Ziara ya Dk. Slaa Marekani yaendelea kwa mafanikio
I. Mafanikio ya ziara kwa miradi ya Maendeleo katika halmashauri ya Karatu
Kama sehemu ya ziara yake nchini Marekani jana jioni Mbunge wa Karatu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA - Dr Willbroad Slaa amefika Norfolk kufanya mikutano kuhusu mipango ya miradi ya maendeleo ya wilaya ya Karatu.
Mpaka sasa amekwisha kufanya mikutano na viongozi au/na taasisi zifuatazo:
- St. Joseph's Medical Center, Baltimore, kuhusu Mradi wa Kuboresha Maisha Vijijini (Village wellness Program) ambayo inahusu miradi ya Afya, Elimu, Maji, na mikopo midogo midogo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, KKKT Dayosisi ya Kaskazini na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu. Wilaya ya Karatu imekwisha kupokea hadi sasa zaidi ya dola milioni 1.2 kutoka St. Joseph's Medical Center na Marafiki zake kwa miradi iliyotajwa hapo juu. Amekutana pia na marafiki na vikundi vyote vinavyotoa misaada wilaya ya Karatu kupitia St. Josph's Medical Center kupitia viongozi wake Mr.John Tolmie, Rais na Mtendaji Mkuu (CEO), na Mr.Don and Joan Tolmie, waanzilishi wa Mpango huo wa ushirikiano na Tanzania.
- Amefanya mkutano wa Mafanikio makubwa pia Notre Dame University, ambapo aliwahutubia wahadhiri na wanafunzi na kuanzisha uhusiano na Kata ya Bassotu. Misaada hiyo itaratibiwa na St. Joseph's Medical Center, ambao ni mratibu mkuu wa misaada inayokwenda Kata ya Bassotu. Uongozi wa St. Joseph's Medical Center, utafika Kata ya Bassotu mwanzoni mwa Mwezi Februari 2008 kuanzisha rasmi uhusiano huo. Uhusiano huu unahusu maeneo ya Elimu ya Shule za Sekondari, Afya na Maji.
- Amekutana pia na World Lutheran Relief na Catholic Relief Services (CRS) ambao wanaendesha kwa miaka minne sasa miradi kadhaa katika wilaya ya Karatu hasa katika Kata ya Endabash na Endamarariek na wanajishughulisha na mikopo midogo midogo kwa vikundi mbalimbali vya Wanawake na vijana. Wanaendesha mradi mkubwa wa ukuzaji wa zao la Mbaazi na wanashughulika na miradi ya Afya ikiwemo VVU/UKIMWI kwa kushirikiana na Dayosisi ya Mbulu na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu. World Lutheran Relief na CRS Makao yao Makuu ni Baltimore, Jimbo la Maryland.
- Amefanya pia Mkutano na Mheshimiwa Brian R. Moe, Naibu Mkuu wa Jimbo (Deputy Secretary of State) Jimbo la Maryland (State of Maryland) na Mary Nitsch, Mkurugenzi wa Masuala ya Kimataifa (Director of International Affairs), Jimbo la Maryland. Jimbo la Maryland linashirikiana na Wilaya ya Karatu kupitia St. Joseph's Medical Center. Mpango wa Ushirikiano kati ya St. Joseph's Medical Center na Wilaya ya Karatu kwa sasa uko katika Kata 5 za wilaya ya Karatu ambazo kwa ujumla zina vijiji 20 kati ya vijiji 45 za Wilaya ya Karatu. Mazungumzo nao yamelenga kupeleka mradi huu katika vijiji vyote. Mradi pia unaanza mpango mpya wa kufuta Malaria katika Wilaya ya Karatu na mpango huu uko kwenye hatua ya maandalizi. Ukifanikiwa mpango huu utakuwa mkombozi kwa wananchi wa Karatu kwani kwa Takwimu za Idara ya Afya Wilaya ya Karatu kwa sasa imeathirika kwa Malaria kwa kiwango cha asilimia 16, mara 4 zaidi ya VVU/UKIMWI wakati ambapo malaria inaweza kuzuilika na kutibika. Kwa mujibu wa Dr Slaa “hakuna sababu ya Wananchi kuendelea kuteseka wakati Malaria inaweza kuzuilika na kutibika.”
II. Mazungumzo na Wizara ya Mambo ya Nje masuala mbalimbali ikiwemo hali ya rushwa Tanzania
Katika ziara hiyo Dr Slaa amefanya pia Mkutano naizara ya Mambo ya Nchi za Nje (State Department) ya Marekani ambapo amekutana na Bwana Jeffrey R. Krilla, Naibu Katibu Msaidizi wa Idara ya Demokrasia, Haki za Binadamu na Kazi(Deputy Assistant Secretary, Department of Democracy, Human Rights and Labor) na Karen Gilbride - Mkuu wa Kitengo cha Afrika(Head Africa Section)
Mazungumzo na viongozi hao waandamizi yamehusu hasa maeneo yafuatayo:
- Miradi ya Wilaya ya Karatu kwa ujumla ambapo St. Joseph's Medical Center pia inategemea kupata msaada mkubwa kutoka Shirika la Misaada la Marekani(USAID) hivi karibuni kwa ajili ya Miradi iliyoko wilaya ya Karatu. USAID tayari ina mradi mwingine mkubwa wa Miaka 5 Wilayani Karatu kupitia Shirika la Minnessota International Health Volunteers (MIHV) uliozinduliwa rasmi mwezi July, 2007 kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
- Ajenda zingine zilihusu masuala ya Haki za Binadamu nchini Tanzania, Rushwa hususani hali ya rushwa ilivyo hivi sasa na Sheria mpya ya TAKUKURU ya mwaka 2007 na mapungufu yake, Hali ya Zanzibar na mazungumzo ya Mwafaka yanayoendelea hivi sasa.
III. Ziara inaendelea mpaka Oktoba 18 ikilenga kutafuta misaada kwa walemavu na udhamini wa wanafunzi.
- Kesho anaondoka Norfolk kuelekea Chicago ambako atakuwa na mikutano kadhaa na hapa mikutano itahusu miradi mbalimbali ya misaada kwa shule za Walemavu na hasa Shule ya Faraja iliyoko Sanya Juu, Moshi, na pia mikutano na vikundi mbalimbali vinavyosaidia Miradi mbalimbali ya Wilaya ya Karatu kupitia St. Joseph's Medical Center.
- Jumamosi, atarejea Norfolk ambako Jumapili atafanya mikutano zaidi na makundi mbalimbali yanayotoa misaada kwa Wilaya ya Karatu kama vile First Lutheran Church.
- Jumatano, 17 Oktoba atakuwa na Mkutano na Grace Lutheran Church ambao wanatoa misaada Wilaya ya Karatu, mkutano na Wafadhili wa The American God Parent Scholarship Foundation ambao wanafadhili zaidi ya wanafunzi 1000 katika shule za Sekondari Tanzania hivi sasa; mazungumzo haya yanalenga kupanua mpango huu wa udhamini (Scholarship). Mpango wa udhamini unaotoa msaada wa Karo, mavazi, nauli, na matumizi ya kawaida kwa wanafunzi wanaotoka kwenye familia maskini kabisa. Kwa sasa mpango huu uko Wilaya ya Karatu na Moshi, na unalenga kupanuka katika Kata ya Bassotu kuanzia mwaka 2008.
- Tarehe 18 Oktoba, Siku ya Alhamisi, atafanya mkutano mwingine Mkubwa Chuo Kikuu cha Regent, Regents University, Wenchester, ambako Mazungumzo haya yatahusu hasa namna ya kuanzisha uhusiano kati ya Chuo Kikuu cha Wenchester na Shule za Sekondari na vyuo katika Wilaya ya Karatu na Kata ya Bassotu, Wilayani Hanang. Jioni yake Msafara wake ambao unajumuisha pia Mkewe unarejea Dar-Es-Salaam kupitia Amsterdam ambako utafika Dar es salaam tarehe 19 Oktoba, 2007. Tarehe 20 Oktoba, Dr. Slaa, anaondoka kuelekea Lilongwe kwa Bunge la Jumuia ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo yeye ni mmoja wa wabunge.
Toka mwaka 2000 Halmashauri ya Karatu iko chini ya CHADEMA kama chama tawala/kiongozi kutokana na kuwa na madiwani wengi zaidi ya CCM. Chini ya uongozi wa CHADEMA halmashauri hii imekuwa mfano wa kuigwa katika kuleta maendeleo hususani katika sekta za maji, elimu, afya na utawala bora.
Imetolewa na 11/10/2007:
John Mnyika
Kaimu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje
Na Mkurugenzi wa Vijana Taifa