lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner
Mengineyo
»Matamko mengine
»Habari Mpya
»Makala mbalimbali
»Midahalo
»Blogu za wanachama
»Picha za matukio
»Maoni Yenu
b.part
Barua Pepe
jina la mtumiaji:
neno-siri
rt.bt.spc
bt.part2

VIONGOZI WA UMMA WALIOKO KATIKA ORODHA HII WAMEKIUKA NA/AU KUVUNJA MASHARTI YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO NA SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA KAMA IFUATAVYO:

A. WALIOSHIRIKI MOJA KWA MOJA KATIKA VITENDO VYA UFISADI

1. DR. DAUDI T.S. BALALI

Dr. Daudi Balali amekuwa na bado ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania tangu mwaka 1997. Katika kipindi hicho cha miaka kumi, Gavana Balali amehujumu taifa la Tanzania kama ifuatavyo:

  1. Kufuatana na barua ya wataalamu wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, ameruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia ufujaji wa fedha za umma unaodaiwa kufikia Shilingi 522, 459, 255,000 katika ujenzi wa majengo ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyoko barabara ya Mirambo, Dar es Salaam na Gulioni, Zanzibar. Aidha taarifa kutoka vyanzo vingine zinaonyesha kwamba mwaka 1998 kampuni ya Skanska Jensen ya Sweden ilituhumiwa kutoa hongo ya Dola za Marekani milioni 5 kwa Gavana Balali tuhuma zilizopelekea kampuni hiyo kupigwa marufuku kushiriki tenda ya ujenzi wa majengo hayo. Hata hivyo, katika mazingira yanayoashiria ufisadi mkubwa, kampuni ya Group 5 ya Afrika ya Kusini ambayo ni kampuni tanzu ya Skanska Jensen ilipewa tenda ya kujenga majengo hayo ya Benki Kuu;

  2. Kufuatana na barua iliyotajwa katika aya ya (i) hapo juu, Gavana Balali aliidhinisha na/au kuruhusu na/au kunyamazia malipo ya Dola za Marekani 118,396,460.36 zilizopelekwa katika akaunti isiyojulikana ya Benki ya Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini kama malipo ya madeni ya kampuni muflisi ya Meremeta Ltd. iliyokuwa inachimba dhahabu katika eneo la Buhemba wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara. Kwa miaka mingi Serikali ilikuwa ikitoa taarifa za uongo kwamba Meremeta Ltd. ilikuwa ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya mradi wake wa Nyumbu, Kibaha, Mkoa wa Pwani. Hata hivyo, nakala ya usajili iliyotolewa na Msajili wa Makampuni wa Uingereza na Wales inaonyesha kwamba kampuni hiyo iliandikishwa nchini Uingereza tarehe 19 Agosti 1997 na ilifilisiwa huko huko Uingereza tarehe 10 Januari 2006. Aidha, taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ya tarehe 31 Mei 2005 inaonyesha kwamba Meremeta Ltd. ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania kama tawi tarehe 3 Oktoba, 1997. Vile vile taarifa hiyo inaonyesha kwamba hisa 50 za Meremeta Ltd. zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini na hisa 50 zilizobaki zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa kupitia kwa Msajili wa Hazina katika Wizara ya Fedha. Inajulikana vile vile kwamba Gavana Balali aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Meremeta Ltd. kati ya mwaka 2004 na 2005. Hata hivyo, kuna utata mkubwa juu ya nani ni mmiliki hasa wa Meremeta Ltd. kwa kuwa taarifa ya BRELA inaonyesha pia kwamba makampuni mawili ya Kiingereza – London Law Services Ltd. na London Law Secretarial Ltd. – nayo yanamiliki hisa moja moja za Meremeta Ltd. Makampuni hayo yanatumia anwani moja iliyoko 84 Temple Chambers, Temple Avenue, jijini London. Haijulikani ni kwanini Gavana Balali aliruhusu fedha za umma kutumika kulipia madeni yote ya kampuni ambayo Serikali ilikuwa inamiliki hisa 50 tu wakati makampuni mengine ya kigeni yalikuwa yanamiliki hisa 52. Na kama ilivyosema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, uhalali wa Serikali kulipa madeni ya Meremeta Ltd. kwa Nedbank Ltd. badala ya kuiacha benki hiyo kudai malipo hayo kutoka kwa mfilisi wa kampuni hiyo sawa na wadeni wengine haujulikani;

