lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

7 Januari 2008

Vijana CHADEMA tunalaani shambulio kwa Waandishi

  1. Vijana wa Tanzania wasikubali kutumika na mafisadi kufanya uhalifu
  2. Vyombo vya dola vichunguze wahusika wakuu na kusudio la shambulizi
  3. Ni uvamizi dhidi ya haki ya kikatiba ya kupata na kutoa habari
  4. "Kalamu za Wanahabari zina nguvu kuliko upanga wa mafisadi"

Kwa niaba ya Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), vijana wa CHADEMA tunaungana na wapenda haki na ukweli kote nchini kutoa pole kwa wanahabari Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage kwa kushambuliwa kwa mapanga na tindikali. Mwenyezi Mungu awawezeshe kupona haraka waweze kurejea katika majukumu yao ya kulijenga na taifa na kwa namna ya pekee tunaziombea familia zako utulivu katika kipindi hiki.

Aidha tunalaani vikali uvamizi na shambulizi hili dhidi ya wahabari hawa na ofisi yao wakiwa katikati ya jukumu la kuandaa toleo la gazeti kwani ni shambulizi dhidi ya binadamu na juu ya haki ya kikatiba ya kupata na kutoa habari.

Kutokana na mtiririko wa matukio na ushahidi wa kimazingira, tungependa tukio hili lisichukuliwe kama vitendo vya kawaida vya ujambazi bali lichunguzwe kama kitendo cha kigaidi na uharamia dhidi ya waandishi wa habari, uandishi wa habari na chombo cha habari. Si wajibu wa wananchi kuhukumu, na ni mapema mno kuhusisha moja kwa moja tukio hili na 'mtu' au 'watu fulani'. Hata hivyo, kwa mtiririko wa matukio na ushahidi wa kimazingira ni rahisi kutuhumu kuwa upo uwezekano mkubwa wa uvamimizi na shambulizi hili kuwa limefanywa na baadhi ya mafisadi wakiwatumia vijana kufanya tendo hili la kifisadi.

Wanahabari hawa na chombo chao wamekuwa mstari wa mbele kwa uwazi bila woga katika mapambano dhidi ya ufisadi na kutetea rasilimali za taifa, na kuwa sehemu ya mashujaa wa habari nchini. Mwanahalisi ni moja ya magazeti ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kuandika tuhuma za ufisadi na/au matumizi mabaya ya madaraka zinazowakabili viongozi kadhaa wa serikali, makampuni na taasisi mbalimbali.

Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwaka jana vyombo mbalimbali vya habari viliandika kuhusu vitisho vinavyotolewa kwa chombo hicho cha habari na vyombo vyake. "Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti hilo, Saed Kubenea, ilieleza kuwa kuna mienendo ya chinichini ya kusambaza vitisho kwa vyombo vya habari hususan MwanaHalisi, wachapishaji wake, wahariri, waandishi na wachangiaji wa makala na taarifa mbalimbali.(Rejea Tanzania Daima-28/9/2007). Hilo lilikuja baada ya gazeti hilo kuandika habari na kuweka hadharani majina ya waliotajwa kwenye 'orodha ya mafisadi'.

Pamoja na kuwa jeshi la polisi limetangaza kuwatafuta watuhumiwa vijana watatu waliohusika na uvamizi huu; tungependa kutoa rai kwa vyombo vya dola kwamba jitihada za uchunguzi zielekezwe katika kuwaibaini pia waliowatuma vijana hawa kufanya uhalifu huo. Katika mazingira ya wahalifu vijana wa kawaida, ni vigumu kuhusisha jitihada za kulenga mwanahabari na kummwagia tindikali machoni, hali ambayo inaashiria shambulizi hili ni la kutumwa na 'mtu' ama 'mtandao Fulani wa watu'. Kadhalika, pamoja na kuwatafuta wahusika, vyombo vya dola vichunguze kusudio hasa ya shambulio hilo - kama nia ilikuwa ni kuwadhuru waandishi hawa siku hiyo ili habari Fulani isitoke au ni kisasi kutokana na habari Fulani ambayo chombo hicho kimekuwa kikiandika. Uchunguzi kamilifu kama huu na hatua zitakazochukuliwa kutokana na uchunguzi huo ni muhimu katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari na kulinda maisha ya wanahabari hapa nchini.

Kama kweli shambulio hili limefanywa na watuhumiwa hao kwa kutumwa na 'fisadi' ama 'mtandao Fulani wa mafisadi' wanaotapatapa, basi tunasikitishwa na pia na jinsi ambavyo 'habari' na 'mwanahabari' wanavyochukuliwa. Tunakumbusha kuwa mwanahabari ni mjumbe tu wakufikisha ujumbe katika jamii; ambaye anapaswa kulindwa na kuheshimiwa. Tabia inayoanza kuchipua ya kumshambulia mjumbe au chombo kilichofikisha ujumbe tena kwa njia ambazo ni kinyume cha sheria na ustaarabu wa binadamu badala ya kuushughulikia ujumbe wenyewe; ikiachwa ikashamiri inaweza ikatishia ufanisi wa sekta ya habari ambayo inapaswa kudumishwa kama mhimili wa nne wa dola.

Serikali ni vyema ikalichukulia suala hili kwa uzito wake, kwani vitendo kama hivi vya wanahabari kushambuliwa vikiendelea vinaweza kuhamia kwa watetezi wengine wa haki; na hali hii ikiachwa itazalisha chuki miongoni mwa jamii na hatimaye jamii itaanza kutoa hukumu ya umma (mob justice) kwa wanaotuhumiwa kufanya vitendo kama hivi vya kifisadi.

Aidha tunachukua fursa hii kutoa mwito kwa vijana kote nchini kutokubali kutumika kufanya vitendo vya uhalifu, na tunatoa rai kwa jamii kuwataja wanaowatumia vijana kufanya vitendo hivyo vya kinyama. Fisadi yoyote aliyetayari kuyaweka rehani maisha ya watanzania waliowengi kwa ufisadi wake hawezi kushindwa kuweka hatarini maisha ya mtanzania mmoja ambaye anachimbua ufisadi wake na kumweka katika mstari kuhukumiwa; hivyo vijana wasikubali kuingia katika mtego huu wa kufanya kazi za mafisadi. Mwisho, tunawaomba vijana wote nchini wakiwemo vijana wanahabari kuendeleza harakati za kutetea haki na ukweli kwa kutumia uandishi wenye kuchochea fikra mbadala zenye kuleta demokrasia na maendeleo nchini. Vitisho visirudishe nyuma uandishi wa habari wenye kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za Taifa kwani "kalamu za wanahabari zina nguvu kuliko upanga wa mafisadi"

John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl