wa Kigoma. Inshallah yatapatikana.
- Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba imefika wakati serikali kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa za madini yetu kwa kushirikiana na sekta binafsi. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kimkakati kununua hisa za kati ya asilimia 10 na 20 katika migodi yote ya madini hapa nchini, na hatimaye kuhamishia Hisa hizo kwa Wananchi kadiri wanavyopata uwezo kiuchumi kwa lengo la kuwanufaisha Wananchi na Rasilimali ya nchi yetu. Vile vile, tunaitaka Serikali kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi kunakofanywa na makampuni ya madini, kwani usafirishaji huu unalipotezea taifa fedha nyingi na maliasili zake.
- Mheshimiwa Spika, Sekta ya viwanda ilikua kwa asilimia 8.6 kwa mwaka 2006 ikilinganishwa na asilimia 9.0 kwa mwaka 2005. Serikali inasema kwamba upunguaji huu ulitokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kulikoambatana na mgao wa umeme hasa kwa viwanda ambavyo viko katika maeneo ya makazi. Vile vile, takwimu za serikali zinaonesha kwamba mchango wa sekta ya bidhaa za viwandani uliongezeka kutoka asilimia 9 mwaka 2005 mpaka asilimia 9.2 mwaka 2006. Kwa maoni ya Kambi ya Upinzani kutokana na taarifa za kiuchumi zilizowasilishwa na Serikali mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa umeongezeka kwa sababu uzalishaji katika kilimo umeshuka lakini katika hali halisi mchango wa sekta hii haujaongezeka. Ni dhahiri Sekta moja ikishuka, kitakwimu sekta nyingine itaonekana kupanda. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu hali hii.
- Mheshimiwa Spika, kinyume na maelezo ya serikali hali halisi ya uchumi inaonesha kwamba ukuaji wa sekta ya viwanda ambayo ni sekta muhimu sana katika uchumi wa nchi uliporomoka. Kushuka huku kwa ukuaji wa sekta ya viwanda kunathibitisha athari za mgao wa umeme zilizoikumba taifa letu kinyume na kauli za serikali kwamba mgao wa umeme haukuathiri uchumi.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi mbali mbali ambazo zinazoendelea katika Sekta hii, Kambi ya Upinzani inaamini jitihada za kutosha hazijafanywa katika mazingira bora ya uwekezaji katika eneo la kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo (Agro Processing). Taifa letu linapoteza mapato mengi kwa kuuza bidhaa ghafi. Uwekezaji katika eneo hili utasaidia sana kupanua uchumi wa maeneo ya vijijini (rural economy) na wakati huo huo kukuza ajira kwa vijana wetu.
- Mheshimiwa Spika, Serikali imetueleza hapa kwamba uzalishaji wa ngozi ulipungua kutoka vipande milioni 3.7 mwaka 2005 hadi vipande milioni 3.4 mwaka 2006. kwa mujibu wa taarifa ya serikali upungufu wa ngozi ulisababishwa na ukame ambao ulisababisha upungufu mkubwa wa malisho na vyakula vya mifugo na hivyo kupelekea kupungua kwa wanyama waliochinjwa wanaotoa ngozi. Kambi ya Upinzani haikubaliani na sababu hizi zilotolewa kwa sababu takwimu za serikali zinaonesha kuwa uzalishaji wa nyama uliongezeka kwa asilimia 2.6. Huwezi kupata nyama zaidi kama hujachinja mifugo. Kwa hiyo ongezeko la uzalishaji wa nyama linapaswa kuendana sambamba na uzalishwaji wa ngozi. Na kimsingi, wakati wa ukame wanyama huchinjwa zaidi kwa ajili ya chakula na hivyo tungetarajia ukame utupatie ngozi nyingi zaidi. Kambi ya Upinzani inataka maelezo ya kina katika eneo hili.
- Mheshimiwa Spika, tatizo tulilonalo katika sekta hii ya mifugo ni kwamba Serikali inakusanya asilimia 60 tu ya ngozi zote zinazozalishwa na asilimia 20 tu ya makusanyo yote ya ngozi ndiyo inayosindikwa. Mbaya zaidi, ubora wa ngozi zetu ni wa daraja la 3 na la 4. Katika mwaka wa fedha unaoisha pato linalotokana na bidhaa za ngozi limefikia bilioni 16.18 wakati kwa maoni ya Kambi ya Upinzani sekta hii inao uwezo wa kuliingizia taifa mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 96. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kufanya mkakati madhubuti zaidi ili kuboresha zao hili. Moja ya mkakati huo ni pamoja na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ya sekta ya mifugo na kuhamasisha wafugaji kuunda ushirika wenye nguvu ili sio tu kutetea maslahi yao bali pia kuboresha ubora, uzalishaji na kutafuta soko la ngozi. Kambi ya Upinzani inapendekeza kufikia lengo la ukuaji wa asilimia 5 mpaka 6 katika sekta hiyo. Maoni kamili ya Kambi ya Upinza ni katika eneo hili yatawasilishwa Waziri kivuli wa Maendeleo ya Mifugo.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2006 sekta ya Umeme na Maji iliathirika sana. Ukuaji katika sekta hii uliporomoka kutoka asilimia 5.1 mpaka asilimia -1.8. Ni dhahiri, janga la mgao wa umeme lilichangia sana kuporomoka kwa sekta hii. Sekta nyeti kama hii, kuporomoka kiasi hiki ni janga kwa taifa. Janga hili halihitaji suluhisho la dharura tu, ni lazima tuwekeze katika miradi mikubwa yenye kudumu muda mrefu. Kwa mfano, kwa miaka mingi wataalamu na wananchi mbali mbali wameshauri uwekezaji mkubwa wa kuzalisha umeme wa njia ya maji katika mto Rufiji katika maporomoko ya Stigler’s Gorge. Licha ya kwamba mradi huu unahitaji mkakati wa muda mrefu, lakini huu ni mwaka wa pili wa bajeti ya Serikali ya Awamu ya Nne. Mradi huu hautajwi kabisa. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze ni Mkakati gani hasa imeweka katika utekelezaji wa Mradi huu, na miradi mingine ya Umeme badala ya kuwekeza katika miradi ya dharura tu.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inadhani pia wakati sasa umefika kuangalia uwezekano wa kuifanya mikoa ama mmoja mmoja au kikanda ijitegemee katika uzalishaji wa nishati ya umeme. Hii itasaidia kuondoa balaa la nchi nzima kuathirika kunapotokea janga la ukame kama ilivyotokea mwaka 2006 na kuwezesha viwanda kufanya relocation pale inapobidi. Njia hii pia itachochea maendeleo sawia kwa mikoa yote.
- Mheshimiwa Spika, Sekta ya uuzaji wa jumla, rejareja na mahoteli ikijumuisha utalii ilikua kwa asilimia 8.4 mwaka wa 2006 ikilinganishwa na asilimia 8.2 mwaka 2005. Taarifa ya serikali inaonyesha kuwa kukua kwa sekta hii kulichangiwa zaidi na kuboreshwa kwa mazingira ya kufanya biashara pamoja na kuongezeka kwa shunguli za utalii, taarifa inaendelea kuonyesha kwamba jumla ya watalii 644,124 waliingia nchini mwaka 2006 ikilinganishwa na watalii 612,754 mwaka wa 2005. Mapato yaliyotokana na utalii ni dola za marekani 862.0 milioni.
- Mheshimiwa spika, mwaka 2006 wakati nawasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu hali ya uchumi nchini niliezea tatizo la upotevu wa mapato kutokana na sekta ya utalii kupitia kitu kinachoitwa ‘package tourism’. Taarifa kutoka kwa wadau wa sekta ya utalii zinaonyesha kuwa katika kila mtalii mmoja aneingia Tanzania kwa siku moja dola za kimarekani 100 zinabaki katika nchi ya ulaya au marekani kwani watalii hivi sasa kupitia mfumo huu wa package tourism wanalipia kila kitu wakiwa huko huko kwao.
- Mheshimiwa spika, Ukilinganisha idadi ya watalii wanoingia Tanzania na mapato ya utalii yaliyorikodiwa mwaka 2006 utagundua kuwa kila mtalii aliyeingia Tanzania alitumia dola za kimarekani 1338 tu. Hii haingii akilini. Iwapo kila Mtalii alikaa nchini siku saba tu, na iwapo nusu ya watalii walitumia mfumo huu wa package tourism na hivyo kila mtalii kulikosesha taifa dola za kimarekani 100 kila siku. Kwa takwimu za mwaka 2006, Taifa lilipoteza mapato ya dola za kimarekani milioni 225.
