Blogu ya Mkurugenzi wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.

Friday, September 29, 2006


DOKEZO KUHUSU UZINDUZI MPYA WA CHADEMA ULIOFANYIKA 13 AGOSTI 2006

Na John John Mnyika

“Ukiona kobe ameinama ujue anatunga sheria” na “kimya kirefu kina mshindo mkuu”. Leo ni siku ya kipekee na ya muhimu sana, si tu kwa chama chetu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), lakini pia kwa wazalendo, wanaharakati, na watanzania wote kwa ujumla. Historia na hali ya chama chetu na vyama vya upinzani kwa ujumla hususani baada ya uchaguzi mkuu uliopita, ndivyo hasa vinavyojenga upekee na umuhimu wa sikuu hii.

Mtakumbuka kuwa miaka kumi na tatu iliyopita CHADEMA ilizinduliwa rasmi baada ya kupata usajili wa kudumu tarehe 1 Julai, 1993 chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wakati huo, waasisi wa chama chetu waliweka bayana imani, matumaini na mwelekeo wa CHADEMA. Toka wakati wa Mzee Edwin Mtei na wenzake, ambaye leo tumemzawadia kwa kuthamini mchango wake kama muasisi na mwenyekiti wa kwanza; Kwenda wakati wa Mzee Bob Makani na wenzake, ambaye leo tumemzawadia kama ishara ya kutambua utumishi wake uliotukuka alipokuwa mwenyekiti wa pili wa CHADEMA. Na sasa wakati wangu Freeman Mbowe na wenzake. Leo historia inaandikwa tena kwa kufanya uzinduzi mwingine. Hii ni ishara ya mwendelezo wa imani, matumaini na mwelekeo wa kweli wa CHADEMA chini ya misingi iliyowekwa na waasisi wa chama hiki.

Nini hatma ya upinzani katika muktadha wa matokeo ya uchaguzi 2005 na utawala wa awamu ya nne?

Tumekuwa kimya kidogo tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu 2005, uchaguzi uliokipa chama tawala ushindi wa asilimia themanini katika nafasi ya uraisi na upinzani kupata idadi ndogo ya wawakilishi wa ubunge na udiwani. Kwa ujumla matokeo yameonesha kuwa upinzani umeporomoka. Bila shaka ni vyema kwanza nikachukua fursa hii kugusia swali ambalo baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza pasipo kuwa na jibu ilhali wengine wakitoa majibu ya kupotosha: Nini hatma ya upinzani Tanzania baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu 2005?. Ama kwa maneno mengine, Upinzani umekufa au unaelekea kufa?. Sina nia ya kujibu swali hili kwa kina kwa kuwa leo si mahali pake. Leo tunafanya uzinduzi wa CHADEMA. Lakini kwa kuwa CHADEMA kinaitwa ‘chama cha upinzani’ naona ni vyema nidokeze hoja kadhaa kuchochea mjadala zaidi kuhusu swali hilo. Hii ni kwa sababu imani, matumaini na mwelekeo wa CHADEMA unategemea pia mtazamo mwafaka wa watanzania kuhusu swali hilo.

Nianze kwa kuweka bayana kwamba sipendezwi na jina – ‘vyama vya upinzani’. Sisi wanachadema tunapenda kukiita CHADEMA- ‘chama mbadala’. Vyama hivi vinavyoitwa vya upinzani ni vyama ambavyo kwa malengo ya muda mfupi vinalenga kutoa fikra na sera mbadala. Havijaanzishwa kwa ajili ya kupinga tu!. Hivi ni vyama ambavyo kwa malengo ya muda mrefu vinalenga kuchukua dola na kutekeleza misingi na mipango mbadala. Ni serikali zinazosubiri. Sasa je, vyama mbadala vimekufa au vitakufa? Mimi nasema hapana. Vyama mbadala makini havijafa na haviwezi kufa. Labda “vyama magirini”. Nadokeza sababu kumi na tatu zifuatazo kuthibitisha hilo:
· Mosi, sababu zilizotufanya tuanzishe mfumo wa vyama vingi,ziwe ni za ndani au za nje bado zipo. Mathalani haja ya kupanua wigo wa demokrasia na kuchochea utawala bora na wenye uwajibikaji bado ipo. Na kwa mantiki hiyo vyama mbadala vitaendelea kuwepo.
· Vipo vyama mbadala ambavyo mpaka sasa vimeonyesha mchango wao kwa taifa. Ukichambua toka mfumo wa vyama vingi uanze kuna maamuzi ya kisera yamefanyika kutokana na hoja ambazo ziliibuliwa na vyama vinavyoitwa vya upinzani. Hata katika utawala wa awamu ya nne, kuna mambo kadhaa ambayo serikali imeyachukua kutoka upinzani. Hii ni sababu tosha ya raia makini kutaka upinzani uendelee kama vyanzo vya sera mbadala.
· Pamoja na uchache wa ‘wapinzani’ katika vyombo vya maamuzi mchango wao wa hoja katika kuiwajibisha serikali umeonekana. Imefikia hatua kwamba raia wengi wanatamani wapinzani wengi zaidi wawepo bungeni. Hii ni sababu ya upinzani kuendelea kuungwa mkono na kuhamasishwa kuendelea kuwepo.
· Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha kuwa vipo vyama ambavyo vina uwakilishi katika vyombo vya maamuzi. Vyama hivi vinavyoitwa vya upinzani pia ni vyama tawala baadhi ya maeneo, mathalani CHADEMA inayotawala halmashauri za karatu na kigoma ujiji. Kwa hiyo haviwezi kufa kwa sababu za kawaida.
· Matatizo ya wananchi bado yapo pamoja na ahadi nyingi. Shida wanazopata wananchi ni sababu tosha ya wao kuwa wapinzani wa mfumo uliopo. Hali hii inaota mizizi zaidi pale wanaposhindwa kuona matokeo yanayoshikika ya uongozi ulioko madarakani.
· ‘Vyama makini’ vya upinzani vinapata nguvu kadiri ‘vyama magirini’ vinavyozidi kupuputika na wakati huohuo vyama mbadala kushirikiana. Vyama hivi vinazidi kuwa katika nafasi ya kukua na kukomaa kadri mamluki wanavyozidi kugundulika siku hata siku na kurudi walikotoka.
· Uzoefu kutoka katika nchi nyingine unaonyesha hata katika hali bora ya maisha upinzani unaendelea kushamiri. Hivyo raia wakati wote wanaendeleza upinzani ili kupata kilicho bora zaidi.
· Vipo vyama vyenye mtandao wa wanachama na wapenzi ambao upinzani uko ndani yao. Upinzani kwao ni suala la kuendelea. It’s a going concern
· Upo upinzani ndani ya mfumo wenyewe wa utawala, upinzani huu ni chanzo kingine cha upinzani wa nje kuendelea kukua.
· Jitihada za kuhujumu na kubomoa upinzani zinaishia katika mambo yanayoshikika tu mathalani ‘kununua vijiwe vya wakereketwa’, upinzani kama fikra, mawazo na imani unaendelea kushamiri katika nafsi za watu. Huu haujafa wala hautakufa mpaka fikra, mawazo na imani vitakapo kufa.
· Vipo vyama vya upinzani ambavyo vimekuwa kisiasa na vinaendelea kujipanga na kujijenga ikiwemo kukabiliana na vikwazo. Hivi vinaonyesha kutokufa na badala yake vinazidi kukua.
· Wapo watu wanaoingia upinzani kutoka katika mfumo wa utawala kama ambavyo wapo wanaotoka katika upinzani kurudi katika chama tawala. Lakini wachunguzi wa mambo wanafananisha wengine wanaotoka upinzani sawa na wale wanaolezewa kwenye vitabu vitakatifu, waliopata taabu jangwani kisha wakawaomba manabii wawarudishe utumwani walipokuwa karibu na masufuria ya nyama. Kwa maneno mengine, ni wapinzani wa kweli pekee ndio wanaosimama kidete kuifikia nchi ya ahadi
· Nasisititiza kuwa vyama vinavyoitwa vya upinzani hususani CHADEMA, havijafa na wala havielekei kufa kwa sababu, “Maendeleo ya kweli hayawezi kuletwa na mafisadi walewale wa chama kilekile chenye uoza ule ule wakiendeleza yale yale eti kwa ari mpya, nguvu mpya, na kasi mpya”. Vyama mbadala hasa CHADEMA vitaendelea kupigania maendeleo ya kweli pasipo kuchoka.
Tunaweza kuzijadili vizuri sababu hizi kwa kuchambua historia ya CHADEMA kama mfano wa kutazama ilipotoka, ilipo na inapokwenda baada ya uchaguzi mkuu wa 2005.

Nini nafasi ya CHADEMA katika siasa Tanzania chini ya muktadha huo?

Pamoja na kushindwa uchaguzi mkuu wa 2005, CHADEMA imeongeza idadi ya wabunge kutoka 5 hadi 11 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 110 na kuongeza idadi ya kura za ujumla za ubunge kutoka asilimia 4.23 mpaka 8.2. ambayo ni asilimia 100. Ruzuku ya chama imeongezeka kutoka milioni 5.6 kwa mwezi mpaka milioni 35.5 na hivyo kutoa nguvu nyingine ya chama kuweza kujijenga kisiasa. CHADEMA ndicho chama cha upinzani chenye wabunge wengi Tanzania bara. Tulisimamisha mgombea Urais kwa mara ya kwanza na kushika nafasi ya tatu. Jumla ya madiwani imeongezeka kutoka 64 mwaka 2000 mpaka 99 katika uchaguzi 2005. Kwa upande wa Zanzibar chama kimeweza kusimamisha wagombea wengi zaidi kuliko chaguzi zingine na kushika nafasi ya tatu katika kura za ubunge katika majimbo mengi na kujitambulisha kama nguvu ya tatu katika siasa za visiwani. Matokeo haya yamepatikana kwa rasilimali ndogo na kwa maandalizi madogo yaliyofanywa muda mchache kabla ya uchaguzi tena katika mazingira ya ‘rafu za kisiasa’. Vipo vyama ambavyo vimeendelea kupata uwiano ule ule wa kura na vingine vimeporomoka. CHADEMA ndicho chama pekee kikubwa cha upinzani ambacho kimekua na kinaendelea kukua kisiasa.