  3. Kufuatana na barua ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu, Gavana Balali aliruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia malipo ya Dola za Marekani 13,736,628.73 kwa kampuni ya Tangold Ltd. Katika hotuba yake Bungeni ya tarehe 27 Juni 2007, Waziri wa Madini na Nishati Mheshimiwa Nazir Karamagi alidai kwamba “… mali na madeni ya MEREMETA yamehamishiwa kwenye kampuni mpya ya TANGOLD ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.” Hata hivyo, barua ya BRELA ya tarehe 4 Julai 2007 inatamka wazi kwamba “Tangold Limited ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Mauritius, na baadae kuandikishwa nchini Tanzania kama tawi la kampuni ya kigeni.” Barua hiyo inaongeza kwamba kampuni hiyo ilipewa hati ya kutimiza masharti ya Tanzania mnamo tarehe 20 Februari 2006 na kwamba Katiba ya kampuni hiyo haikuonyesha “majina ya wanahisa wa kampuni na mgawanyo wa hisa.” Barua hiyo ya BRELA inaonyesha kwamba wakurugenzi wa Tangold Limited ni pamoja na Gavana Balali, Gray S. Mgonja ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Andrew J. Chenge ambaye ni Waziri wa sasa wa Miundo Mbinu, Patrick W.R. Rutabanzibwa ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Vincent F. Mrisho ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha fomu Na. 1F inayohusu usajili wa kampuni za kigeni iliyowasilishwa BRELA na mawakili wa Tangold Limited na kusainiwa na Gavana Balali tarehe 20 Mei 2005 inaonyesha kwamba kampuni hii imetokea “Jamhuri ya Mauritius” na anwani yake iko Suite 520, Barkly Wharf, Le Caudan, Waterfront, Port Louis, Mauritius. Hivyo ndivyo kinavyoonyesha cheti cha usajili kilichotolewa na Msajili wa Makampuni wa Jamhuri ya Mauritius mnamo tarehe 5 Aprili 2005 na pia leseni ya biashara iliyotolewa kwa Tangold Ltd. Port Louis nchini Mauritius tarehe 8 Aprili 2005. nyaraka hizi pia zinaonyesha kwamba Tangold Limited ni kampuni binafsi (private company limited by shares). Kuna utata zaidi kwani kifungu cha 7(e) cha Katiba ya Tangold Ltd. kinaruhusu hisa za wanaomiliki kampuni hiyo binafsi kuhamisha hisa zao kwa wanandoa, baba, mama, watoto, wajukuu au wakwe zao wa kike au wa kiume! Sasa kama ni kweli kwamba Tangold Ltd. inamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia mia moja, je nani ni mke au mume au baba au mama au motto au mjukuu au mkwe wa kike au wa kiume wa Serikali ya Tanzania ambaye anaweza kuhamishiwa hisa za kampuni hiyo? Katika barua yake ya ukaguzi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu alidai kwamba Ofisi yake ilishindwa kuelewa uhalali wa malipo ya dola za Marekani 13,340,168.37 yaliyofanywa na Benki Kuu kwa Tangold Limited;

  4. Gavana Balali aliruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia mkopo usio na riba wa Dola za Marekani 5,512,398.55 kwa kampuni ya Mwananchi Gold Co. Ltd. kati ya mwaka 2004 na tarehe 30 Juni 2006. Kati ya fedha hizo, deni la dola 2,807,920 limedhaminiwa kwa dhahabu ghafi ambayo ingenunuliwa kutokana na fedha za mkopo zilizotolewa na Benki Kuu yenyewe! Kwa maana rahisi ni kwamba kampuni ya Mwananchi Gold haijatoa dhamana yoyote inayoeleweka kwa mabilioni ya shilingi ilizokopeshwa na Benki Kuu chini ya Gavana Balali. Kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, hadi kufikia mwezi Desemba 2006 Mwananchi Gold Co. Ltd. ilikuwa imeshindwa kulipa hata riba ya mkopo huo kwa kiasi cha dola za Marekani 62,847.91. “Katika mazingira haya”, inasema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, “hatukuweza kujiridhisha kwamba deni la dola la Marekani 5512398.55 inalodaiwa (Mwananchi Gold Co. Ltd.) hadi kufikia tarehe 30 Juni 2006 linaweza kulipika.” Je, ni kampuni gani hii iliyopewa mamilioni ya fedha za umma katika fedha za kigeni bila kudaiwa riba au kupewa kipindi maalumu cha kulipa mkopo huo? Kufuatana na taarifa za BRELA, Mwananchi Gold Co. Ltd. ni kampuni binafsi ambayo wanahisa wake ni Benki Kuu ya Tanzania yenye hisa 500, Shirika la Maendeleo la Taifa (hisa 500), Mwananchi Trust Co. Ltd. (hisa 1,123) na Chimera Co. Ltd. (hisa 500). Kampuni hii ilisajiliwa kama kampuni binafsi tarehe 12 Desemba 2002. Mawakili wake ni kampuni ya mawakili ya Nyalali, Warioba & Mahalu Associates ikiwashirikisha aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania wakati huo marehemu Francis L. Nyalali, Waziri Mkuu wa zamani Joseph Sinde Warioba na aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa R. Mahalu. Wakurugenzi wa Mwananchi Gold ni Joseph Sinde Warioba, Gavana Daudi Balali, Col. J. Simbakalia, Vulfrida Grace Mahalu, Yusuf H. Mushi na raia wawili wa Italia, Paolo Cesari na Patrizio Magrini. Vulfrida Mahalu ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa kampuni binafsi ya VMB Holdings (1996) Ltd. na pia ni mke wa Profesa Mahalu ambaye kwa sasa anakabiliwa na tuhuma za kuhujumu uchumi kutokana na madai ya wizi wa zaidi ya shilingi bilioni tatu za Serikali wakati akiwa balozi wa Tanzania nchini Italia! Kanali Simbakalia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Taifa na Yusuf Mushi ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni binafsi ya Business Machines Consultants (T) Ltd;

  5. Gavana Balali aliruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia malipo ya shilingi 131,950,750,000 kwa watu wasiojulikana wanaodaiwa kuingiza fedha za kigeni nchini. Vile vile Gavana Balali anadaiwa kuidhinisha malipo ya shilingi bilioni 4,228,658,000 kwa watu wasiojulikana wanaodaiwa kuingiza fedha za kigeni nchini. “Katika mazingira haya”, inasema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, “hatukuridhika na uhalali wa hasara ya shillingi bilioni 131.9 zinazoonekana katika taarifa za fedha hadi kufikia tarehe 30 Juni 2006….” Kwa mantiki hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu aliiasa Benki Kuu kuanzisha uchunguzi wa malipo yaliyosababisha hasara ya shilingi 131,950,750,000 na shilingi 4,228,658,000 zilizolipwa kama malipo ya madeni ya nje. Waziri wa Fedha Zakia Meghji mwenyewe amekiri kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma katika akaunti za malipo ya madeni ya nje katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). IMF yenyewe katika taarifa kwa vyombo vya habari ya tarehe 27 Juni 2007 imetamka kwamba “Serikali (ya Tanzania) imekwisha kusimamisha malipo kutoka akaunti hiyo hadi uchunguzi huo utakapokamilika.” Wakati Serikali ikitoa taarifa hizi kwa IMF imekataa kata kata kutoa taarifa hizi kwa umma wa Watanzania wala wawakilishi wao Bungeni.
rudi...     inaendelea...

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl