UKIUKWAJI wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge sheria namba 3 ya 1988 na Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2004.
Mheshimiwa Spika,
Februari 8 mwaka huu ulitoa uamuzi kuhusu suala la Mheshimiwa Adam Malima (Mb) na Bwana Reginald Mengi. Katika uamuzi wako uliamua kuwakutanisha Mheshimiwa Malima na Bwana Mengi ili kutafuta suluhu kwa manufaa ya jamii ya Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa barua kutoka kwa Mheshimiwa Malima kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Yusuf Makamba (Mb) isiyo na kumbukumbu ya tarehe 3 Machi 2007, mheshimiwa Malima sio tu amekataa uamuzi wako bali amekushitaki wewe Mheshimiwa Spika kwa Katibu Mkuu wa CCM, chama unachotoka, ulichotumikia na unachoendelea kukitumikia kwa uadilifu mkubwa.
Katika gazeti la Mzalendo (gazeti la chama cha Mapinduzi) la Aprili 8, 2007 toleo namba 1871, Katibu Mkuu wa CCM amenukuliwa kama ifuatavyo “Malima na Sitta wote ni wabunge wa CCM na masuala yao yanaweza kujadiliwa kwa dhati ndani ya vikao ya CCM.”
Gazeti hilo linaendelea kumkunuu Mheshimiwa Makamba kuwa “Malima ndie aliyeandika barua kwake (Makamba) akilalamika kutotendewa haki na Spika Sitta alipokuwa akitoa uamuzi wa sakata kati ya yeye (Malima) na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Reginald Mengi kwenye kikao cha Bunge kilichopita.
Gazeti la Mzalendo linaendelea kumnukuu Mheshimiwa Makamba akisema, “Sitta na yeye mwenyewe (Makamba) ni wajumbe wa kamati ya wabunge wa CCM. Hata hivyo, alisema suala hilo wameamua kulifikisha kwenye secretariat ya NEC na litapata ufumbuzi.
Hii inadhihirisha kuwa Katibu Mkuu wa CCM amepata barua ya Malima, ameipokea na kuanza kuifanyia kazi. Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu wa CCM, na hajayakanusha, Mheshimiwa Kighoma Ali Malima, Mbunge wa Mkuranga mkoa wa Pwani, amelalamika kwa katibu mkuu wa chama chake kutotendewa haki na Spika wa Bunge.
Vile vile, inaonekana kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Makamba katika gazeti la Mzalendo, kuwa Sekretariat ya NEC ya CCM ina mamlaka ya kuhoji maamuzi ya Bunge kana kwamba nchi hii bado ipo katika mfumo wa chama kimoja. Huku ni kuingilia uhuru wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, sina tatizo hata kidogo na haki ya Mheshimiwa Malima kukaidi uamuzi wako halali, bali kwa maoni yangu na kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni zetu Mheshimiwa Malima ameingilia uhuru wa Bunge (Contempt of Parliament) na anahatarisha uhuru wa muhimili mmoja mkuu wa Dola, Bunge.
Kwa maoni yangu, kitendo cha mheshismiwa Malima kulalamika kwa Katibu Mkuu wa CCM kwamba hakutendewa haki na Spika ni kinyume na Kanuni za Bunge, kanuni ya 4 (3).
Pia Mbunge kutoa nje suala linalohusu Bunge ni kitendo cha kuvunja Katiba na kulivunjia heshima Bunge.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha mbunge kupeleka suala la Bunge katika chama cha siasa anachotoka ni hatari sana , na kinahatarisha uhai wa demokrasia ya vyama vingi.
Tukiliacha bila kulidhibiti, kesho na keshokutwa mbunge wa Chadema atakerwa na Spika na kuamua kumshtaki kwa katibu mkuu wa CHADEMA. Nchi haiwezi kuongozwa namna hii maana itakuwa ni vurugu.
Mheshimiwa Spika, msingi wa maelezo yangu haya ni Katiba ya Jamhuri ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, namba 3 ya mwaka 1988 na Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2004.
Mheshimiwa Spika, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara imeonesha wazi wazi mamlaka ya Bunge katika dola ya Tanzania , na kwamba uhuru na utaratibu wa Bunge hauwezi kuhojiwa na chombo chochote nje ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 100(1) ya Katiba inasema, “Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano au katika mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.
Mahala penginepo nje ya Bunge ni pamoja na katika vyama vya siasa tunavyotoka sisi waheshimiwa wabunge.
Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao Katiba yetu imeutaja kuwa hautavunjwa wala kuhojiwa mahala popote umewekwa na kanuni za Bunge ambazo nazo zimetajwa na Katiba yetu ambayo sote tuliapa kuilinda, kuitetea na kuihifadhi.
Mheshimiwa Spika, katika barua ya Mheshimiwa Malima kwenda kwa katibu mkuu wa CCM ameonyesha dharau kwa Spika wa Bunge kinyume na kifungu cha 24 cha sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge.
Ninanukuu sehemu ya barua ya Mheshimiwa Malima kwa Katibu Mkuu wa CCM. Anasema “……….kulikuwa hakuna haja ya Spika kupuuzia ushauri aliopewa na wengi na kuchukua maamuzi ya wachache ambayo yanaonekana yametawaliwa na misingi ya ubinafsi, kinyume na maadili, heshima na nidhamu ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi”
Mheshimiwa Spika, matamshi haya katika barua yanamshutumu Spika wa Bunge hili kuwa ni mtu mpuuzi, ni mbinafsi na haheshimu nidhamu ya chama chake.
Hii ni dharau kubwa kwa Spika wa Bunge. Hii ni kejeli kubwa sio tu kwa Spika bali pia kwa Bunge kama asasi muhimu wa demokrasia nchini.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha mbunge kutoa nje suala la Bunge na kulipeleka katika chama cha siasa ni kitendo cha kuvunja katiba pia.
Kwa kuwa kitendo hiki kimefanywa na mbunge anayetoka CCM na katibu mkuu aliyepelekewa barua naye pia anatoka CCM na wewe mheshimiwa spika ni mbunge kutoka CCM, basi ni rahisi mno kuacha suala kupita hivi hivi tu.
Mheshimiwa Spika, kuthibitisha maelezo yangu hapo juu ninapenda nilifahamishe Bunge kuwa mheshimiwa Malima, licha ya kuvunja Katiba, Sheria na Kanuni wazi wazi na kwa kujua ameendelea kuongea suala hili katika vyombo vya habari.
Katika gazeti la HabariLeo (gazeti linalomilikiwa na serikali la Aprili 9, mwaka 2007 mheshimiwa Malima amenukuliwa akisema maneno yafuatayo.
“Mimi sitarajii kama spika atakuwa amechukia na hatua yangu ya kuomba chama kitumie busara zake kwenye suala hili. Mimi na spika sote tumenufaika huko nyuma na busara za CCM kututeua kugombea ubunge kwa niaba ya chama, hivyo sitarajii kama leo Spika atakuwa na hofu na vikao vya chama wakati ndicho kilichompendekeza kugombea Ubunge.
Mheshimiwa Spika, maneno haya ni kejeli kubwa kwa Taasisi ya Uspika. Kwa maneno haya ambayo yamesomwa na umma wa Watanzania wote, mheshimiwa Malima anataka kuonesha kuwa Spika wa Bunge la Tanzania ambaye alichaguliwa bila kupingwa na wabunge wote ni mwoga na ana hofu na vikao vya chama chake.
Vile vile anataka kuonesha kuwa Spika wa Bunge ni mtu wa kawaida tu kama yeye kwani wote wamepitishwa na vikao vile vile, hivyo hababaishwi.
Mheshimiwa Spika, uspika sio sawa na Usitta au Umsekwa au Ukificho au Ukinana au Umongela. Uspika ni Taasisi ya Uspika. Spika ni kiongozi wa vyama vyote ndani ya Bunge.
Kama ilivyo kwa Mheshimiwa Malima, Spika pia ni wa Mheshimiwa Chacha Wangwe. Spika pia ni wa Mheshimiwa Khalifa Khalifa. Spika pia ni wa Mheshimiwa John Cheyo.
Maneno ya Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ni kejeli kwa Uspika. Ni dharau kwa Spika. Ni matusi kwa Mheshimiwa John Sitta (Mb).
Kejeli na dharau hii haipaswi kuvumiliwa na Mbunge yeyote naayeheshimu Uspika!
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa kwamba Spika kama binaadamu anaweza kukosea, Bunge letu lilipitisha kanuni namba 4(3) ambayo inamtaka Mbunge yeyote ambaye hakuridhika na uamuzi wa Spika wa Bunge kukata rufaa katika kamati ya kanuni za Bunge ambapo katika kikao kitakachojadili suala hilo Spika hatakuwa Mwenyekiti.
Mheshimiwa Spika, nimepitia rekodi zote za Bunge za Kamati ya Kanuni na sijakuta uthibitisho wowote kuonesha kuwa Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima (Mb) alikata rufaa huko na hakutendewa haki na hivyo kupeleka suala lake katika vikao vya chama cha CCM.
Mheshimiwa Spika, mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima (Mb) amepeleka suala la Bunge nje ya Bunge tena bila kumaliza taratibu zote za kibunge. Kwa maoni yangu hiki ni kitendo cha kuingilia uhuru wa Bunge kinyume na sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge ya mwaka 1988.
Mheshimiwa Spika, nimesoma kanuni za Bunge toleo la mwaka 2004. Sijaona sehemu yeyote ambayo katibu mkuu wa CCM au katibu mkuu wa chama kingine chochote anatajwa. Kanuni zinamtaja spika, naibu spika, waziri mkuu na kiongozi wa upinzani bungeni.
Ndani ya Bunge hili, tunao makatibu wakuu wawili wa vyama. Mheshimiwa Dk. Willibrod Slaa (Mb) mbunge wa Karatu (Chadema) na Yusuf Makamba (Mb) (kuteuliwa). Ni nini nafasi yao katika mfumo wa Bunge letu?
Mheshimiwa Spika, tunao makamu wenyeviti taifa wawili wa vyama vya siasa humu ndani ya Bunge. Mheshimiwa John Malecela mbunge wa Mtera mheshimiwa Phares Kabuye, mbunge wa Biharamulo makamu mwenyekiti wa TLP. Ni nini nafasi yao katika mfumo wa Bunge letu?
Ni wapi katika kanuni zetu pametajwa kuwa kama huridhiki na maamuzi ya Spika ukimbilie katika chama chako cha Siasa?
Maamuzi ya Spika sio masuala binafsi ambayo viongozi wa chama waweza kusuluhisha. Maamuzi ya Spika ni maamuzi ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia naomba ninukuu kifungu cha sheria namba 3 ya mwaka 1988 ambayo ndio inatekeleza takwa la kikatiba la kulinda hadhi ya Bunge.
Mheshimiwa spika, kipengele husika kina maana kuwa ni kosa kwa mbunge kuonyesha dharau kwa spika wa Bunge na vile vile ni kosa kuonyesha dalili zozote za dharau kwa spika au naibu spika au mwenyekiti wa Bunge.
Maelezo yangu hapo juu yanaonesha kinaga ubaga kuwa mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima, amevunja sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kifungu cha 24(d)(e). Kwa kutenda kosa hili anastahili kuchukuliwa hatua.
Vilevile, kwa kitendo chake cha kuandika barua kwa katibu mkuu wa CCM, Mheshimiwa Malima ametenda kosa la kudharau taratibu za Bunge zilizowekwa na kanuni ya 4(3) na mwenendo wa Bunge ambao kwayo ulifikia maamuzi yako ya tarehe 8 Februari 2007 na hivyo anastahili kuadhibiwa.
Nyongeza ya hapo Mheshimiwa Malima ametenda kosa kwa kitendo cha kupeleka suala la Bunge nje ya Bunge na hivyo kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 100(1).
Achukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa mbunge mwingine yeyote ambaye atathubutu kulivunjia heshima Bunge kama muhimili mkuu wa dola.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa, kwa mujibu wa madaraka uliyo nayo na kwa kutumia utaratibu utakaoona unafaa suala hili lishughulikiwe na kutolewa maamuzi kwa misingi ya sheria na bila ya kuathiri haki ya mtu kusikilizwa na kujitetea.
Mheshimiwa spika, naomba kuwasilisha.
Halima James Mdee (Mb)
Mbunge wa Viti Maalumu
Dodoma , 10 Aprili 2007