Mambo gani ya pekee ambayo CHADEMA imeyapata kutokana na uchaguzi 2005?
Uchaguzi wa mwaka 2005 unaonesha kuwa CHADEMA ni chama chenye sura ya utaifa na kitaifa. Tulisema wazi wakati wa kampeni “Tanzania kwanza”. Mwaka 2005 ulishuhudia CHADEMA ikisimamia kidete masuala ya utaifa. Kuanzia haja ya wananchi kumiliki na kunufaika na raslimali na maliasili zetu. Mpaka kwenye mijadala kuhusu uzalendo na alama za taifa mathalani bendera na haja ya kuwaenzi kwa vitendo waasisi wa taifa hili hususani Mwalimu Nyerere. Yote yalitoa mwelekeo wa misimamo yetu kuhusu utaifa.

CHADEMA ilichukua sura ya kitaifa katika kampeni, ikipendwa kuanzia kusini mwa Tanzania mpaka kaskazini. Kutoka magharibi mpaka mashariki. Matokeo ya uchaguzi yanadhihirisha mwelekeo huu wa kitaifa. Tumepata ushindi katika kona mbalimbali za nchi yetu. Kutoka Karatu huko Arusha mpaka Mpanda Kati mkoani Rukwa. Kutoka Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro mpaka Kigoma Kaskazini huko Kigoma. Tumesambaa zaidi na kushinda hata Tarime mkoani Mara. Tumeendelea kuwa chama tawala katika halmashauri ya Karatu na kutawala kwa mseto katika halmashauri ya Kigoma Ujiji. Na madiwani wetu 99 nao wamesambaa katika kila pahali nchini. Katika kila mkoa lazima kuna majimbo au jimbo ama walau kata ambapo tuna na nguvu kubwa kisiasa. CHADEMA ni chama cha utaifa na cha kitaifa. Hii ni mbegu ya mwelekeo tuliyoipanda mwaka 2005.

Nini chanzo cha uzinduzi mpya wa CHADEMA?

Naam! “Kobe akiinama ujue anatunga sheria” na “kimya kirefu kina mshindo mkuu”. CHADEMA tulikuwa kimya tukijipanga. Baada ya uchaguzi tulikaa kimya na kuibuka kwenye vikao vya kamati kuu na baraza kuu la chama tukitathmini kwa kina uchaguzi na kuandaa mikakati ya hatua za awali. Tulikaa kimya tena na kutuma timu zetu katika wilaya mbalimbali kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya chama. Leo tumemaliza mkutano mkuu wa chama, na sasa ni wakati wa kazi. Tunaumaliza ukimya wetu kwa kishindo kwa kuizindua upya CHADEMA baada ya zaidi muongo mmoja tangu kuasisiwa kwake.

Tunafanya hivi kujenga chama imara na makini zaidi ili kuongeza ufanisi katika ushindani demokrasia ya vyama vingi. Tunazindua mchakato wa kwanza unaohusisha zaidi mabadiliko ya kimuundo na zana kisha tutaanza mchakato wa maboresho ya kisera na uongozi. Tunazindua alama na zana sita za CHADEMA. Ndani ya alama na zana hizi upo ujumbe mahsusi kwa wanaCHADEMA na watanzania. Alama na zana hizi ni ishara tu ya imani, matumaini na mwelekeo wetu kwa mustakabali wa chama na taifa letu.. Tunatazama mbali, tukiwa na imani, matumaini na mwelekeo.



Uzinduzi wa mpango mkakati wa CHADEMA 2006 na mpaka 2010 ni nini?

Mosi, tunazindua rasmi utekelezaji wa Mpango Mkakati wa CHADEMA kuanzia 2006 mpaka 2010. Mpango Mkakati ni dhana iliyotoka katika medani ya kivita. CHADEMA tunaitumia dhana hii je tunajipanga kuingia msituni? Naam, tunaingia vitani kwa silaha ya demokrasia ili kupambana na maadui ambao tunao katika ngazi mbili. Ya kwanza ni maadui wanaowakabili wananchi-ujinga, umaskini, maradhi na ufisadi. Ya pili ni mfumo uliowekwa na chama tawala. Hivyo tunajipanga kupambana kwa kutumia siasa na si silaha, ili kutumia uongozi kuleta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli. Mpango Mkakati ni dhana inayotufanya kutambua nguvu na kuzitumia, kufahamu fursa na kuziendea, kubaini udhaifu na kuuondoa na kugundua vikwazo na kuviepuka ili kupata ushindi. Katika medani ya maendeleo, Mpango Mkakati tunaweza kuulezea kuwa ni mpangilio unaoelekeza tulipotoka, tulipo, tunapotaka kwenda na namna tutakavyokwenda. Katika Mpango Mkakati huu, yapo mambo ambayo tumedhamiria kuyafanya kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kweli ndani ya chama. Pia yapo mambo ambayo tumedhamiria kuyasimamia kuleta mabadiliko ya kweli nje ya chama,kwa maneno mengine, katika taifa kwa ujumla. Mpango Mkakati huu una mambo mengi, mengine ni siri za ushindi. Kwa mantiki hiyo, nadokeza machache tu:

Kwa ndani tumepanga kujiendesha kama “chama taasisi” na “chama uchaguzi”. Tumemaliza kampeni ya uchaguzi mkuu. Sasa tunaendesha kampeni ya mabadiliko na maendeleo. Tutaendelea kufanya mabadiliko mbalimbali ndani ya chama pamoja na kuboresha mtandao wa chama ikiwemo vijijini. Baadhi ya mabadiliko ya alama na zana ambayo tumeshayatekeleza tunayazindua leo. Kwa upande mwingine tumejipanga kuwa sauti ya wasio na sauti tukitetea, kuendeleza na kutekeleza mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli. Tumedhamiria kusimamia uwajibikaji wa serikali na kuishinikiza kutekeleza ahadi ilizozitoa. Tutaendelea kuwa wenye mtizamo chanya na wenye kujenga katika kuiwajibisha serikali. Na tutakuwa watu wa fikra, wenye nafsi wazi(open mind) na nishati katika kuibua mawazo na kutengeneza sera tunazohitaji kukabiliana na changamoto hususani za muda mrefu ambazo nchi yetu inakabiliana nazo. CHADEMA kinaendelea kuwa moja ya vyanzo vya imani, matumaini na mwelekeo wa Taifa letu.

Tulishaanza hatua hizi kwa kutoa sera mbadala. Zipo ambazo serikali imeamua kuzitekeleza. Hatuna tatizo na hilo maana hiyo pia. ndio faida ya kuwa na vyama mbadala kama CHADEMA . Tatizo letu ni kwamba kwa uzoefu wa huko nyuma na dalili zinavyoonyesha sasa serikali inazitekeleza sera hizi nusu nusu na pengine ovyo ovyo. Tunatoa rai kwa serikali kuchota kwa kina utaalamu wa kutekeleza sera hizi toka kwetu. Mkishindwa kutekeleza ushauri huu ni wazi wananchi watakuwa na sababu ya ziada ya kuwapumzisha katika chaguzi zijazo ili tuingie madarakani kutekeleza sera hizo kwa umakini na ufanisi zaidi. Hayo ndiyo mabadiliko ya kweli yanayotakiwa.


Uzinduzi wa kauli mbiu za ‘Tumanini Jipya’ la “mabadiliko ya kweli, Uhuru wa Kweli”?

Pili, Tunazindua kauli mbiu ya mchakato huu. “Tumaini Jipya”. Hii ni kauli mbiu inayobeba dhana nzima ya “imani, matumaini na mwelekeo”. Kauli mbiu hii itakwenda sambamba na uzinduzi rasmi kauli mbiu ya: “Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli”. Hii ni kauli mbiu tuliyoitumia wakati wa kampeni za uchaguzi.Tunaizindua tena kama ishara ya kuindeleza na kuitekeleza.Wakati wa kampeni tulisema- “ Maendeleo ya kweli hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale wa chama kile kile chenye uoza ule ule wakiendeleza yale yale eti kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. CHADEMA inaamini kwamba kwa falsafa ya Chukua Chako Mapema (CCM), Tanzania yenye neema haitawezekana”, mwisho wa kunukuu. Tuliyasema haya tukitaka mabadiliko ya kweli na hatimaye uhuru wa kweli.

Kwa maneno ya mtaalamu wa siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM), Profesa Mwesiga Baregu aliyoyatoa hivi karibuni, “Ari, Nguvu na Kasi mpya haiwezi kuwa na maana kama hakuna fikra mpya”. Zaidi ya miezi sita imepita toka utawala wa awamu ya nne ukae madarakani, tumeanza kuona haja ya kuendelea kutetea mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli.Tumesikiliza maneno zaidi ya kuona vitendo. Tumeendelea kupata ahadi lakini nyingine zikiwa na hadaa. Tumewauliza wananchi kadhaa wa kawaida swali moja: Je, umeanza kuona japo matumaini ya maisha bora katika hali yako ya kila siku? Jibu la kijana mmoja ambalo kwa muhtasari linatoa mawazo ya wengine ni - “Tunauziwa mbuzi kwenye gunia”.

Hapa ndipo inapokuja haja ya kuendelea kutetea mabadiliko ya kweli, uhuru wa kweli. Raisi Kikwete na Waziri Mkuu Lowasa walianza kwa hekaheka. Lakini mfumo unaelekea kuwakwaza. Na hii ni wazi kama alivyotoa wosia Mwalimu Nyerere kwenye kitabu cha uongozi wetu na hatma ya Tanzania- nchi yetu imeoza. “Our country is rotten to the core”. Tunahitaji mabadiliko ya kimfumo. Ndio maana tumedhamiria kutetea na kutekeleza mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli. Katika ngao na wimbo wa Taifa ipo ndoto yetu watanzania: “Uhuru na Umoja”. Hii ni ndoto ya pamoja bila kujali itikadi. Ni ndoto tuliyorithi toka kwa waasisi wa Taifa letu. Wakati wa kudai uhuru, viongozi wetu waliweka bayana kwamba tunataka uhuru ili tuondokane na umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi ambavyo mkoloni alishindwa kuviondoa. Hatuwezi kusema tuna umoja katika taifa lenye pengo kubwa baina ya maskini na matajiri. Hatuwezi kusema tuna umoja katika ubaguzi. Nia ya kudai uhuru ilikuwa ni kuondoa maadui hawa na matokeo ya uhuru ni taifa lenye elimu, afya, utajiri na uongozi bora. Bado hatujafika. Ndio maana tunasema, ni wakati wa kuendeleza na kutekeleza mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli. Katika hali hii, nawakumbusha tena, “Hakuna Kulala, Mpaka Kieleweke”. Hakuna kulala, tuendeleze mabadiliko ya kweli. Mpaka kieleweke! Kikieleweka tutakuwa na uhuru wa kweli. Huwezi kulala kwa furaha katika ujinga, huwezi kulala kwa raha katika umaskini, utalala kwa karaha katika maradhi, huwezi kulala katika ufisadi. Hivyo hakuna kulala mpaka kieleweke. Mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli ni sehemu ya imani, matumaini na mwelekeo tunaouzindua leo.

Uzinduzi wa marekebesho ya katiba ya CHADEMA ni nini?;

Tatu, tunazindua marekebisho ya katiba ya CHADEMA. Tumefanya marekebisho ya katiba ya chama hususani katika itikadi, muundo na wajibu. Hii ni alama ya mabadiliko ya kweli. Tunasema kwa maneno na kwa vitendo. Mabadiliko yanawezekana. Tunaamini mabadiliko ya kweli yanaanzia ndani. Wanasosholojia wanasema “Mabadiliko huanzia kwangu”. Huu ndio ujumbe ambao tunamwambia kila mtanzania-‘badilika, tuibadili nchi yetu’.

Tumeweka bayana itikadi yetu.Hapo nyuma tulisema CHADEMA inaamini katika falsafa na itikadi ya nguvu na mamlaka ya umma. Sasa tumeamua kuweka bayana falsafa yetu na itikadi yetu. CHADEMA tunaendelea kuwa na falsafa ya nguvu na mamlaka ya umma. Huu ni msimamo wetu wa asili: Kwamba falsafa ya CHADEMA ni kuamini katika “nguvu na Mamlaka ya Umma”(People’s Power) katika kumiliki, kuendesha, kubuni na kuendeleza mawazo, raslimali, uchumi na siasa za nchi. Aidha, falsafa ya nguvu na mamlaka ya umma ndiyo msingi na chimbuko la kuundwa kwa dola ya nchi na kuwa umma ndio wenye madaraka ya mwanzo na mwisho katika kuamua hatma ya nchi na taifa pasipo kuingiliwa, kudanganywa au kughilibiwa na viongozi, watawala au wageni....hivyo basi, falsafa ya “nguvu na mamlaka ya Umma” ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma, ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa, na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vinavyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na haki. Hii ni falsafa tuliyokuwa nayo ambayo tunaiendeleza.

Kwa upande mwingine tumepitia madhumuni ya kuanzishwa kwa CHADEMA pamoja na sera za chama. Tumejitafakari kiitikadi na kuona tutamke bayana katika katiba yetu tuko wapi. Leo tunatamka kwamba Mkutano mkuu wetu umeamua kwa kauli moja kwamba CHADEMA ni chama cha itikadi ya MRENGO WA KATI(center party). Leo tunazindua kijitabu cha muhtasari wa falsafa na itikadi ya CHADEMA kama sehemu ya kuchochea mjadala kuhusu falsafa na itikadi katika nchi yetu. Kwangu mimi itikadi ni imani. Ni imani inayotuunganisha. Ni imani inayotuongoza. Ni imani inayotuelekeza. Ni imani tunayoielekea. Dhana ya “Mrengo wa kati” pengine itaeleweka vyema kama nitasimulia kisa cha dola moja ya kifalme kama ifuatavyo;

“Katika ufalme huo palikuwa na baraza ambalo lilikuwa na wajumbe wa makundi matatu. Kundi moja lilikuwa upande wa kulia: Hili lilikuwa ni kundi la watawala, wakati wote lilitetea utawala, nidhamu ya kijamii na maslahi ya watu binafsi. Kundi la pili lilikaa upande wa kushoto: Hili lilikuwa likitetea umuhimu wa dola kuhudumia wananchi ikiwemo umiliki wa pamoja wa njia zote za uzalishaji mali na kuweka mkazo katika haki za matabaka. Kundi la tatu lilikaa katikati: Hili lilikuwa likitetea umuhimu zaidi wa dola kuwawezesha wananchi, likiweka mkazo katika uhuru na uwezekano wa kuboresha maisha ya mwanadamu na jamii. Kundi hili la tatu ndio asili ya itikadi ya mrengo wa kati.

CHADEMA ni chama cha mrengo wa kati kwa mujibu wa madhumuni yake na sera zake. Mathalani, ukipitia madhumuni ya kiuchumi ya CHADEMA, utabaini kuwa ni chama kinachoamini kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kutumia raslimali za nchi yetu bila kuathiri uhuru wa Taifa, na kuhakikisha kuwa umma kwa ujumla unanufaika na raslimali zao. CHADEMA inaamini katika kujenga na kuimarisha uchumi wa soko huru, utakaoheshimu na kulinda haki na mali za watu, biashara huru na sekta ya watu binafsi bila kupoka mamlaka ya umma katika maeneo nyeti. Tunaamini katika soko huru sio soko holela. CHADEMA inaamini kuhakikisha matumizi bora ya raslimali asilia za nchi ili zichangie kikamilifu katika pato la taifa na hasa kuboresha huduma za kiuchumi zinazotumiwa na wananchi wote.

Pia CHADEMA kinayo misingi muhimu katika sera na ajenda zake inayokiweka chama katika Mrengo wa Kati. Tunaamini katika uzalendo na kuthamini mila na desturi zetu zilizo nzuri. Tunaamini katika uhuru chini ya sheria zilizo nzuri. Tunaamini katika siasa ambazo ziko juu ya vyama zenye kusimamia zaidi maslahi ya Taifa. Tunaamini katika umuhimu wa dini katika kujenga maadili ya mwanajamii mmoja mmoja bila kuifanya dini kuwa sehemu ya dola. Tunaamini taifa linaundwa na watu, hivyo uhai wake unawategemea watu, na mabadiliko yake yanatokana na watu. Tunaamini kumiliki raslimali na mali miongoni mwa wananchi kunawapa uhuru zaidi hivyo tunataka kujenga chama na baadaye taifa lenye kutoa fursa, ambapo kila mtu bila kujali asili na hali yake anaweza kutimiza na kufanikiwa kadiri ya vipaji vyake. Hizi ni baadhi tu ya sababu zinazofanya CHADEMA kuwa chama cha mrengo wa kati.

Hatahivyo, hatuamini kwamba itikadi ni suluhisho pekee la matatizo katika taifa. Tutaendelea na utamaduni wetu wa kuwa na itikadi laini (relaxed ideology) badala ya itikadi iliyojibana (restrictive ideology). Tutaendelea na msimamo wetu wa kutaka mabadiliko kwa vitendo (pragmatism). Hiyo ni imani, matumaini na mwelekeo wetu.


Yapi ya ziada kuhusu marekebisho ya katiba ya CHADEMA?

Tumezindua marekebisho ya katiba ya CHADEMA yaliyofanywa na mkutano mkuu maalumu uliomalizika leo. Katika mabadiliko haya tumeboresha pia muundo wa chama na kuweka mkazo wajibu wa wanachama. CHADEMA inauchukulia muundo wa chama kama nyenzo muhimu ya kuwezesha ufanisi kwa kuzingatia malengo ya chama na mazingira ya kisiasa na kiutawala katika jamii. Tumepunguza ukubwa wa baadhi ya vyombo katika ngazi mbalimbali hususani mikoa na kupeleka chama katika ngazi ya chini kabisa ambayo tumeiita “Msingi”. Huu ni muundo ambao utarahisisha mawasiliano katika ngazi mbalimbali za uongozi na kuwezesha ushiriki/ushirikishwaji wa wanachama hasa ngazi za chini na kumilikisha zaidi chama kwa wanachama kwa ujumla. Muundo wa sasa unaendana na ukubwa wa chama kitaasisi na hivyo utapunguza gharama za uendeshaji. Muundo wa sasa unapeleka chama zaidi katika vitovu vya mapambano ya kisiasa.

Tumebadili muundo wa chama kutoa nafasi zaidi kwa makundi ya kijamii ya wanawake, wazee na vijana. Katiba ya sasa imetoa mwanya wa kuundwa kwa mabaraza ya wanawake, wazee na vijana. Pia tumeweka katika muundo wetu wa chama nafasi maalumu kwa ajili ya wenye ulemavu na kuwa chama cha kwanza kufanya hivyo katika muundo wake wa kikatiba. Tumeweka bayana mamlaka za kinidhamu pamoja na kuboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro. Tumeweka mkazo kwenye wajibu wa mwanachama. Tunasisitiza kwamba chama cha siasa ni mjumuiko wa watu mbalimbali wenye imani inayofanana wenye lengo la kuchukua dola ili kuhakikisha imani hiyo inatekelezwa kwa maslahi ya taifa. Chama ni wanachama na uhai wa chama unategemea wanachama. Hivyo kila mwanachama anawajibu wa kutoa mchango wake wa hali na mali katika kutekeleza malengo ya chama. Mabadiliko haya ya kimuundo na kiwajibu yatakuwa msingi muhimu wakati tutakapoanza kujenga chama kuanzia katika ngazi ya chini kabisa ikiwemo vijijini. Tumeanzisha mabalozi wa kaya kumi na kuingiza mfumo wa ngazi ya majimbo kadiri ya sera yetu ya majimbo. Hii ni sehemu ya imani, matumaini na mwelekeo wetu.

Uzinduzi wa bendera mpya ya CHADEMA ni nini?

Nne, tunazindua na kupandisha bendera mpya ya CHADEMA. Ni alama nyingine ya imani, matumaini na mwelekeo wetu.

Kimuundo bendera ya CHADEMA ina rangi nne: Nyeusi, Bluu isiyokoza(light blue), nyeupe na nyekundu.

Bendera ya CHADEMA ina nembo ya kiganya cha mkono kilichonyoosha vidole viwili katika mfumo wa V kama ishara ya USHINDI. CHADEMA ni chama kinacholenga kushinda kidemokrasia na hatimaye kuleta ushindi wa maendeleo ya taifa.

Rangi ya BLUU ISIYOKOZA iko juu ya rangi NYEKUNDU kama ishara kwamba kama taifa tumevushwa na mashujaa kuelekea katika jamii yenye haki, na wakati wote CHADEMA imevuka hatua kama chama cha siasa na sasa inasimamia haki.

Rangi nyeupe iko mbele ya rangi zote kama ishara kwamba chama kinatanguliza UKWELI NA UWAZI katika nyanja zote. Pia rangi nyeupi imebeba nembo ya chama kwa kuwa UKWELI NA UWAZI ni misingi muhimu sana kwa chama. Nembo ya chama iko mbele kama kama ishara ya CHADEMA kuwa chama kiongozi katika kuchochea misingi muhimu katika kuleta mabadiliko na maendeleo katika Taifa.

Rangi zingine zinatenganishwa na ufito mweusi ambao unaumbo la “T” ikiwasilisha kifupi cha jina la taifa la Tanzania.


RANGI ZA BENDERA:

NYEUSI
Rangi hii inawakilisha WATU WA TANZANIA. Hii ni rangi ya wazawa asili wa nchi yetu. Ni rangi ambayo inabeba pia falsafa ya NGUVU YA UMMA.

BLUU ISIYOKOZA (LIGHT BLUE)
Hii ni rangi ya asili ya CHADEMA. Ni rangi ambayo inawasilisha HAKI. Lakini pia rangi hiyo inawakilisha BAHARI kama ishara ya maliasili/raslimaji na Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

NYEUPE
Rangi nyeupe inawasilisha UKWELI, UWAZI na AMANI. Huu ni msingi muhimu wa CHADEMA. CHADEMA ni chama ambacho kitasimamia uadilifu kwa njia ya demokrasia.

NYEKUNDU
Rangi nyekundu inawakilisha MASHUJAA. CHADEMA inathamini historia ya nchi yetu ambayo inawasilisha kumbukumbu ya mashujaa waliotupitisha katika michakato ya mbalimbali ya demokrasia na maendeleo ikiwemo harakati za kuondoa ukoloni. Rangi ni chimbuko la uzalendo wetu.


Uzinduzi wa kadi mpya ya CHADEMA nini?

Tano, tunazindua kadi mpya za uanachama wa CHADEMA. Tumeamua kuleta imani, matumaini na mwelekeo zaidi katika uanachama sasa tutaanza kuandikisha wanachama upya. Tumeamua kusitisha utamaduni wa kutoa kadi bure ingawa kadi za CHADEMA bado zitaendelea kuuzwa kwa bei ndogo ili kila mtanzania aweze kugharamia. Lengo ni kuhakikisha kila anayechukua kadi ya chama anachangia kama ishara ya nia yake ya kuunga mkono chama na harakati za ukombozi wa nchi hii. Tunataka tuwe na wanachama hai chini ya mkakati wa “CHADEMA ni msingi”. Tunataka wanachama wamiliki na kukiendesha chama. Michango hii midogo midogo ikiunganishwa pamoja ni nguvu ya pekee katika kuchochea kujitegemea na kuendesha chama kwa nguvu ya wanachama. Kama ambavyo bahari ni muunganiko wa matone madogo madogo ya maji ndivyo ambavyo michango hii inaweza kukijenga chama. Tunataka uanachama uwe chachu ya imani, matumaini na mwelekeo wa CHADEMA.



Uzinduzi wa wimbo wa CHADEMA kitaifa nini?

Sita, tunazindua wimbo wa CHADEMA. Huu ni wimbo rasmi wa chama utakaoimbwa kote nchini. Ni sauti ya CHADEMA. Ni njia ya kutumia sanaa kuwasilisha hisia, misimamo, hamasa, matamanio na matarajio yetu kuhusu imani, matumaini na mwelekeo wa CHADEMA na taifa. Ni muhtasari wa yote.

Ubeti wa kwanza ni sala. Tunaimba:

MUNGU TUSAIDIE, MUNGU TUWEZESHE,
TANZANIA INA KILIO,
WANAO TWATESEKA MAOVU YANASHAMIRI;
NCHI YATEKETEA WATAWALA WANEEMEKA

Tunakabidhi harakati zetu zote kwa nguvu na mamlaka iliyo asili na juu ya yote. Tunaeleza hali halisi ya Taifa letu. Si kwa kukata tamaa, hapana!. Ni ishara ya kujitambua. Ili kwa nguvu yetu na baraka zake tuweze kutoka tulipo na kuelekea kwenye mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli.Tunaeleza, kwamba tunatambua kuwa hatukuumbwa maskini. Tunathamini utu, maliasili na raslimali ambazo tumepatiwa. Tunajua kuwa tunachokosa ni uongozi bora. Hii ni sehemu ya imani, matumaini na mwelekeo wetu

Ubeti wa pili ni CHADEMA. Tunaimba:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo,
Tumaini la ukombozi wa kiuchumi na kisiasa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
Chimbuko la fikra mpya nayo mikakati ya utumishi
Mtetezi wa uhuru, uhuru wa kweli
Maendeleo ya kweli wanayostahili Watanzania

Mlinzi wa uzalendo raslimali za taifa la Tanzania
Jukwaa la harakati kukomesha ufisadi, na uoza wa kimaadili

Hapa tunatoa suluhisho. Tunaeleza nini ambacho tunatetea. Yapi ambayo tunaendeleza. Na kwa vipi tunatekeleza. Kutoka kudai mabadiliko ya kweli, maendeleo ya kweli mpaka uhuru wa kweli. Tunaweka bayana misingi yetu kama chama. Hii ni sehemu nyingine muhimu ya imani, matumaini na mwelekeo wetu.

Sehemu ya tatu ni Wito: Tunaimba;
Wazee na akina Baba (twende)
Vijana na akina mama (amka)
Pamoja tuna umaskini (tuna maisha duni)
Pamoja tuna uchungu
Watoto nanyi jiungeni (twende)
Tunaweza acheni acheni woga x 2
KIITIKIO: WanaCHADEMA tushikamane
Demokrasia Yawezekana
WanaCHADEMA tushikamane
Maendeleo Yawezekana
Watanzania tushikamane
Mabadiliko Yawezekana
Nguvu ya Umma, People’s Power
Nguvu ya Umma, People’s Power

Hapa tunamalizia wimbo wetu kwa kuchochea hamasa na kutoa wito kwa wote. Ni wito kwa kila mmoja kujiunga nasi katika kuleta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli. Ni wito wa kutuunga mkono katika kuchochea demokrasia na maendeleo. Ni mwamko, uamsho na hamasa.

Sasa nini tufanye?

Wimbo wa CHADEMA umehitimisha kwa kusema kila kitu. Na utuingie katika nafsi zetu. Tusiuimbe kama kasuku, tuuimbe tukiwa na imani, matumaini na mwelekeo. Tuuimbe kwa maneno na kuucheza kwa vitendo. Ndio mchango mwingine ambao tunaweza kutoa kwa CHADEMA, Tanzania na ubinadamu.

Na huu ndio ujumbe wangu kwenu:

Ewe mwanaCHADEMA, usihoji CHADEMA inafanya nini. Jiulize wewe umefanya nini kama mwanachama wa CHADEMA. Chama ni cha wanachama, jumla ya maneno na matendo ya wanachama ndio matokeo ya chama.

Ewe mtanzania, usiulize mfumo wa vyama vingi uko wapi. Jiulize wewe umechangia nini kufanya vyama vya siasa hususani vyama mbadala kama CHADEMA kuendeleza yale unayoyaamini. Kama Mahatma Ghandi alivyosema, “Kuwa wakala wa mabadiliko unayotaka kuyaona”.

Ewe mdau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi, usiulize demokrasia ina hali gani Tanzania. Jiulize, wewe umetoa ushikirikano gani kuwaunga mkono watanzania wenye kutetea, kuendeleza na kutekeleza demokrasia. Michango ya kimaendeleo unayoitoa haitaleta matokeo unayoyataka kama taifa halitakuwa na mifumo ya udhibiti thabiti ikiwemo upinzani makini na wenye nguvu.

Mabadiliko yanawezekana kama kila mmoja akitimiza wajibu. Na tuanze sasa.

Dokezo hili limeandaliwa kwa ajili ya kuwa rejea kwa yoyote anayetaka kufahamu au kufanya uchambuzi kuhusu uzinduzi mpya wa CHADEMA. Mtayarishaji ni Mkurugenzi wa vijana anayepatikana kupitia mnyika@yahoo.com na 0744 694 553