Tarehe 10/1/2007 Mhe. Philemon Ndesamburo (Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya CHADEMA) aliwasilisha barua kwa Spika na nakala katika ofisi yangu ya kujiuzulu kuwa mjumbe wa kamati ya haki, maadili na madaraka ya Bunge.
Katika barua yake Mhe. Ndesamburo ametaja sababu za kujiuzulu kwake ni pamoja na: Mosi, kuwepo kwa tuhuma kwamba wabunge wamepewa rushwa na kwamba kamati ilikataa kufuatilia kwanza ukweli wa tuhuma hizo kabla ya kamati kusikiliza kesi ya msingi; Pili, kuwepo kwa mazingira ya mhimili wa serikali (executive) kuingilia mhimili wa bunge (legislative) ambayo ni kinyume cha utawala wa sheria.
Kadhalika tarehe 11/1/2007 vyombo mbalimbali vya habari vilinukuu masuala kadhaa aliyoyasema Mhe. Ndesamburo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya baada ya kujiuzulu. Pamoja na mambo mengine alinukuliwa akisema kwamba Mengi amemwambia kuwa wewe (Mh Lowassa) ulimwambia kwamba afute kesi yake kwa kuwa atashindwa kwa kuwa Manji ametoa rushwa kwa wabunge. Na kwamba baada ya Mhe. Ndesamburo kuwasilisha taarifa hii kwenye kamati wewe (Mh Lowassa) ukamwambia Mengi amkane.
Pamoja na uzito wa tuhuma hizi na hasa ukizingatia uzito wa nafasi yako ya Uwaziri Mkuu mpaka sasa hujajitokeza wewe mwenyewe kukanusha au kukubali taarifa hii.
Kama kweli wewe ulifahamau kuwa kuna mtu ametoa rushwa kwa wabunge na hakuchukua hatua zinazostahili kwa vyovyote vile ni kinyume na sheria, maadili ya uongozi na dhamira ya Mheshimiwa Rais Kikwete ya kupambana na rushwa bila kumfumbia macho yeyote.
Kwa upande mwingine tuhuma kwamba mhimili wa serikali (executive) unaingilia mhimili wa bunge (legislature) zinakuelekea wewe (Waziri Mkuu) moja kwa moja kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni. Suala hili ni kinyume na utawala bora na mgawanyo wa madaraka uliomo katika sheria na katiba ya nchi ambayo umeapa kuilinda.
Kwa barua hii tunakuomba wewe (Mhe Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu) utoe tamko lako rasmi kuhusu kauli za Mh. Ndesamburo zinazokuhusu wewe na ofisi yako moja kwa moja.
Kwa vyovyote vile ukimya wako katika suala hili kadiri unavyoendelea unaweza kuwafanya wananchi kupoteza imani kuhusu msimamo wako katika vita dhidi ya rushwa na jitihada za kuleta utawala bora nchini.
Wako katika ujenzi wa Taifa,
Dr. Wilbroad Slaa (Mb)
Katibu Mkuu
Nakala kwa taarifa:
Rais - Jamhuri wa Muungano wa Tanzania
Spika - Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Vyombo vya Habari