Utangulizi
Ndugu Wana habari mnafahamu kuwa CHADEMA kwa niaba ya vyama vilivyopo kwenye Ushirikiano kilimsimamisha Ndugu
Victor Kimesera kuwa mgombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiteto unaotegemea kufanyika Februari24,2008.
Aidha; Yamejitokeza matukio mbalimbali tangu kuzindua kampeni ambayo ni muhimu Umma ukaendelea kufahamishwa kwakuwa yanahusu tukio muhimu kwa mchakato wa Demokrasia na Maendeleo nchini.
Katika kutimiza wajibu huo, Leo tumewaita kuzungumzia matukio makubwa mawili kuhusu kile kinachoendelea huko Kiteto; kwanza ni tukio la wafuasi wa CCM wakishirikiana na polisi kuwavamia na kuwajeruhi vibaya viongozi wa CHADEMA walioko kwenye kampeni Kiteto pamoja na Uamuzi wa Tume ya Uchaguzi kukizuia CHADEMA kutotumia watu wake wanaotoka nje ya Kiteto kwa ajili ya kazi ya uwakala siku ya uchaguzi.
Kuhusu viongozi wa CHADEMA kuvamiwa na kujeruhiwa
CHADEMA tumesikitishwa sana na vitendo vinavyofanywa na wafuasi wa CCM kwa kushirikiana na Polisi kuendesha uharamia katika mchakato wa kidemokrasia kama uchaguzi. Tunaamini kuwa tukio hili ni pigo kwa harakati za demokrasia nchini hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Kikwete imekuwa ikidai kuimarisha Demokrasia na mahusiano na vyama vya upinzani.
Na ni kwa sababu hiyo tunawaomba wapenda Demokrasia na Maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na Wanaharakati wa Haki za Bindamu, Viongozi wa dini, Vyombo vya Habari, na wadau wengine wa Demokrasia nchini kulaani uharamia huu kwa imani kuwa kilichofanywa na Wafuasi hao wa CCM kwa kushirikiana na polisi ni aibu kwa Demokrasia nchini na hasa kwa Chama Cha Mapinduzi ambacho niwazi kimekuwa kikiwatumia vijana hao kwa mwavuli wa Greenguard.
Pamoja na kuitaka serikali iwakamate watu wote waliotajwa kuhusika na tukio hili wakati uchunguzi unaendelea, Tunapenda kusisitiza kuwa tukio hili limedhihirisha madai yetu ambayo tumekuwa tukisisitiza wakati wote kuwa CCM ni Chama Cha watu wasio na ustaarabu na waumini wa vurugu kila wanapobaini kuwa wanaelekea kushindwa. Na ni kwa misingi hiyo kama chama tunaendelea kuongeza nguvu kuhakikisha wananchi wanampata kiongozi wanayemtaka kwa maslahi ya wanakiteto na bila kuogopa matendo ya kiharamia yanayoendeshwa huko.
Kuhusu uamuzi wa Tume
Tunapenda kuwafahamisha kuwa baada ya uamuzi wa CHADEMA kuamua kuwatumia wanachama na viongozi wetu wakiwemo Dk Willbrod Slaa, Zitto Kabwe, Grace Kiwelu pamoja na viongozi wengine wa Kamati kuu na Baraza kuu katika kusimamia uchaguzi, katika hali isiyotarajiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimwelekeza msimamizi wa Uchaguzi kiteto kuzuia mawakala kutoka nje ya kata husika za uchaguzi.
Baada ya kuwasiliana na Mwanasheria wa Tume ya Taifa ya uchaguzi na kujiridhisha kuwa uamuzi huo ulitoka juu kwa maana ya tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jana Februari 18, 2008 tuliiandikia barua Tume ya taifa ya Uchaguzi kuieleza kuwa uamuzi huo hauendani na sheria wala taratibu za uchaguzi na hivyo ni kinyume na misingi na matakwa ya uchaguzi na kuitaka ibatilishe uamuzi huo mara moja na taratibu za msingi tu kuhusu uchaguzi ndio zizingatiwe.
Tunafahamu kuwa kesho tume ya Taifa ya Uchaguzi itafanya kikao kujadili kadhia hii, lakini kama Chama tunapenda kusisitiza msimamo wetu kuwa tumeshangazwa na kushtushwa mno na uamuzi wa tume ya taifa ya uchaguzi ambayo inapaswa kusimamia sheria na taratibu za uendeshaji uchaguzi inapogeuka kuwa chanzo na kinara wa kuingiza taratibu zisizo rasmi, zisizopatikana katika Katiba, Sheria, Kanuni wala Maadili ya uchaguzi katika mchakato nyeti kama huu.
Mwisho
CHADEMA tunapenda kutoa rai kwa wanaCHADEMA, na wananchi kwa ujumla kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo viongozi wetu waliojeruhiwa wanaendelea kuapata matibabu na hali zao zikiendelea vizuri. Tunawaomba wasikatishwe tamaa na matukio ya aina hii kwakuwa ndio changamoto za kusaka mabadiliko ya Kweli na Uhuru wa kweli hasa katika mazingira ya sasa ambapo tunapambana na Chama kisichoheshimu hata uhai wa binadamu wenzao.
Imetolewa na;
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana na Kaimu Katibu Mkuu.