lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner
»Kwaheri Chacha
»Wasifu wa Marehemu
»Habari Mpya
»Matamko ya Chama
»Makala mbalimbali
»Uchaguzi wa Viongozi
»Uchaguzi Kiteto
»Bajeti ya Upinzani
»Ushirikiano Wapinzani
»Orodha ya Mafisadi
»CCM wezi wa Kura

Kwaheri Mpambanaji

Wasifu wa Marehemu Chacha Zakayo Wangwe

Mhe Chacha Wangwe
Mheshimiwa Chacha Zakayo Wangwe alifariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Julai 28, 2008 saa mbili na dakika hamsini na tano usiku akitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam kuwahi mazishi ya aliyekuwa mbunge wa kwanza wa Jimbo la Tarime Marehemu Bhoke Munanka. Chacha Wangwe alikutwa na umauti akiwa na umri wa miaka 53 ya uhai wake hapa duniani. Alizaliwa Julai 15, 1956 katika kijiji cha Kemakorere wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Historia ya maisha yake inaonyesha kuwa, Marehemu alipata elimu ya msingi shule ya Rosana mwaka 1962 hadi mwaka 1969, na baadaye alijiunga Shule ya Sekondari ya Kinondoni Muslim Dar es Salaam kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne mwaka 1970 mpaka 1973 kabla ya kujiunga sekondari ya Mkwawa Mkoani Iringa kwa masomo ya kidato cha tano na sita mwaka 1975 mpaka mwaka 1976.

Baada ya hapo alijiunga Chuo kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978 mpaka mwaka 1979 akichukua masomo ya shahada ya sanaa kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Bremen, Humburg, Ujerumani alipochukua Stashahada katika fani ya Lugha za Kifaransa, Kiingereza na Kijerumani hadi kufikia mwaka 1985.

Kwakuwa aliamini katika utamaduni wa kujielimisha siku zote kila alipopata fursa, Marehemu aliamua kuendelea kujiendeleza kielimu baada ya kuwa Mbunge, ambapo mpaka anafariki dunia alikuwa mwanafunzi wa Shahada ya Sheria (LLB) Chuo kikuu huria cha Tanzania (OUT).

Katika maisha yake yote hapa duniani alikuwa mwanaharakati mwenye msimamo na kutenda katika aliyoyaamini, hali iliyomfanya achaguliwe kuwa Diwani wa Tarime mwaka 2000 mpaka 2005, na kisha kuchaguliwa kuwa Diwani na Mbunge mwaka 2005 mpaka mauti yalipomkuta Julai 28,2008.

Pamoja na nafasi zote hizo alizopata kuaminiwa katika jamii alimoishi, Marehemu amewahi kufanya kazi za utendaji. Mwaka 1996 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya LACOP Interservices Co Ltd kuanzia mwaka 1996 mpaka mwaka 2007.

Akiwa Mbunge, Pamoja na Harakati zake za kutetea wanyonge na wasio na fursa jimbo la Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla, hususan wachimbaji wenye mitaji midogo. Mh Chacha Zakayo Wangwe alianzisha Asasi ya kusimamia maendeleo jimbo la Tarime ijulikanayo kama; Tarime Development Iniative Programme (TADI) kuanzia mwaka 2006 mpaka alipokutwa na umauti.

Katika uhai wake, Marehemu alikuwa muumini wa harakati za kisiasa kupitia vyama. Katika medani za siasa , Marehemu alikuwa mwanachama wa TANU Youth League (TYL) tangu mwaka 1975 na baadae CCM kabla ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi Tanzania mwaka 1992, ambapo alijiunga na kilichokuwa Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania, wakati huo NCCR-Mageuzi na kufanikiwa kuwa Diwani kwa tiketi ya chama hicho na baadae kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.

Baada ya kujiunga CHADEMA mwaka 2002, Marehemu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mara mwaka 2003, ambapo kutokana na juhudi zake za kusimamia mabadiliko makubwa ya kisiasa, alifanikiwa kushinda udiwani na Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.

Wadhifa wa juu aliopata kuushika kisiasa mpaka alipokutwa na umauti ni kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA. Marehemu alichaguliwa kuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti kwa Tanzania Bara Disemba mwaka 2007.

Ni wazi kwamba haikuwa rahisi kwa marehemu kufikia mafanikio hayo makubwa kisiasa nje ya vikwazo hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa mwanasiasa aliyeamini katika falsafa ya ukombozi na nguvu ya umma katika mageuzi ya kisiasa. Ni katika msingi huo, marehemu amekabiliwa na changamoto za kesi zaidi ya kumi na hata kufungwa mwaka mmoja na miezi minne mwaka 2004 alipokuwa akitetea wazawa wa Tarime kwa kupinga mpango wa serikali ya CCM kuwahamisha kinyama wakazi wa Tarime wenye makazi yao maeneo ya migodini. Ni kutokana na msimamo wake usioyumba katika kutetea haki za wananchi wanyonge ilifikia mahali wananchi wa Tarime wakampa jina la MANDELA.

Pamoja na kutumia muda wake mwingi katika harakati za ukombozi, marehemu hakusahau mila na desturi za kiafrika zinazohimiza umuhimu na nafasi ya familia kwa maisha ya mwanadamu. Mpaka mauti yanamkuta, marehemu alikuwa na wake watatu; Jacquiline Chacha Wangwe, Dotto Chacha Wangwe na Mariam Chacha Wangwe. Kwa ujumla marehemu ameacha watoto 10, wakiume wanne na wakike watano.

Kama alivyopata kujibainisha mwenyewe, Marehemu alikuwa mwanasiasa na mwanaharakati mwenye msimamo katika yale aliyoyaamini, na siku zote hakuyumba katika kuyasimamia. Akiwa Makamu Mwenyekiti, Marehemu aliamini kuwa CHADEMA kinayo fursa ya kushinda vijiji, kata, na majimbo mengi zaidi kabla ya kushinda Urais na kuchukua dola ili kumkomboa mtanzania dhidi ya umasikini ambao aliamini kuwa ulisababishwa na chama kilichoko madarakani hivi sasa. Na hiyo ndio Changamoto kwetu, katika kuleta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli.

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl