Nazir Mustafa Karamagi ni Waziri wa sasa wa Nishati na
Madini. Aliingia kwa mara ya kwanza katika Baraza la
Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete kama Waziri wa
Biashara, Viwanda na Masoko. Lakini kufuatia Kashfa ya
Umeme wa Richmond iliyomwondoa Waziri wa Nishati na
Madini wa wakati huo Dr. Ibrahim Msabaha na Naibu wake
Lau Masha, Mheshimiwa Karamagi alihamishiwa Wizara ya
Nishati na Madini. Katika kipindi cha karibu mwaka
mmoja ambao Mheshimiwa Karamagi ameshikilia madaraka
yake ya sasa amehujumu taifa la Tanzania kwa kusaini
mkataba wa ujenzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi
wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga na kampuni ya Pangea
Minerals Limited ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick
Gold Corporation ya Canada. Mkataba huo ulisainiwa
Churchill Hotel, London, Uingereza tarehe 17 Februari
2007. Kwa vile kusainiwa kwa Mkataba huo ndio ulikuwa
chimbuko la hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge
iliyopelekea Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mheshimiwa
Zitto Z. Kabwe kusimamishwa kufanya shughuli za Bunge
kwa miezi mitano, ni vema madhara na/au manufaa ya
kiuchumi, kijamii na kisiasa ya Mkataba huo kwa
Tanzania yachunguzwe kwa makini kama ifuatavyo:
I. MUDA WA MKATABA
(i) Kwamba Waziri Karamagi atatoa Leseni Maalum ya
Uchimbaji kwa Pangea Minerals ya muda wa kuanzia wa
miaka ishirini na tano (25). Leseni hiyo itatolewa
haraka iwezekanavyo na kwa vyovyote vile ndani ya muda
usiozidi siku sitini (60) tangu Pangea Minerals
kuwasilisha maombi yao ya Leseni Maalum ys Uchimbaji.
Aidha, Pangea Minerals ". watakuwa na uhuru wa
kuongeza muda wa Leseni hiyo kwa masharti hayo hayo
kwa miaka mingine ishirini na tano (25)." Na endapo
muda huo wa nyongeza ukiisha na Pangea Minerals
wakaomba kuongezewa muda zaidi, ". basi iwapo Waziri
ataona ni kwa maslahi ya taifa kuwaongezea muda kama
walivyoomba atawaongezea muda wa ziada atakaoona
unafaa." Kwa masharti haya ya mkataba, Pangea Minerals
wana haki ya kuendelea kuchimba dhahabu kwa miaka
hamsini au zaidi kufuatana na mahitaji yao na matakwa
ya Waziri wa Nishati na Madini na kwa masharti yale
yale yaliyowekwa siku ya kusaini mkataba;
II. MAPATO YA SERIKALI
Mkataba wa Buzwagi unadai kwamba "Kampuni inachukulia
suala la kutobadilika badilika kwa kodi na sheria za
fedha za Tanzania kama sharti la msingi katika
uwekezaji wake kwenye Mgodi na kwamba Kampuni itakuwa
na uhakika kwamba kodi na utaratibu wa kifedha ulivyo
wakati wa kusaini Mkataba utaendelea kuwa hivyo kwa
Kampuni wakati wote wa uhai wa Mradi" wa Buzwagi.
Katika kuhakikisha suala hili, Mkataba huu umeweka
masharti yafuatayo kuhusiana na masuala ya kodi na/au
ya kifedha:
(i) Kwamba Pangea Minerals watalipa kwa Serikali kodi
zifuatazo:
(a) Asilimia 3 (3%) thamani ya madini baada ya kuondoa
gharama za uzalishaji kama mrahaba kwa madini yote
yatakayochimbwa eneo la Buzwagi isipokuwa almasi
ambayo mrahaba wake utakuwa asilimia 5 (5%) ya thamani
ya almasi hiyo baada ya kuondoa gharama za uzalishaji;
(b) Ushuru wa stempu (stamp duty) kama ulivyoainishwa
na Sheria ya Ushuru wa Stempu Na. 20 ya Mwaka 1972
kuanzia tarehe ya kuanza kwa mkataba wa Buzwagi. Hata
hivyo, kuna uwezekano wa Pangea Minerals kutolipa hata
senti moja kama ushuru wa stempu kwani kifungu cha
5(1) cha Sheria ya Ushuru wa Stempu kimetoa angalizo
kwamba "hakuna ushuru wowote utakaolipwa kutokana na
waraka (instrument) wowote uliosainiwa na, au kwa
niaba au kwa taarifa ya Serikali ambapo kama kifungu
hiki kisingekuwapo, basi Serikali ingekuwa na wajibu
wa kulipa ushuru huo kuhusiana na waraka huo. Neno
'instrument' limetafsiriwa kuwa linajumuisha "kila
nyaraka ambayo kwayo haki au deni/wajibu
l/imetengenezwa au imedaiwa kutengenezwa au
kuhamishwa, kupunguzwa, kuongezwa, kufutwa au
kurekodiwa." Kwa tafsiri hii, ni wazi kwamba Mkataba
wa Buzwagi ni 'waraka' (instrument) ambao kwayo haki
na wajibu wa Serikali na Pangea Minerals
imetengenezwa, kuhamishwa na/au kurekodiwa;
(c) Dola za Marekani laki moja na ishirini na tano
elfu (US$ 125,000) kwa ajili ya Mfuko wa Uwezeshwaji
(Empowerment Fund) zitakazolipwa kila tarehe 31
Desemba ya kila mwaka kuanzia mwaka wa uzalishaji. Ni
muhimu kuelewa hapa kwamba 'Mwaka wa Uzalishaji'
umetafsiriwa katika mkataba huu kuwa ni kipindi ambapo
uzalishaji wa dhahabu safi au isiyosafishwa utafikia
kiasi cha wakia 20,000. Kwa maana nyingine Pangea
Minerals hawawajibiki kulipa kodi ya Mfuko wa
Uwezeshwaji iwapo uzalishaji wa dhahabu hautafikia
wakia 20,000 kwa mwaka;
(ii) Kwamba kodi yoyote, ushuru wowote, ada yoyote au
malipo mengine ambayo Kampuni, wenye hisa wake,
washirika au wadeni wake watatakiwa kulipa kutokana na
mapato, ikiwa ni pamoja na mapato ya gawio, yatokanayo
na uchimbaji madini unaofanyika chini ya Leseni Maalum
ya Uchimbaji vitalipwa kuanzia tarehe ya mkataba
kufuatana na matakwa ya Sheria ya Kodi y Mapato ya
mwaka 2004 na Sheria ya Ushuru wa Forodha ya mwaka
1976. Ni muhimu kuelewa hapa kwamba Sheria hizo mbili
zilifanyiwa marekebisho makubwa na Sheria ya
Mabadiliko ya Sheria za Fedha Na. 27 ya mwaka 1997.
Chini ya marekebisho hayo kodi, ushuru au ada
zinazozungumziwa katika kifungu hiki cha Mkataba
ziliondolewa au kupunguzwa kwa kiasi kikubwa au
kufanywa kuwa tegemezi wa wakati makampuni ya madini
yatakapoanza kupata na/au kutangaza faida. Kwa maana
nyingine, Serikali inaweza isipate fedha yoyote
kutokana na kifungu hiki cha Mkataba wa Buzwagi;
(iii) Kwamba kiwango cha jumla ya kodi zote ambazo
Pangea Minerals italipa kwa halmashauri za wilaya au
serikali za mitaa kwa ujumla hakitazidi Dola za
Marekani laki mbili US$ 200,000) kwa mwaka. Aidha
Kampuni haitalipa kodi za halmashauri na/au serikali
za mitaa:
(a) ambazo zinazidi viwango vya sehemu nyingine za
Tanzania;
(b) ambazo zimetokana na faida, mauzo au uzalishaji
unaotokana na uchimbaji madini; au
(c) ambazo zimetokana na thamani ya ardhi inayotumika
kama mgodi, kwa miundombinu ya uchimbaji madini au
mitambo;
(iv) Kwamba Pangea Minerals haitawajibika kulipa kodi
zifuatazo kutokana na shughuli zake za uchimbaji
madini:
(a) Ushuru, ada au mchango wowote wa lazima zaidi ya
vile ilivyoelezwa katika aya ya (iv) isipokuwa kwa
kodi, ushuru, ada au michango midogo midogo ambayo kwa
pamoja haitazidi Dola za Marekani elfu kumi (US$
10,000) kwa mwaka;
(b) Malipo yatozwayo chini ya Sheria ya Madini au
kanuni zake yanayozidi Dola za Marekani elfu mbili
(US$ 2,000) kwa kilometa ya mraba kwa mwaka. Kwa maana
hiyo, kodi ya kiwanja inayotakiwa kulipwa kwa eneo
lote la Mkataba wa Buzwagi lenye ukubwa wa kilometa za
24.49 ni Dola za Marekani elfu arobaini na nane mia
tisa na themanini (US$ 48,980) kwa mwaka;
(c) Kodi ya matumizi ya barabara iliyowekwa na Sheria
ya Kodi za Mafuta na Barabara ya mwaka 1985
itakayozidi Dola za Marekani laki mbili (US$ 200,000)
kwa mwaka;
(d) Kodi yoyote ya mauzo, matumizi au ongezeko la
thamani isipokuwa kama ilivyowekwa chini ya Sheria ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 1997. Hapa vile
vile ni muhimu kuelewa kwamba Sheria Na. 27 ya mwaka
iliyofanya marekebisho ya sheria mbali mbali za fedha
iliondoa kabisa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa
mauzo ya madini yote yanayouzwa nje ya Tanzania kama
dhahabu au almasi, n.k. Ndio maana kifungu hiki cha
Mkataba wa Buzwagi kimesema wazi kwamba Pangea
Minerals ina haki ya kunufaika na nafuu za VAT
zilizopo katika Nyongeza ya Tatu ya Sheria ya VAT
kuanzia tarehe ya Mkataba;
(v) Kwamba Pangea Minerals italipa kodi ya zuio
(withholding tax) kutokana na malipo kwa watu wengine
kama inavyotakiwa na sheria husika, isipokuwa Kampuni
haitawajibika kushikilia kodi:
(a) Kwa kiwango chochote kutokana na malipo ya mkopo
au deni la riba inayotakiwa kulipwa kwa fedha za
kigeni kwa ajili ya mikopo, ikiwa ni pamoja na mikopo
ya washirika wake, iliyokopwa nje ya Tanzania kwa
ajili ya shughuli za uchimbaji madini. Kwa maana
nyingine, malipo ya mikopo mikubwa ambayo makampuni ya
madini yamekuwa yanadai kulipa kwa wadeni wao wa nje
na kwa hiyo kushindwa kupata faida ya kulipa kodi ya
mapato kwa Serikali ya Tanzania nayo haitalipiwa kodi
ya zuio;
(b) Kwa kiwango chochote kinachozidi asilimia 5 ya
malipo ya jumla kuhusiana na huduma za kiutaalamu au
ada za menejimenti;
(vi) Pale ambapo asilimia 5 ya malipo ya jumla kwa
ajili ya huduma za kiutaalamu au ada ya menejimenti
inashikiliwa na Pangea Minerals imezuiliwa, kodi hiyo
ya zuio itahesabika kuwa ni sawa na malipo yote ya
kodi ya mapato inayotakiwa kulipwa na mtu anayetoa
huduma za kiutaalamu au menejimenti. Maana ya kifungu
hiki ni kuwawezesha watoa huduma za kiutaalamu au
menejimenti kutolipa kodi ya mapato ambayo kisheria ni
asilimia 30 ya mapato yao;
(vii) Kwamba Pangea Minerals itaruhusiwa kukata
asilimia 80 ya mtaji uliotumika kwa mwaka uliotumika
mtaji huo na baada ya hapo itakata asilimia 50 kwa
mwaka isipokuwa tu kwamba Serikali ya Tanzania
itatakiwa kufanya marekebisho ya sheria ili kuyafanya
makato haya yakubalike chini ya sheria za Tanzania.
Kifungu hiki cha Mkataba kina maana kwamba endapo
Serikali haitafanya marekebisho ya Sheria husika, basi
Pangea Minerals itaendelea kukata asilimia mia moja ya
mtaji uliotumika kwa mwaka wa kwanza!
(viii) Kwamba mnunuzi wa madini yoyote yaliyochimbwa
katika eneo la Mkataba hatalazimika kuzuia kiasi
chochote kutoka katika bei ya mauzo.
Itakumbukwa kwamba wakati akijibu hoja ya Mheshimiwa
Zitto Kabwe juu ya kuundwa Kamati Teule ya Bunge
kuchunguza tuhuma zake dhidi ya kusainiwa kwa Mkataba
wa Buzwagi, Waziri Karamagi aliliambia Bunge la
Jamhuri ya Muungano juu ya faida zifuatazo
zinazotarajiwa kutokana na kusainiwa kwa Mkataba wa
Buzwagi:
(a) Malipo ya mrahaba na kodi nyingine za kiasi cha
Dola za Marekani milioni 198.9;
(b) Makato ya kodi ya mishahara ya wafanyakazi (pay as
you earn) ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 50.3;
(c) Ujenzi wa laini na matumizi ya umeme ya Mgodi na
maeneo yanayouzunguka ya Dola za Marekani milioni 30;
(d) Manunuzi ya huduma mbali mbali wakati wa kujenga
miundo mbinu, mitambo na wakati wa uzalishaji ya kiasi
cha Dola za Marekani milioni 568.4;
(e) Jumla ya mapato yote yatakayoingia kwenye uchumi
wa taifa katika kipindi cha uhai wa mgodi ni takriban
Dola za Marekani milioni 818.3;
(f) Ajira 630 kwa Watanzania; kuongezeka kwa pato la
taifa la fedha za kigeni; miundo mbinu ya kiuchumi na
kijamii, n.k.
Hata hivyo, vifungu vilivyotajwa hapo juu vinaonyesha
kwamba nje ya malipo ya mrahaba na kodi ya zuio, sana
sana Serikali ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na
Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, itakuwa inalipwa
jumla ya Dola za Marekani 583,980 kwa mwaka. Na kwa
kuzingatia taarifa ya Waziri Karamagi kwamba Mgodi wa
Buzwagi unatazamiwa kuwa na 'uhai' wa miaka kumi,
Serikali italipwa Dola za Marekani 5,839,800 nje ya
mrahaba na kodi ya zuio kutokana na utajiri wa madini
yote yaliyoko eneo la Buzwagi. Ukweli ni kwamba kiasi
hicho kinaweza kupungua zaidi kwa kuangalia maelezo ya
aya za ii(c), iv na v(a), (b) na (c) katika Waraka
huu. Kuhusiana na madai ya Waziri Karamagi juu ya
malipo ya mrahaba na kodi nyinginezo ya Dola za
Marekani milioni 198.9, taarifa aliyoitoa Naibu wake
William Ngeleja inaonyesha kwamba katika kipindi cha
miaka kumi iliyopita, Serikali ya Tanzania imepokea
Dola za Marekani milioni 78 tu kama mrahaba na kodi
nyingine kutoka kwa migodi yote 6 ya dhahabu ambayo
inafanya kazi hadi sasa. Kwa kiwango hicho, Buzwagi
ambao Waziri Karamagi mwenyewe aliuita kama 'Marginal
Mine', yaani 'Mgodi Mdogo' ni wazi kwamba matarajio ya
Serikali kuhusu manufaa ya Mgodi wa Buzwagi hayana
msingi wowote katika hali halisi.
III. UHAMISHAJI WA RASILMALI YA TAIFA
Mkataba wa Buzwagi pia utakuwa na madhara makubwa kwa
uchumi wa taifa kwa sababu utapelekea kuhamishwa kwa
rasilmali ya taifa letu kwenda nje ya nchi (capital
flight). Kwa muda wote wa uhai wa Mkataba, Pangea
Minerals ". ina haki na itaendelea kuwa na haki ya":
(a) Kubakisha nje ya nchi fedha za mauzo ya madini
yanayomilikiwa na Kampuni na, ilimradi tu inatimiza
wajibu wake wa kufanya malipo ndani ya Tanzania,
Kampuni itakuwa na haki ya kuhamisha na/au kupeleka
fedha hizo za mauzo ya madini popote inapotaka na kwa
namna yoyote inayotaka;
(b) Kuingia katika makubaliano ya mikopo nje ya
Tanzania inayohusu shughuli za uchimbaji na kubakisha
nje ya nchi fedha zinazotokana na malipo ya mikopo
hiyo;
(c) Kufungua na kuendesha akaunti za fedha za Tanzania
au za kigeni endapo akaunti hizo zinatumika kwa ajili
ya fedha zinazotokana na/au zinazohusu shughuli za
uchimbaji madini;
(d) Kufungua na kuendesha akaunti za fedha za kigeni
nje ya Tanzania zinazoweza kuingiziwa fedha bila
kizuizi chochote na kuhamisha fedha hizo kwa uhuru na
bila kizuizi na bila masharti ya kuzibadilisha fedha
hizo kwa fedha za Tanzania na/au kurudisha Tanzania
sehemu yoyote ya fedha hizo ilimradi tu Kampuni
inaweza kutoa taarifa kwa Benki Kuu ya Tanzania juu
matumizi ya akaunti hizo kuhusiana na shughuli za
uchimbaji madini kama itakavyotakiwa na Benki Kuu;
(e) Kusafirisha na kuuza kwa wanunuzi wa nje madini
yoyote na mazao yanayohusiana nayo yatakayochimbwa
na/au kupatikana katika eneo la Mkataba.
Masharti yaliyotajwa katika (a), (b) na (d) yanahitaji
vibali vya Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo, kifungu
cha 5.2 cha Mkataba kinailazimu Serikali ya Tanzania
kumfanya Gavana wa Benki Kuu kuiandikia Kampuni barua
itakayotoa vibali vyote vinavyotakiwa chini ya Mkataba
huu ndani ya siku thelathini (30) kutoka tarehe ya
kusainiwa kwa Mkataba. Na endapo vibali hivyo
havitatolewa kitendo hicho "hakitaathiri au kuzuia
Kampuni kutumia haki zake au kufaidika na manufaa
yaliyoko kwenye Mkataba huu"! Vile vile Serikali na
Waziri Karamagi wanatakiwa kuchukua hatua zote
kuruhusu kitendo au kitu chochote cha kuhakikisha
kwamba Kampuni inakuwa na haki na manufaa yaliyotolewa
na Mkataba huu. Aidha taarifa zozote zinazotakiwa
kuchapishwa ili kuhalalisha haki na manufaa ya Kampuni
chini ya Mkataba huu zitachapishwa lakini
kutochapishwa kwa taarifa hizo ". hakutaizuia Kampuni
kufaidika na manufaa yoyote yanayotarajiwa chini ya
Mkataba huu." Kwa masharti yaliyotajwa katika sehemu
hii, ni vigumu kuelewa na/au kukubali kauli ya Waziri
Karamagi Bungeni kwamba Mgodi wa Buzwagi utaingiza
mapato ya takriban Dola za Marekani milioni 818.3
kwenye uchumi wa taifa katika kipindi cha uhai wa
mgodi huo!
IV. MANUNUZI YA BIDHAA NA HUDUMA
Katika hotuba yake Bungeni Waziri Karamagi alidai
kwamba moja ya faida zitakazopatikana kwa kusainiwa
Mkataba wa Buzwagi ni "kununua huduma mbali mbali za
wakati wa kujenga miundombinu mingine kwenda mgodini,
ujenzi wa mitambo na wakati wa uzalishaji ambao
unatarajiwa kugharimu takriban USD 568.4 milioni."
Ushahidi wa Mkataba wenyewe unapingana na hoja ya
Waziri Karamagi. Kwanza, kifungu cha 7 kinasema
yafuatayo: "Kampuni itatoa upendeleo wa kununua bidhaa
na huduma zilizoko Tanzania ilimradi bidhaa na huduma
hizo zina ubora wa kimataifa, zinapatikana kwa wakati
na idadi inayotakiwa na zinauzwa kwa bei ya ushindani
zinapofikishwa Tanzania." Vile vile Kampuni kwa
kushauriana na Waziri itaweka utaratibu wa zabuni
utakaowawezesha wakandarasi kushindania zabuni hizo
kwa kuangalia mazingira ya Tanzania. Hakuna chochote
katika kifungu hiki cha Mkataba kinachoelezea kiasi
cha fedha kitakachotumika katika kununua bidhaa na
huduma ndani ya nchi na kama bidhaa au huduma zenyewe
zitazalishwa Tanzania au zimenunuliwa nje kwa matumizi
ya ndani.
Pili, kifungu cha 8 cha Mkataba pia kinaitaka Kampuni
na makandarasi wake kutumia bidhaa, vifaa na ugavi
vilivyozalishwa ndani ya nchi kadri inavyowezekana
wakati wa ujenzi na uendeshaji wa Mgodi na miundombinu
yake. "Hata hivyo", kifungu hiki kinatahadharisha,
"Kampuni na makandarasi wake watakuwa na haki ya
kuagiza, bila kizuizi, vitu vyote vinavyohitajika kwa
usanifu, ujenzi, kuweka mitambo na uendeshaji wa
Mradi, ikiwa ni pamoja na mafuta, spea na sehemu za
spea . ilimradi tu ushuru wowote unaohusu uingizaji
mafuta, ikiwa ni pamoja na mchango wa ushuru wa
barabara hautazidi Dola za Marekani 200,000." Aidha,
"ushuru wowote wa forodha utakaotozwa kwa bidhaa na/au
vifaa vilivyoagizwa nje utakufuatana na matakwa ya
Sheria ya Ushuru wa Forodha Na. 12 ya mwaka 1976 kama
ilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho ya Sheria za
Fedha Na. 27 ya mwaka 1997." Kama tulivyoonyesha,
Sheria Na. 27 ilifuta masharti mbali mbali ya ulipaji
wa ushuru wa forodha kwa ajili ya bidhaa na/au vifaa
vinavyotumika au kuhusika na uchimbaji madini. Kifungu
hiki pia kinapingana na hoja ya Waziri Karamagi juu ya
manufaa yatakayotokana na manunuzi ya bidhaa na/au
huduma.
V. 'UTAKATIFU' WA MKATABA
Mkataba wa Buzwagi unaitaka Serikali kuhakikisha
kwamba vifungu vya sheria vinavyohusu manufaa, haki na
wajibu wa Kampuni na/au wanahisa wake hazibadilishwi
wakati wowote wa uhai wa Mkataba:
(a) Muda wa Leseni Maalumu ya Uchimbaji au matumizi ya
ardhi ya eneo la Mkataba ikiwa ni pamoja na matumizi
ya ardhi yoyote iliyoko nje ya eneo la Mkataba kwa
miundombinu, utunzaji au usafirishaji wa bidhaa zake;
(b) Kuingiza Tanzania wafanyakazi wa nje, mashine,
mitambo, magari ya usafirishaji na vifaa vingine
muhimu kwa ajili ya ujenzi wa Mgodi na uendeshaji wa
shughuli za uchimbaji madini;
(c) Misamaha ya kodi, ushuru, ada na michango ya aina
yoyote;
(d) Ulinzi wa kuhamisha mtaji, faida na gawio na
ulinzi dhidi ya utaifishaji ;
(e) Upangaji wa bei au mauzo ya dhahabu;
(f) Kubakisha na kuhamisha nje ya nchi fedha za
kigeni;
(g) Wajibu wa kulipa mrahaba, kodi ya mapato na namna
ya kuzihesabu kodi hizo;
(h) Jambo lolote ambalo ni la msingi kwa hali ya
kiuchumi ya Kampuni.
Mkataba unatamka kwamba vifungu hivyo vya Mkataba ni
vya 'msingi' na 'vitakatifu' na kwamba endapo
vitabadilishwa na ". kuiweka Kampuni katika hali mbaya
ya kiuchumi kuliko ilivyokuwa wakati wa kusaini
Mkataba, basi Serikali kwa mashauriano na Kampuni
itachukua hatua za lazima kuhakikisha kwamba haki au
maslahi ya Kampuni hayaporomoshwi au kupunguzwa
kimsingi"!
