CHADEMA tunaamini kuwa Watanzania wengi wamepoteza imani ya kupata maendeleo kupitia serikali inayoongozwa na chama cha mapinduzi CCM, Wamekata tamaa kwasababu waliopo madarakani kwa takribani nusu karne wameshindwa kuleta mabadiliko ya kweli na mbaya zaidi wamedhamiria kubaki madarakani kwa gharama yoyote. Wamedhamiria kubaki madarakani kwa gharama ya umasikini wa watanzania.
Mwaka 1958 wakati Mwalimu Nyerere akihutubia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Mwalimu alisema , Tunadai Uhuru wetui si kwasababu tunataka kutawala, bali kwasababu mwingireza ameshindwa kuwapatia watanganyika elimu, ameshindwa kuwapatia huduma za afya ameshindwa kuondoa umasikini wa watanganyika.
Leo hii, ni takribani nusu karne, hakuna mabadiliko ya kweli yaliyopatikana katika elimu, hakuna mabadiliko ya kweli yaliyopatikana katika kumpatia mtanzania huduma za afya, hakun a hatua iliyopigwa katika kumwondoa mtanzan na umasikini, na katika baadhi ya maeneo tumerudi nyuma zaidi.
Yote haya yanahalalisha sababu za watanzania makini kuhoji uhuru walioupata, inaelekea Uhuru tulioupata ulikuwa wa wachache, ulikuwa uhuru wa vigogo wa CCM na serikali yao wakishirikiana na vibepari uchwara kwa upande mmoja, na wageni kwa upande wa pili. Mtanzania wa kawaida hana cha kujivunia kama matunda ya Uhuru alioupigania mwenyewe, hajafaidi chochote kama matunda ya uhuru uliopiganiwa na Baba na Mama zake, hajafaidi chochote kama matunda ya uhuru uliopiganiwa na Babu na Bibi zake.
Baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, watanzania wengi walianza kupata imani kuwa, vyama hivi ndio ilikuwa nguzo pekee ya wao kujikomboa dhidi ya minyororo ya umasikini waliyofungwa tangu enzi za ukoloni mpaka baada ya uhuru.
Hata hivyo,Kwa muda mrefu kumekuwepo nguvu kubwa na mikakati haramu na ya makusudi ya serikali na chama tawala kudhibiti utashi wa wananchi katika kuamua ni chama gani, na ni mtanzania gani wa kuwaongoza, Kasi hii imekuwa ikiongezeka siku hadi siku, uchaguzi hadi uchaguzi.
Nguvu hii imesababisha baadhi ya watanzania kuondokewa na imani, baadhi ya watanzania sasa hawaamini kama sanduku la kura linaweza kubadilisha uongozi na hatimaye kujiondoa kwenye minyororo ya umasikini ambayo serikali imewafunga.
Serikali ya CCM kushindwa kufikia matarajio ya watanzania sanjari na mikakati ya maksudi ya chama tawala kukataa kuondoka madarakani hata katika maeneo ambayo wananchi wamefikia ukomo wa uvumilivu kunatoa mwito kwa vyama vya siasa makini kujiimarisha zaidi, kukusanya nguvu za wanyonge ili kwa pamoja kutengeneza nguvu kubwa ili kulikomboa taifa lao! Huo ndio msingi wa TUMAINI JIPYA!kutoa fursa nyingine kwa watanzania kujikomboa badala ya kukata tamaa!.
CHADEMA tunaamini kuwa matatizo ya nchi hii ni matokeo ya mfumo mbovu tulionao, mfumo ambao kwa kiasi kikubwa haujatokana na maamuzi ya watawaliwa.Na hii ndio sababu mabadiliko ya sura za viongozi yameshindwa na hayawezi asilan kuzaa tija bali kuzidi kuwakatisha tamaa!
Uzinduzi mpya wa CHADEMA unalenga kuwajengea watanzania Imani, Matumaini na Mwelekeo kwa kuamini kuwa watanzania wengi wamechoka na utawala uliopo, Hivyo CHADEMA inatoa fursa kwa watanzania wote wenye lengo la kuikomboa nchi yao tuungane ili kwa pamoja tujenge Taifa lenye mwelekeo, Taifa ambalo raia wake wana Imani na Matumaini ya maisha, wana matumaini ya mustakabali wa taifa lao kwa miongo na karne kadhaa zijazo.