lf.bevel
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE

6 Novemba 2007

Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wamiminika CHADEMA

Dodoma

WANAFUNZI wa vyuo vikuu hapa nchini na wasomi wengine waliobobea ndio watakaoleta mabadiliko ya kisiasa na uchumi kwa kuwa jamii inawaamini kutokana na upeo wao wa kujua mambo na kuyachanganua bila kuburuzwa.

Mbunge wa jimbo la Tarime, Chacha Wangwe alisema mjini hapa wakati wa kufungua tawi la vijana la chama cha demokrasia na maendeleo, CHADEMA linaloundwa na wanafunzi wa vyuo viwili mkoani humo kutoka chuo kikuu cha Dodoma na Mtakatifu John waliojiunga na chama hicho katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa reli.

Zaidi ya wanachuo 300 kutoka vyuo hivyo viwili wamejiunga na CHADEMA kwa madai ya kuridhishwa na sera za chama hicho na kukiona kuwa ndicho chama pekee kinachoweza kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi na ndicho chama chenye mwelekeo mkubwa unaoweza kuleta upinzani wa juu dhidi ya CCM.

Wabunge watano wa CHADEMA, Lucy Owenya, Mhonga Said, Said Arfi, Grace Kiwelu na Chacha Wangwe walihudhuria kwenye hafla hiyo ya kuwapokea wanachama wapya kutoka kwenye vyuo hivyo ambao kwa pamoja wanaunda tawi la vijana la chama hicho na kuwa tawi la mfano kwenye mkoa huo ambao pia ndio makao makuu ya CCM.

Mbunge wa jimbo la Mpanda kati, Arfi alisema kuwa muda mrefu alikuwa akifikiria jinsi wasomi wa nchi hii walivyowasaliti wananchi kwa kuogopa kuwatetea na kutetea maslahi ya nchi lakini hivi sasa anaona mambo yamebadilika na wasomi wamekuwa mstari wa mbele kuhakikidha kuwa wanaleta mabadiliko ya kisiasa.

Alisema kuwa vijana wasomi, wenye nguvu n a ari ndio wanaoweza kuleta mabadiliko katika nchi hii wakichukulia mfano wa chama hicho chenye viti 11 vya ubunge ndani ya bunge la Jamhuri ya Muungano kwamba idadi kubwa ya wabunge hao ni vijana walioacha kuogopa vitisho na kuingia upinzani.

Akisisitiza kuhusu moyo na ujasiri ulioonyeshwa na wanafunzi hao wa Dodoma, Mbunge Wangwe alisema kuwa wachukulie mfano wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliyefuykuzwa bungeni kwa muda kuwa hali hiyo imeleta changamoto kubwa ya kisiasa na watu wengi wamepata fursa ya kujua mambo mengi yaliyokuwa yakifichwa na serikali.

Akiwaelezea hali ya ujasiri na kutokuoogopa kitu aliwaambia wanachuo hao kuwa katika harakati zake za kisiasa amekwisha wekwa mahabusu mara 98 na katika kipindi hicho ameweza kufunguliwa kesi 10 mahakamani na kwa vile nyingi zilikuwa zinalenga uchochezi aliweza kushinda baada ya kukosekana ushahidi.

Mbunge wa viti maalum wa chama hicho, Mhonga alisema kuwa wabunge vijana wanapaswa kufanya kazi ya kuwaelimisha wenzao wasomi na kuwatia hamasa ya kutosha ili waweze kushiriki vyema kwenye mchakato mzima wa kuunga mkono umoja wa vyama vya kidemokrasia Afrika kwa kushiriki kwenye makongamano mbali yanayowahusu vijana.

Akielezea kwa kina Mbunge,Arfi aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa tawi hilo la vijana wa vyuo hivyo,alisema kuwa hatua ya wasomi hao kuja upinzani na kufungua tawi lao ni ushindi mkubwa wa kisiasa na kuwataka wanafunzi wa vyuo vingine hapa nchini kuiga mfano huo ili waweze kutumia nafasi yao ya kuanza kujiandaa mapema kuja kuongoza hapo baadae baada ya wanasiasa wengi wakongwe kupoteza mwelekeo.

"Sisi tumekwisha zeeka wakati wetu wa kuendelea kuwa viongozi unafikia ukingoni,tupo wengi tuliochoka lakini watu bado wanang'ang'ania madalaka,jiandaeni kuongoza nchi ndio wasomi tunaowategemea, wengine watakuwa mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya hizo zote ni nafasi zenu msimuogope mtu hebu waangalieni hawa wabunge wa CHADEMA ni vijana hata nyinyi mnaweza" alisema Arfi.

Katika hafla hiyo wanachama hao wapya kutoka kwenye vyuo hivyo watapatiwa ofisi mahali watakapokuwa wakikutana na vifaa mbalimbali vitakavyowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuendesha mijadala ya wazi ili kuwahamasisha vijana wenzao kujiunga na chama hicho kwa lengo la kukiimarisha na kuwa chama chenye nguvu.


 
lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl