lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

Mkutano wa viongozi wa Vijana Afrika kufanyika Tanzania

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

  1. CHADEMA kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Vijana Afrika
  2. Vijana wa Vyama vya Afrika kukutana kujadili maendeleo ya kiitikadi


Mkutano wa Viongozi wa Vijana wa Vyama Vya Kidemokrasia Afrika (DUA Youth Conference) unatarajiwa kufanyika Tanzania kuanzia tarehe 18 mpaka 20 Agosti 2007 katika Hoteli ya Kunduchi, Dar es Salaam chini ya CHADEMA kama mwenyeji.

Mkutano huo wa siku tatu utajadili masuala ya maendeleo ya kiitikadi ya vyama vya kidemokrasia Afrika hususani katika kujenga mabaraza/jumuia za vijana za vyama hivyo. Katika Mkutano huo vijana watapata pia fursa ya kujadili hali ya kisiasa pamoja na michakato ya kiuchaguzi Afrika ikiwemo kuhusu mustakabali wa kisiasa wa nchi za Zimbabwe, Sudan (Darfur) na Tanzania (Zanzibar) na kutoa maazimio mbalimbali kuhusu maendeleo ya kiitikadi na demokrasia katika nchi zao. Kadhalika katika mkutano huo mtandao wa viongozi vijana wa vyama vya kidemokrasia Afrika utaendelezwa.

Zaidi ya viongozi vijana 30 wameshathibitisha kushiriki mkutano huo mpaka sasa kutoka nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Angola, Botswana, Ghana, Ivory Coast, Lesotho, Liberia, Msumbiji, Namibia, Uganda, Seychelles na wenyeji Tanzania. Nchi nyingine zaidi zinatarajiwa kuhudhuria katika mkutano huu. Pia watakuwepo wageni kutoka Sweden na Uingereza kutoa uzoefu wao kuhusu maendeleo ya kiitikadi hususani kwa taasisi za vijana za vyama vya siasa duniani.

Itakumbukwa kwamba tangu mwishoni mwa mwaka jana, makao makuu ya Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (Democratic Union of Africa - DUA) yalihamia Tanzania chini ya CHADEMA kama mwenyeji. Kwa muktadha huo, sekretariati ya DUA inaratibiwa na ofisi ya katibu mkuu CHADEMA kupitia kurugenzi ya mambo ya nchi za nje ya CHADEMA. Kabla ya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji Mikutano ya Vijana wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika ilikuwa ikifanyika kila mwaka nchini Afrika Kusini.

CHADEMA ni mwanachama wa umoja huu ambao wanachama wake ni vyama vya kidemokrasia Afrika ambavyo vingine ni vyama tawala na vingine ni vyama mbadala ama kama wengi walivyozoea kuviita vyama vya upinzani. Baadhi ya vyama vilivyoko katika umoja huu ambavyo ni vyama tawala ni pamoja na NPP cha Ghana, DP cha Kenya na Unity Party cha Liberia. Baadhi ya vyama mbadala vilivyomo katika umoja huu ni pamoja na DTA ya Namibia na FDC cha Uganda ya Uganda inayoongozwa na Dk. Besigye. Wanachama wa umoja huu ni vyama vyenye itikadi ya mrengo wa kati na vile vya mrengo wa kati kulia; CHADEMA ni chama chenye itikadi ya mrengo wa kati chini ya falsafa ya ‘nguvu ya umma’.

“Hii ni heshima nyingine ambayo chama chetu kimepewa. Ni ishara ya kuendelea kutambuliwa katika kada za kimataifa. Historia ya nchi yetu katika siasa za Afrika inaendelea kujiandika vizuri zaidi kupitia CHADEMA. Wakati wa kudai uhuru Tanzania ilikuwa ni kitovu cha mapambano ya ukombozi, na kwa kiasi kikubwa yakiongozwa na vijana wa wakati huo. Sasa ni wakati wa vijana kuongoza harakati za kudai uhuru wa kweli hivyo huu ni wakati wa kudai mabadiliko kwa njia ya demokrasia. Vijana wa CHADEMA tumedhamiria kuwa kitovu cha mabadiliko katika Afrika kupitia mfumo wa vyama vingi. Tunahitaji vijana wenzetu na wadau wengine mtuunge mkono kufanikisha azma hii.”

Mpaka sasa Tanzania imepata fursa mbalimbali kutokana na makao makuu ya Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA) kuhamia nchini. Baadhi ya fursa hizo ni pamoja na mikutano na matukio ya DUA kufanyikia Tanzania na hivyo kuvuta raslimali ambapo mapema mwaka huu Mkutano wa Viongozi wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika ulifanyika hapa nchini uliojadili ‘demokrasia Afrika’.

Imetolewa tarehe 12 Agosti 2007 na:

John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa wa CHADEMA na
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IYDU)




 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl