Baada ya uchaguzi mkuu wa 2005 chama kilituma timu katika wilaya mbalimbali kukusanya maoni kuhusu kama kunahitajika mabadiliko ndani ya chama. Mapendekezo ya wanachama ndiyo yamekisukuma chama kufanya maabadiliko katika Katiba.
Tumefanya marekebisho ya katiba ya chama hususani katika itikadi, muundo na wajibu. Hii ni alama ya mabadiliko ya kweli. Tunasema kwa maneno na kwa vitendo. Mabadiliko yanawezekana. Tunaamini mabadiliko ya kweli yanaanzia ndani. Wanasosholojia wanasema “Mabadiliko huanzia kwangu”. Huu ndio ujumbe ambao tunamwambia kila Mtanzania - ‘badilika, tuibadili nchi yetu’.
Tumeweka bayana itikadi yetu. Hapo nyuma tulisema CHADEMA inaamini katika falsafa na itikadi ya nguvu na mamlaka ya umma. Sasa tumeamua kuweka bayana falsafa yetu na itikadi yetu. CHADEMA tunaendelea kuwa na falsafa ya nguvu na mamlaka ya umma. Huu ni msimamo wetu wa asili: Kwamba falsafa ya CHADEMA ni kuamini katika “Nguvu na Mamlaka ya Umma” (People’s Power) katika kumiliki, kuendesha, kubuni na kuendeleza mawazo, raslimali, uchumi na siasa za nchi. Aidha, falsafa ya nguvu na mamlaka ya umma ndiyo msingi na chimbuko la kuundwa kwa dola ya nchi na kuwa umma ndio wenye madaraka ya mwanzo na mwisho katika kuamua hatma ya nchi na taifa pasipo kuingiliwa, kudanganywa, kutakrimiwa au kughilibiwa na viongozi, watawala au wageni....hivyo basi, falsafa ya “nguvu na mamlaka ya Umma” ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vinavyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na haki. Hii ni falsafa tuliyokuwa nayo ambayo tunaiendeleza.
Kwa upande mwingine tumepitia madhumuni ya kuanzishwa kwa CHADEMA pamoja na sera za chama. Tumejitafakari kiitikadi na kuona tutamke bayana katika katiba yetu tuko wapi. Leo tunatamka kwamba Mkutano mkuu wetu umeamua kwa kauli moja kwamba CHADEMA ni chama cha itikadi ya MRENGO WA KATI (center party). Leo tunazindua kijitabu cha muhtasari wa falsafa na itikadi ya CHADEMA kama sehemu ya kuchochea mjadala kuhusu falsafa na itikadi katika nchi yetu. Kwangu mimi itikadi ni imani. Ni imani inayotuunganisha. Ni imani inayotuongoza. Ni imani inayotuelekeza. Ni imani tunayoielekea. Dhana ya “Mrengo wa kati” pengine itaeleweka vyema kama nitasimulia kisa cha dola moja ya kifalme kama ifuatavyo;
“Katika ufalme huo palikuwa na baraza ambalo lilikuwa na wajumbe wa makundi matatu. Kundi moja lilikuwa upande wa kulia: Hili lilikuwa ni kundi la watawala, wakati wote lilitetea utawala, nidhamu ya kijamii na maslahi ya watu binafsi. Kundi la pili lilikaa upande wa kushoto: Hili lilikuwa likitetea umuhimu wa dola kuhudumia wananchi ikiwemo umiliki wa pamoja wa njia zote za uzalishaji mali na kuweka mkazo katika haki za matabaka. Kundi la tatu lilikaa katikati: Hili lilikuwa likitetea umuhimu zaidi wa dola kuwawezesha wananchi, likiweka mkazo katika uhuru na uwezekano wa kuboresha maisha ya mwanadamu na jamii. Kundi hili la tatu ndio asili ya itikadi ya mrengo wa kati.
CHADEMA ni chama cha mrengo wa kati kwa mujibu wa madhumuni yake na sera zake. Mathalani, ukipitia madhumuni ya kiuchumi ya CHADEMA, utabaini kuwa ni chama kinachoamini kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutumia raslimali za nchi yetu bila kuathiri uhuru wa Taifa, na kuhakikisha kuwa umma kwa ujumla unanufaika na raslimali zao. CHADEMA inaamini katika kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huru, utakaoheshimu na kulinda haki na mali za watu, biashara huru na sekta ya watu binafsi bila kupoka mamlaka ya umma katika maeneo nyeti. Tunaamini katika soko huru sio soko holela. CHADEMA inaamini kuhakikisha matumizi bora ya raslimali asilia za nchi ili zichangie kikamilifu katika pato la taifa na hasa kuboresha huduma za kiuchumi zinazotumiwa na wananchi wote.
Pia CHADEMA kinayo misingi muhimu katika sera na ajenda zake inayokiweka chama katika Mrengo wa Kati. Tunaamini katika uzalendo na kuthamini mila na desturi zetu zilizo nzuri. Tunaamini katika uhuru chini ya sheria zilizo nzuri. Tunaamini katika siasa ambazo ziko juu ya vyama zenye kusimamia zaidi maslahi ya Taifa. Tunaamini katika umuhimu wa dini katika kujenga maadili ya mwanajamii mmoja mmoja bila kuifanya dini kuwa sehemu ya dola. Tunaamini taifa linaundwa na watu, hivyo uhai wake unawategemea watu, na mabadiliko yake yanatokana na watu. Tunaamini kumiliki raslimali na mali miongoni mwa wananchi kunawapa uhuru zaidi hivyo tunataka kujenga chama na baadaye taifa lenye kutoa fursa, ambapo kila mtu bila kujali asili na hali yake anaweza kutimiza na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake. Hizi ni baadhi tu ya sababu zinazofanya CHADEMA kuwa chama cha mrengo wa kati.
Hatahivyo, hatuamini kwamba itikadi ni suluhisho pekee la matatizo katika taifa. Tutaendelea na utamaduni wetu wa kuwa na itikadi laini (relaxed ideology) badala ya itikadi iliyojibana (restrictive ideology). Tutaendelea na msimamo wetu wa kutaka mabadiliko kwa vitendo (pragmatism). Hiyo ni imani, matumaini na mwelekeo wetu.