VI. UTATUZI WA MIGOGORO
Kufuatiwa hoja ya Mheshimiwa Zitto Kabwe juu ya
kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mazingira
ya kusainiwa kwa Mkataba wa Buzwagi, kumejitokeza
mjadala mkali juu ya utashi wa kimaadili na/au madhara
ya kisheria ya Mkataba huu kusainiwa London nchini
Uingereza. Tumezungumzia kwa kirefu viwango vya
maadili na/au utashi unaotakiwa kwa viongozi wa umma
chini ya Sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma na
hatuna haja ya kurudia mjadala huo. Mjadala unaohusu
madhara ya kisheria ni wa muhimu vile vile. Mahali
unaposainiwa mkataba (locus contractus) ni muhimu sana
kisheria kwa sababu endapo mkataba wenyewe uko kimya
juu ya utaratibu wa kutatua migogoro inayoweza
kutokana na utekelezaji wa mkataba wake basi sheria za
mahali uliposainiwa ndio zinazotumika.
Mkataba wa Buzwagi umefafanua juu ya utaratibu wa
kutatua migogoro inayoweza kutokea kutokana na
utekelezaji wa Mkataba huu. Kama alivyosema Waziri
Karamagi Bungeni, Mkataba wa Buzwagi unataja kuwa
sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo
itaongoza mkataba huo." Kauli hii ya Waziri Karamagi
ni sehemu tu ya ukweli wa jambo hili kwani kuna ukweli
mwingine ambao Waziri Karamagi hakuutaja. Kwanza,
Mkataba huu utatawaliwa na sheria za Tanzania "na
taratibu za sheria za kimataifa zinazohusika." Jambo
hili limetiliwa nguvu zaidi na kifungu cha 13 cha
Mkataba kinachoamrisha kwamba mgogoro wowote
"utatatuliwa kwa upatanishi kufuatana na Kanuni za
Upatanishi za Tume ya Umoja wa Mataifa ya Sheria za
Kimataifa za Biashara (UNCITRAL)."
Pili, mahakama za Tanzania hazina mamlaka ya
kusikiliza na/au kutatua migogoro chini ya Mkataba huu
kwani jukumu hilo imepewa "Mahakama ya Upatanishi wa
Kimaifa ya London kufuatana na Kanuni za Upatanishi za
UNCITRAL zitakazokuwa zinatumika wakati wa kusaini
Mkataba huu." Chini ya utaratibu wa Mkataba huu, kila
upande unapaswa kuteua mpatanishi mmoja na wapatanishi
hao wawili watachagua mpatanishi wa tatu ambaye ndiye
atakuwa Mwenyekiti wa Mahakama ya Upatanishi. Aidha,
kesi ya upatanishi huo itafanyika London na lugha
itakayotumika ni Kiingereza. Vile vile hukumu yoyote
itakayotolewa na Mahakama ya Upatanishi itazifunga
pande zote na Serikali inafuta haki zake za kudai
ulinzi dhidi ya mashtaka kwa nchi huru (sovereign
immunity) na inafuta madai yoyote ya ulinzi huo kuhusu
mashauri ya kukaza hukumu hiyo . na ulinzi kuhusu
ukazaji wa hukumu dhidi ya mali yoyote ya Serikali
inayotumika kwa ajili ya shughuli za biashara."
Tatu, ni muhimu kuelewa kwamba ingawa Mkataba wa
Buzwagi unasema kwamba utaongozwa na sheria za
Tanzania, sheria zenyewe hazilindi uhuru wa taifa letu
na mamlaka ya kikatiba ya taasisi zetu za kutatua
migogoro. Kwa mfano, Sheria ya Madini Na. 5 ya mwaka
1998 - ambayo ndiyo sheria itakayoongoza Mkataba huu -
inatamka kwamba migogoro yoyote kati ya mmiliki wa
Leseni Maalumu ya Uchimbaji na serikali utatatuliwa
kwa kufuata kanuni au taratibu za Kituo cha Kimataifa
cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID). Kituo
hiki ni moja ya taasisi za Benki ya Dunia na kina
makao yake makuu New York, Marekani.