- Mheshimiwa Spika, katika sekta ndogo ya uwindaji wa kitalii kumetokea malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi. Sekta hii imekuwa ni chanzo cha mapato mengi ya serikali kupotea. Kambi ya upinzani katika Bajeti yake kivuli itakayosomwa muda mfupi ujao inadhani kuna Taifa lingeweza kukusanya mapato zaidi kutoka katika sekta hii. Ili lengo hili lifanikiwe, pamoja na mambo mengine hatua zifuatazo lazima zichukuliwe:-
- Sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 1974 kupitiwa upya na kufanyiwa marekebisho makubwa na au kuifuta na kuitunga upya. Sheria mpya itoe kipaumbele kwa watanzania katika TASNIA ya uwindaji wa kitalii.
- Ifikapo mwisho wa kipindi cha umilikaji vitalu vyote virudishwe serikalini kwa ugawaji mpya na kampuni za uwindaji za watanzania zipewe fursa na nafasi ya kwanza kushindania umiliki wa vitalu.
- Taratibu za ugawaji wa vitalu ziwe wazi ikiwa ni pamoja na kutangaza vitalu vilivyo wazi na biaonuwai zake.
-
Mheshimiwa spika, wakati tunaongeza juhudi za kutangaza zaidi vivutio vya utalii vilivyopo nchini mwetu na hivyo kufikia lengo la kuwa na idadi ya watalii milioni 1 kwa mwaka, ni vyema Serikali ikachukua hatua za makusudi kudhibiti upotevu huu wa mapato yatokanayo na utalii. Waziri kivuli wa Fedha na Waziri kivuli wa Maliasili na Utalii wataelezea mapendekezo ya mikakati maalum itakayopelekea kuongeza mapato zaidi kutokana na sekta hii.
- Mheshimiwa Spika, taarifa ya serikali inaonyesha ya kwamba thamani ya mauzo ya bidhaa nje iliongezeka kwa asilimia 2.8. Ongezeko hili, kwa mujibu wa serikali, lilichangiwa zaidi na bidhaa zisizo asilia kama dhahabu na bidha za viwandani. Naomba nichukue nafasi hii kufanya uchambuzi kidogo kuhusiana na mauzo yetu nje ya nchi. Tazama jedwali hapa chini.
Mchango wa Bidhaa katika Thamani ya Mauzo yote Nje mwaka 2006
| No. |
AINA YA BIDHAA |
MCHANGO(%) |
1 |
Madini |
47.8 |
2 |
Bidhaa za viwanda |
14 |
3 |
Bidha nyinginezo |
8.9 |
4 |
Samaki na bidhaa zake |
8 |
5 |
Re-exports |
7.4 |
6 |
Tumbaku |
3.8 |
7 |
Kahawa |
3.6 |
8 |
Pamba |
3.2 |
9 |
Korosho |
2.3 |
10 |
Chai |
1.8 |
11 |
Maua |
0.9 |
12 |
Karafuu |
0.5 |
13 |
Katani |
0.4 |
Chanzo: Tarifa ya hali ya uchumi ya taifa2006 kwa Kamati ya Bunge, Fedha na Uchumi,Dar-Es-Salaam, 2007.
- Mheshimiwa Spika, ukichunguza kwa makini jedwali hilo hapo juu utaona dhahiri kabisa kwamba bidhaa mbili tu, yaani Madini na Samaki, zinachangia takribani asilimia 55.7 ya mauzo yote ya nje. Kwa uchumi wowote ule unaokua na wenye lengo la kunufaisha watu wengi zaidi mwenendo huu wa mauzo ya nje unatisha. Mbaya zaidi sekta hizi zinazochangia zaidi ya nusu ya mauzo yetu nje ziko mikononi mwa watu wachache na wa kutoka nje. Hivyo watanzania walio wengi na wanyonge hawafaidiki moja kwa moja.
- Mheshimiwa Spika, ukifanya uchunguzi zaidi katika takwimu nilizotoa hapo juu utaona kuwa, mauzo yetu ya nje yanachangiwa kwa zaidi ya nusu na bidhaa zinazotoka sehemu moja ya nchi. Sote tunafahamu kwamba madini na samaki ambazo zinachangia asilimia hiyo yote zinatoka katika mikoa ya kanda ya Ziwa, Shinyanga, Mwanza, Mara na Kagera. Ukiongeza mchango wa Pamba na Kahawa kutoka eneo hili la nchi mchango wake katika mauzo ya nje unafikia takribani asilimia 60 ya mauzo yote.
- Mheshimiwa Spika, Hali hii siyo nzuri kwa umoja na mshikamano wa taifa letu wachochezi wachache wanaweza kuanza kudai sehemu kubwa ya mapato yanayotokana na mauzo nje yarudi maeneo hayo na kuhatarisha amani yetu. Hivyo ni lazima Serikali ichukue hatua za haraka kurekebisha hali hii kwa kuhamasisha uzalishaji katika mikoa mingine na mazao mengine na hasa mazao ya kilimo na hivyo kuongeza pato la Taifa kutoka nje na kwa muda huo huo kuongeza usawa wa kiuchumi baina ya mikoa.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuanza kutumia bajeti ya nchi (budget as a policy instrument) ili kuchochea uzalishaji wa bidha za Viwandani na Mashambani na hivyo kuongeza mauzo ya nje. Baada ya muda mfupi ujao Waziri Kivuli wa Fedha atawasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu taratibu makini kwa ajili ya kuchochea uzalishaji katika uchumi na mauzo ya nje kupitia Bajeti ya Serikali jambo ambalo haliko wazi katika Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji na hata Waziri wa Fedha.
- Mheshimiwa Spika, taarifa ya serikali kutoka wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji inaonyesha kuwa katika mwaka 20006/2007 kulikuwa na jumla ya kilomita 9,000 za barabara kuu na Kilomita 18,000 ya barabara za mikoa zilizofanyiwa ukarabati katika kipindi cha Mwaka wa Fedha unaoisha. Kwa mujibu wa taarifa hii katika mwaka wa fedha unaomalizika hakuna barabara mpya zilizojengwa.
- Mheshimiwa Spika, mara baada ya Rais wa awamu ya pili, ndugu Ali Hassan Mwinyi kushika uongozi wa nchi yetu aliulizwa na waandishi wa habari wa vyombo vya magharibi juu ya vipaumbele vya utawala wake akawajibu kwa kusema ‘Kipaumbele changu cha kwanza ni barabara, kipaumbele changu cha pili ni barabara, na kipaumbele changu cha tatu ni barabara’. Rais wa awamu ya tatu ndugu Benjamin Mkapa ambaye ndiye aliyenukuu maneno hayo ya mtangulizi wake wakati alipokuwa akikabidhiwa Uenyekiti CCM naye akasema vipaumbele vyake ni Barabara, Ukuaji wa uchumi na Elimu.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kwamba katika moja ya vipaumbele vya serikali ya Awamu ya Nne swala la miundombinu ya barabara halipo na hii inathibitishwa na hatua ya Serikali ya Awamu ya Nne ya kutojenga angalau kilomita moja ya barabara mpya na badala yake kuendelea kukarabati Barabara ambazo zimetengenezwa na serikali zilizopita. Kama ipo barabara mpya iliyofunguliwa, Kambi ya Upinzani inapenda Taarifa hiyo itolewe kikamilifu ndani ya Bunge hili Tukufu.
- Mheshimiwa Spika, Maoni ya Kambi ya Upinzani ni kuwa kwa mwaka huu wa fedha asilimia 21 ya bajeti itengwe kwa ajili ya miuondombinu ya barabara kutokana na umuhimu wake katika kukuza uchumi. Vipaumbele ni katika kufungua maeneo ya nchi ambayo hajafunguliwa ya kutosha au hata kabisa kwa muda mrefu sasa. Hivyo, tofauti na Mpango wa Serikali katika Bajeti ya Serikali 2007/08 maoni ya Mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya barabara, pamoja na kuendeleza miradi iliyopo, kufungua miradi ya ujenzi katika barabara muhimu zifuatazo:
- Masasi-Tunduru-Songea mpaka Mbamba Bay
- Tunduma- Sumbawanga-Mpanda mpaka Kigoma
- Kigoma-Tabora mpaka Manyoni
- Mbeya-Sikonge mpaka Nzega
- Iringa-Dodoma-Kondoa mpaka Babati
- Babati-mpaka Singida
- Oldeani-Matala mpaka Lalago
- Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile miradi hii inahitaji fedha nyingi sana na haiwezi kuisha kwa haraka na kwa pamoja kwa wakati moja. Hata hivyo ni lazima kuanza ili kuendelea kuipangia fedha za maendeleo katika kila mwaka wa bajeti mpaka zitakapo kamilika. Uwekezaji huu utalipa kwani utaifungua nchi yetu, utaongeza uzalishaji na na kupanua uchumi wetu. Waziri kivuli wa Fedha na Waziri kivuli wa Miundombinu watatoa maelezo zaidi juu ya utekelezaji wa miradi hii ya kipaumbele ya barabara.
- Mheshimiwa Spika, ili kukua kwa uchumi kuwe na manufaa kwa Watanzania ni lazima serikali kwa makusudi kabisa iamue kuweka sera rafiki kwa masikini (pro-poor policy). Sera rafiki kwa watu masikini ni zile sera zinazoelekea kuweka rasilimali katika sekta zinazokua na zinazoajiri watu wengi zaidi. Kilimo ni sekta pekee inayoweza kuondoa umasikini nchini Tanzania. Hivyo, lazima maamuzi ya makusudi yafanywe ili kuwekeza rasilimali za kutosha kabisa katika kilimo.
- Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi uliofanyika mwaka 2005/2006 hivi sasa Tanzania Bara ina jumla ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi wanaofikia milioni 20.6. Utafiti huo unaonyesha kuwa wastani wa ongezeko la watu katika soko la ajira kila mwaka ni watu 760,000.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inatambua kuwa kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu sasa tunayo Tafsiri ya Taifa ya Ajira, kwa viwango vya ILO. Tafsiri hiyo inazingatia mazingira ya ajira katika Tanzania ambapo sehemu kubwa ya watu wanafanya kazi za kujiajiri badala ya kuajiriwa, na kazi nyingi ni za msingi katika sekta ya kilimo na sekta isiyo rasmi. Kati ya watu milioni 20.6 wenye uwezo wa kufanya kazi, watu milioni 18.3 walikuwa wana kazi na watu milioni 2.3 hawakuwa na kazi. Kwa mujibu wa tafsiri hiyo 11% ya Watanzania hawana kazi. Katika jiji la Dar es Salaam 31.4% ya watu hawana kazi.
- Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, wakati wa kampeni zake aliahidi kutengeneza ajira 1,000,000 katika kipindi cha miaka 5. Hii ni sawa na ajira 250,000 kila mwaka kuanzia mwaka 2006 mpaka 2010. Nasikitika kwamba Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji katika Hotuba yake na hata katika Taarifa ya Hali ya Uchumi haikuelezea ni ajira ngapi zimetengenezwa kwa mwaka wa fedha 2006/2007 na kama tumefikia malengo ya mwaka kwa mujibu wa ahadi ya Mheshimiwa Rais na ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. Hata kama tungeweza kutimiza lengo la kuwa na ajira 250,000 bado hii ingelikuwa ni 33% tu ya Watanzania wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka. Taarifa ya Hali ya Uchumi inaelezea tu ‘kuwa Serikali itawashirikisha vijana katika kuanzisha na kutekeleza mipango, mikakati na Programu mbalimbali. Hii ni lugha iliyozoeleka miaka nenda rudi na haitoi sana matumainikuwa lengo la Millioni moja(1) itafikiwa.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa tatizo la ajira lianze kutazamwa kwa muono mpana zaidi na tunashauri katika mwaka huu ujao wa fedha mchakato wa kuchambua upya sera ya Taifa ya ajira uendane na mjadala wa kitaifa kuhusu ajira, ujira na tija. Tatizo la Ajira ni ‘Bomu’ linaloweza kulipuka wakati wowote lisiposimamiwa vizuri.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imefurahishwa sana na uamuzi wa kurudisha miliki ya Kampuni ya Ndege Tanzania katika serikali. Uamuzi huo ni ushahidi tosha wa kwamba tulifanya maamuzi mengi mabaya sana katika ubinafsishaji wa mashirika yetu ya umma. Pia umetugharimu sana. Linalotusikitisha ni kwamba wahusika waliofanya maamuzi haya mabovu hawajachukuliwa hatua zozote. Kambi ya upinzani inapendekeza kutenga fedha za kutosha kabisa katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2007/2008 kulifanya Kampuni ya ndege Tanzania lifanye kazi zake kikamilifu.
- Mheshimiwa Spika, mwaka 2006 Shirika la reli Tanzania lilisafirisha mizigo tani 775,281 ikilinganishwa na tani 1,169,000 mwaka 2005. Usafirishaji wa mizigo ulipungua kwa 34%. Upungufu huu ulitokana na Treni ya abiria kuanzia safari zake Dodoma badala ya Dar es Salaam.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa kwa tathmini hii nchi yetu inarudi nyuma kimaendeleo. Hebu tujiulize, wakati tunapata uhuru treni ilikuwa ikitoka Kigoma inafika Dar es Salaam. Leo, miaka 45 baada ya uhuru, treni ikitoka Kigoma inaishia Dodoma. Twaenda mbele au twarudi nyuma?
- Mheshimiwa Spika, tumepokea taarifa kwamba hatua ya ukodishaji wa shirika la reli kwa kampuni ya RITES ya India sasa imekamilika. Tunatoa angalizo ya kwamba pamoja na kuwa matumaini ni kuwa mwekezaji ataborasha miundombinu ya reli na kununua vichwa vipya, kubadilisha line na mitambo iliyochakaa, ni vigumu mwekezaji ambaye nia yake ni biashara kufanya haya yote Angalizo hii iwe Ilani kwa Serikali kusimamia kikamilifu zoezi la Ukodishaji wa Reli yetu, na kusimamia utekelezaji wa mkataba wa ukodishaji. Kambi ya Upinzani inaamini Serikali itakuwa tayari kuleta taarifa ya mara kwa mara Bungeni ili kuona jinsi utekelezaji huo unavyoenda kulingana na matarajio yetu. Kambi ya upinzani inapendekeza mkakati maalum ubuniwe ili kuongeza uwezo wa reli yetu ili kusafirisha mizigo ya kutosha kutoka nchi jirani za Burundi na DRC. Reli ya kati inalipa sana kiuchumi, changamoto ni kuwekeza katika reli hii.
- Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu 2006/2007 nilizungumzia kuhusu taarifa ya hali ya umasikini nchini na kutaka iwe sehemu ya taarifa ya hali ya Uchumi. Katika kitabu cha Hali ya Uchumi mwaka 2006, suala la umasikini limeongelewa sanjari na utekelezaji wa MKUKUTA. Kasi ya upunguaji wa Umasikini bado ni ndogo mno. Hata hivyo kitakwimu, kasi ya upunguaji wa umasikini mijini ni kubwa zaidi kuliko ile ya vijijini japo katika hali halisi mambo yanaweza kuwa tofauti kabisa, hasa kwa upande wa umaskini wa kipato.
- Mheshimiwa Spika, licha ya kugawa rasilimali zetu kulingana na clusters za MKUKUTA, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa hali ya umasikini kiwilaya izingatiwe katika kugawa rasilimali za Bajeti. Kambi ya Upinzani inatambua kuwa fedha zinazokwenda katika serikali za Mitaa zinagawiwa kwa formula maalum, iliyo wazi na yenye kueleweka kwa kila moja, badala ya formula ya sasa ambapo Wilaya inaweza kukosa fedha kutokana na vigezo ambavyo havitokani moja kwa moja na wilaya yenyewe( Benchmarks).
- Mheshimiwa Spika, naomba niwasilishe hali ya umasikini kiwilaya kwa wananchi kwa kigezo cha idadi ya wananchi walio katika Umaskini wa kutupwa (% of households below basic needs poverty line). Tazama jedwali lifuatalo:-
| Wilaya masikini Zaidi |
Wilaya zenye Ahueni |
| Bunda |
68% |
Bukoba Mjini |
11% |
| Musoma |
64% |
Arusha Mjini |
12% |
| Geita (Vijijini) |
62% |
Mbeya Mjini |
12% |
| Serengeti |
61% |
Mbarari |
13% |
| Singida (Mjini) |
56% |
Morogoro Mjini |
14% |
| Namtumbo |
55% |
Kinondoni |
14% |
| Meatu |
53% |
Nyamagana |
15% |
| Lindi (Vijijini) |
51% |
Lushoto |
16% |
| Kisarawe |
51% |
Ilala MC |
16% |
| Babati |
50% |
Tanga Mjini |
17% |
Source:Poverty and Human Development Report, 2005
- Mheshimiwa Spika, ili kukua kwa uchumi kuwe na manufaa kwa Watanzania ni lazima serikali kwa makusudi kabisa iamue kuweka sera rafiki kwa masikini (pro-poor policy). Sera rafiki kwa watu masikini ni zile sera zinazoelekea kuweka rasilimali katika sekta zinazokua na zinazoajiri watu wengi zaidi. Kilimo ni sekta pekee inayoweza kuondoa umasikini nchini Tanzania. Hivyo, kama Kambi ya Upinzani ilivyopendekeza lazima maamuzi ya makusudi yafanywe ili kuwekeza rasilimali za kutosha kabisa katika kilimo.
- Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuwa mwanachama wa mashirika ya kikanda na ya kimataifa. Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Utekelezaji wa itifaki ya ushuru wa forodha inaendelea kutekelezwa na maandalizi ya itifaki ya Soko la Pamoja inafanyiwa kazi. Uamuzi wa kuruhusu nchi za Rwanda na Burundi kuwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokelewa kwa hisia tofauti na wananchi wa Tanzania. Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kuwa uanachama wa nchi hizi katika EAC utatusaidia sana Tanzania kwani uamuzi huu utakuza soko la bidhaa la ndani la eneo letu. Tanzania ianze kuangalia uwezekano wa kuishawishi nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili nayo ijiunge na Jumuiya ya Afrika Mashariki na hatimaye kuwa na Soko la Pamoja na Maziwa Makuu (Great Lakes Community ie glcom) na kisha umoja wa Sarafu. Tukipata soko la pamoja kutoka Bahari ya Hindi mpaka Bahari ya Atlantik, chumi za nchi yetu zitapaa!
- Mheshimiwa Spika, hivi sasa nchi zote za Afrika Mashariki zipo katika mjadala kuhusuu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Ni imani yangu kuwa maoni ya wananchi yatazingatiwa katika ripoti ya Kamati ya Rais ya Uharakishaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki. Changamoto kubwa kwa Watanzania ni kuepuka unyonge na kujiona sisi tupo nyuma kwa kila kitu na badala yake kuweka mikakati thabiti ya kufaidika na Shirikisho kama litakuja leo au kesho vyovyote itakavyokuwa.
- Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inarejea ushawishi wake wa kutaka nchi yetu irejee uanachama katika COMESA. Vile vile ijadiliane kuhusu Economic Partnership Agreements (EPA) kupitia kundi la nchi za ESA. Lengo ni kuwa katika soko kubwa litakalochochea uzalishaji wetu wa ndani.
- Mheshimiwa Spika, kuitangaza nchi ni muhimu sana katika kushawishi uwekezaji nchini. Kituo cha Uwekezaji, TIC bado kina changamoto kubwa. Ni lazima tutumie pesa nyingi kujitangaza. Kuna ushindani mkubwa katika kila nchi kujitangaza, wengine hata majimbo hujitangaza, mfano Jamhuri ya Afrika Kusini. Lazima tuchangamke sasa katika ulimwengu huu wa ushindani kama tunataka wawekezaji wa maana.
- Mheshimiwa Spika, Mpango wa MCC utasaidia sana kuboresha miundombinu, kusambaza huduma za Maji na kuondokana na tatizo la umeme. Kambi ya Upinzani inashauri kuwa kabla ya kuwasilisha ‘compact proposal’ kwa Serikali ya Marekani, ni vema waheshimiwa Wabunge ama kupitia Bunge zima au katika Kamati husika waone, kujadili na kupitisha mpango huo. Uwazi katika miradi ya maendeleo ni kitu muhimu sana ili kuondoa hisia za upendeleo wa baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
KABWE ZUBERI ZITTO (MB)
Waziri kivuli Mipango, Uchumi na Uwezeshaji.
Dodoma, 18.06.07
|
 |
 |
|
 |
 |
|
|
|
|