Tumepokea barua yako ya tarehe 10/1/2007 ikitujulisha kuhusu uamuzi wako wa kujiuzulu ujumbe katika kamati ya haki, maadili na madaraka ya Bunge.
Baada ya kutafakari sababu ulizozitoa tumeamua tukupongeze kwa uamuzi wako wa kishujaa wa kusimama bila ya hofu katika misingi ya haki, uadilifu na ukweli.
Uamuzi wako ni ishara tosha kwamba wewe ni mbunge, kiongozi na mwanachama unayepeperusha vizuri bendera ya CHADEMA hususani katika kusimamia misingi yetu ya maadili, ukweli, demokrasia na maendeleo.
Tunaungana nawe kwamba uwepo wa madai kwamba wabunge wamepewa rushwa na kamati kuamua kulifumbia macho suala hili ili kubaini ukweli wa tuhuma hizi kabla ya kutoa uamuzi wa kesi ya msingi ni kinyume na misingi ya haki na utawala bora.
Tunaimani kwamba uamuzi wako utaviamsha vyombo vya dola; asasi zinazosimamia haki za binadamu na utawala bora na ofisi ya spika kufuatilia masuala uliyoyaweka bayana kwa undani na kuchukua hatua zinazostahili.
Aidha tunategemea wananchi waliokupigia kura na watanzania kwa ujumla watafuatilia kwa umakini suala hili na kukuunga mkono kama sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa na kuhamasisha uwajibikaji.
Kwa upande wetu tunaendelea kufuatilia suala hili kwa undani na tutatoa tamko la CHADEMA kwa umma wa watanzania hivi karibuni ili haki na ukweli uweze kusimamiwa kwa nguvu ya umma.
Na tunaahidi kuendelea kukupa ushirikiano wa dhati katika mchakato mzima wa suala hili.
Pamoja na salam za chama,
Mzee Victor Kimesera
Kny. Katibu Mkuu
Nakala: Vyombo vya habari