Blogu ya Mkurugenzi wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.

Tuesday, July 25, 2006


Chambelecho cha maadhimisho ya Siku ya Mashujaa: Tunu yangu kwa wakina Kinjeketile

Na John John Mnyika

Kamaradi Kinjeketile na mashujaa wenzako popote mlipo!Hii ni tunu kwenu. Hidaya kwenu mliomwaga damu wakati mapambano kadhaa na Mreno na Mwarabu. Tuzo kwenu nyinyi mliopigana na Ujerumani wakati wa utawala na mliomwaga damu katika vita vya dunia. Heko ninyi ambao damu ilisafisha safari ya kumng’oa Nduli Amin. Heri wewe Sethi Benjamini na wote waliopotesha maisha katika hekaheka za kueneza Azimio la Arusha. Kumbukumbu kwenu mliotoa damu katika mikikimikiki ya mfumo wa vyama vingi kutoka Zanzibar mpaka bara. Damu yenu iliyomwagika haizoleki, ukiwa mlioucha hauzoeleki lakini fikra mlizosimamia hazizeeki. Mapambano bado yanaendelea!

Kwako Bushiri bin Salim wa Tanga, suriama wa kiarabu na kiafrika, pamoja na nia yako tenge ya kulinda maslahi katika biashara ya utumwa ulimwaga damu kwa kunyogwa Pangani baada ya kuongoza maasi makali dhidi ya kuingia kwa ukoloni wa Kijeruamani-damu yako ilimwagika pamoja na damu za wapiganaji wa Pwani, Morogoro mpaka uhehe. Ewe Mtemi Meli, uliowashinda wadachi mpaka mwenzio Sina alipokusaliti hatimaye wewe na mashujaa wenzako mkamwaga damu kaskazini mkilinda uhuru.Wewe Chifu Mkwawa, tunakukumbuka uliovyowaunganisha wahehe-toka Kalenga, Tosamaganga mpaka ulipoamua kuimwaga damu yako mwenyewe kuliko uhuru upotee mikononi mwako. Mtemi Isiki wa Tabora uliendesha mashambulizi ya kishujaa, hatimaye ukaamua kumwaga damu yako na ya familia yako kwa kujilipua na baruti ili tu usipate aibu ya uhuru kuchukuliwa mbele ya macho yako. Ewe Mtemi Makongoro wa Musoma, ulipambana kwa ushujaa mpaka ilibidi kikosi cha wanamaji kiletwe kupitia miji ya Mombasa na Kisumu kukumaliza.

Nakutunuku Kinjeketile kwa kuongoza vita vya kutisha vya Maji Maji kwa miaka kadhaa vilivyoanzia vilima vya Matumbi karibu na Kilwa. Nyinyi mlitaka kumwondoa mkoloni kwa nguvu na mlikuwa tayari kumwaga damu kuliko kuendelea kuishi bila ya uhuru. Mapambano yenu yalisambaa maeneo mengi ya ardhi yetu. Ninyi mlikuwa mashujaa kweli kweli mliojua umuhimu wa imani na falsafa katika mapambano-mkawapa watu ujasiri kwa dawa ya “Kugeuza risasi, Kuwa maji”. Pamoja na kushindwa vita na wazalendo zaidi ya laki moja kupoteza maisha katika wakati ambao ardhi ilikuwa na watu wachache yapo mapigano ambayo mlishinda. Pamoja na machifu 47 wa Kingoni kunyongwa damu yenu ilileta mabadiliko katika utawala. Kwa vyovyote vile damu nyingi kiasi hiki iliyomwagika kwa sababu ya kudai uhuru haiwezi kupuuzwa. Hivyo waraka huu ni tunu kwenu. Mapambano bado yanaendelea!

Nawaandikia waraka huu ninyi wahenga mashujaa muweze kurejea na kurekebisha historia. Najua mnaweza msirudi kimwili, lakini ni vyema kiroho mkandelea kuwa nasi. Fikra zenu za kimapambano hazipaswi kupotea. Kumbukumbu zenu za kishujaa hazistahili kufutika. Taifa lisilo na historia haliishi, linakufa. Kupotosha historia ya mashujaa ni kinyaa. Karibu kila eneo katika nchi yetu yupo shujaa ambaye anaweza kukumbukwa laiti kama historia zenu zingejulikana kizazi hata kizazi na kuwa chimbuko la kujiamini, kujithamini na uzalendo miongoni mwa Watanzania.

Julai 25 ilikuwa siku nyingine ambapo tulifanya maadhimisho ya kinafiki ya siku ya mashujaa. Mtanishangaa kwa kutumia dhana kali- “UNAFIKI”. Namaanisha!. Ni dhana ambayo mnaifahamu na hamkuipenda. Ndio maana hamkutaka kuishi katika unafiki wa kukubaliana ama kutumiwa na watawala. Mkaamua kupambana! Mkamwaga damu mkiukimbia unafiki. Sasa tunawakumbuka!. Lakini nasema tena, tunawakumbuka kwa kufanya maadhimisho ya kinafiki ya siku ya mashujaa. Ndani ya dhana ya unafiki kuna tabia nyingi, mojawapo ni kunena tofauti na matendo na kutenda tofauti na kauli. Na ndiyo tabia tunayoifanya wakati wa maadhimisho ya siku ya mashujaa. Ndio maana nasema, tunafanya maadhimisho ya kinafiki.

Labda ni waambie wakina Kinjeketile, nini tulifanya huku kama ishara ya kuuadhimisha ushujaa wenu. Siku chache zilizopita 25 Julai, tulijumuika chini ya Amiri Jeshi Mkuu, kwa sasa ni Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yeye mwenyewe hakuwepo, alituma mwakilishi wake. Tulielezwa kwamba Rais yupo kwenye ziara ya kikazi Ujerumani!

Usiku mmoja kabla tuliwasha mwenge wa uhuru pale Mnazi mmoja. Halafu asubuhi yake gwaride lilijipanga kuwapokea wageni wa Kitaifa. Zikatolewa salam za Rais na wimbo wa Taifa ukapigwa kwa heshima yenu. Kikundi cha Buruji kikapiga “last post” na gwaride likaweka silaha begani. Askari sita waliojipanga vyema wakapindua silaha zao chini na baadae mizinga ikapigwa kwa ajili yenu huku watu wote wakiwa kimya. Gwaride likafanya “present arms” na kikundi cha buruji kikapiga “reveilles”. Gwaride likateremsha silaha na kufungua miguu.

Halafu silaha za asili ambazo nyingine nyinyi mashujaa mlizitumia zikawekwa kwenye mnara pamoja na maua. Baadhi ya silaha zilizowekwa ni pamoja na mkuki, ngao, sime, shoka, pinde na mishale. Hizi ni kumbukumbu sanifu za mapambano mliyoyafanya.

Hatimaye zikafuata sala na swala kutoka kwa viongozi wa dini wakiwakilishwa na sheikh, mchungaji, padri na maraji wa wahindu. Ingawaje sikumwona kiongozi wa dini ya jadi-ambao najua baadhi yenu nyinyi mashujaa na wahenga mliwaamini. Pengine dini za jadi zilitoweka na damu zenu. Gwaride likatoa tena heshima na wimbo wa taifa kupigwa ukafuatiwa na itifaki za viongozi wa kitaifa kuondoka. Wakabaki polisi kuzilinda silaha za kumbukumbu ya mashujaa mpaka jioni na hatimaye mwenge wa uhuru ukazimwa kama ishara ya mwisho wa maadhimisho ya kumbukumbu yenu ninyi mashujaa. Niwaulize wakina Kinjeketile, haya siyo maadhimisho ya kinafiki ya mashujaa?Pengine mtanijibu hapana!.

Ngoja niwaeleze masuala kadhaa halafu niwaulize tena. Siku hizi kuna kitu kinaitwa Bunge, hiki ni chombo cha juu chenye uwakilishi wa wananchi ambacho kunafanya maamuzi mbalimbali ambayo mengine huwa sheria. Chombo hiki ni kama yale mabaraza ya jadi yaliyokuwepo wakati wenu. Wiki iliyopita bunge lilijadili kuhusu maadhimisho ya vita vya Maji Maji ambavyo nyinyi wakina Kinjeketile mliviongoza. Miaka mia moja imepita toka damu yenu azizi ilipomwagika katika mapambano hayo ya kumwondoa mkoloni.Ungekuwepo najua ungekuwa Mbunge wa Kilwa, ungeshangaa sana-Eti maadhimisho ya vita mlivyovianza Kilwa na mapambano ya mwisho yakawa Songea, yanafanyika kinyume chake!Maadhimisho yameanzia Songea na waziri ameahidi pengine yataishia Kilwa. Chacha Wangwe, mbunge wa CHADEMA(wakati wenu hakukuwa na vyama vya siasa vyenye majina haya) jimbo la Tarime, yeye akahoji-kwanini bendera ya taifa isiwekwe rangi nyekundu kama ishara ya kuwakumbuka nyinyi mashujaa wetu? Naibu waziri wa habari na michezo, Mheshimiwa Emanuel Nchimbi-yeye akajibu, hakukuwa na sababu ya rangi nyekundu kuwekwa kwenye bendera ya Taifa kama ishara ya kuwakumbuka mashujaa. Eti, historia ya uhuru wa nchi yetu inaamuliwa kuanzia mkoloni wa mwisho aliyetutawala ambaye ni Muingereza. Sasa kwa kuwa tulipata uhuru wetu kwa amani bila kumwaga damu chini ya uongozi wa mwalimu Nyerere basi hakukuwa na sababu ya kuweka rangi nyekundu. Enyi mashujaa Kinjeketile na wenzako tunaowakumbuka leo mnakubaliana na jibu hili?

Ndio maana nikasema ni maadhimisho ya kinafiki. Tunanena tofauti na matendo. Nimesema awali, tunaanza maadhimisho ya leo kwa kuwasha mwenge wa uhuru halafu baadae tunaweka silaha za jadi. Kinjeketile na wenzako, iulizeni serikali- kama uhuru wetu tuliupata kwa amani, iulizeni serikali kwanini tunawasha mwenge wa uhuru na baadaye kuweka silaha za jadi? Tunanena tofauti na tunavyotenda? Iulizeni serikali, je harakati za mwisho za uhuru ni kipimo pekee cha historia ya nchi na hivyo kuwa kigezo pekee cha kuamua alama za nchi ikiwemo bendera?

Enyi mashujaa mlioambana kuulinda uhuru wetu dhidi ya wakoloni kuingia kuanzia wakati wa Mreno, Mwarabu na Mjerumani na kumwaga damu, mnakubaliana na majibu haya? Kushindwa kwenu na hatimaye ukoloni kuingia hakuondoi historia kuwa mlimwaga damu kwa ajili ya kulinda uhuru wa ardhi hii tukiyoirithi!

Enyi mashujaa mliopambana kuondoa ukoloni hususani ule wa Ujerumani mkamwaga damu, mnakubaliana na kumbukumbu hii?Kwamba mliyoyafanya si historia kuu kama historia ya uhuru toka kwa Mwingereza?

Enyi mashujaa, waulizeni wataalamu wa historia-baada ya Ujerumani kushindwa na makoloni yake yote kuwekwa chini ya halmashauri ya mataifa na baadaye baraza la udhamini, Tanganyika ikiwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza-si kwamba tulikuwa katika hatua za mwisho kabisa za kupewa uhuru ambao tayari tulishaupata kwa damu?Waulizeni pia, hakuna damu yoyote iliyomwagika wakati wa Mwingereza?Je, historia ya nchi yetu iliyojikita katika kipenzi chetu Nyerere imewajumuisha mashujaa wote wa ardhi hii?

Nasema kwa damu-kuanzia ushindi pamoja na kushindwa dhidi Mjerumani ambao ulileta mabadiliko katika mfumo wa utawala sanjari na mashujaa ambao walikuwa mstari wa mbele katika jeshi la Mwingereza na washirika wake katika vita dhidi ya Mjerumani, vile vita vya dunia ambavyo vilipiganwa pia katika ardhi yetu?Wakina nani walimwaga damu zaidi katika kile kinachoitwa ukombozi ulioletwa na majeshi ya mfalme Afrika(KAR) kama si nyinyi babu zetu?

Hojini serikali, hivi bendera hii ni ya Tanganyika au Tanzania? Jibu la Nchimbi limetolewa katika muktadha wa historia ya Tanganyika, Ingekuwa vipi jibu lingetolewa mintaarafu bendera ya Tanzania ambayo ilipatikana kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilihali visiwani kuna historia ya damu kumwagika ama kumwagwa wakati wa mapinduzi? Kama kweli tuna serikali ya mapinduzi Zanzibar na utawala wa Chama cha Mapinduzi(CCM), je ni mapinduzi yasiyo na ‘rangi nyekundu’?

Tunatenda tofauti na kauli! Tunafanya maadhimisho ya kinafiki. Wakina Kinjeketile tunawakumbuka kwa kuwa mlimwaga damu kupinga ukoloni na unyanyasaji. Mtuulize wajukuu zenu, je tunawaadhisha kwa kuendelea kupiga vita yale mliyoyakataa? Kwa hali ilivyo, wapo wanaotenda yale mliyoyakataa pamoja na kuwa wote kwa kauli tunawaenzi ninyi mashujaa. Tunapaswa sasa kuweka fikra zenu katika vitendo kwa ajili ya ukombozi wa taifa letu. Mwalimu Nyerere alikumbuka fikra zenu akatamka na kutenda kwamba uhuru, si uhuru wa maneno. Ni uhuru dhidi ya ujinga, uhuru dhidi ya maradhi, uhuru dhidi ya umaskini na baadaye akaongezea uhuru dhidi ya rushwa ama ufisadi. Enyi wahenga mashujaa, shukeni katika nyoyo za watoto na wajuu zenu, mtufanye kutokana na maadhimisho ya mwaka huu tuweke dhamira ya kupigana vita kwa zana kisasa kuleta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli, kuleta haki na maisha bora. Hii ndiyo hidaya kwa damu yenu azizi. Sio siri, kwa sera bila silaha, mapambano bado yanaendelea!

Mwandishi wa makala hii ni mwanaharakati na mwanasiasa kijana anayepatikana kupitia mnyika@yahoo.com na 0744 694 553


Friday, July 14, 2006

HOTUBA YA NDUGU JOHN J. MNYIKA-MKURUGENZI WA VIJANA WA CHADEMA KATIKA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA SIKUKUU YA WANAWAKE WA KIKRISTU WA KANISA LA MORAVIAN KANDA YA KUSINI, MABIBO-DAR ES SALAAM, 25 JUNI 2006



Wapendwa wanawake wa Moravian,

Wageni waalikwa-mabibi na mabwana.

Amani iwe kwenu!


Leo ni siku yenye furaha sana kwenu, ni maadhimisho ya sikukuu ya wanawake wa kikristu wa Moravian kanda ya kusini kama sehemu ya utamaduni mliojiwekea. Lakini ni siku ya furaha pia kwangu, kwanza kwa kuwa mahali pa furaha yenu, lakini pili na muhimu zaidi kwa hadhi mliyonipa ya kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa siku hii muhimu.

Mmeacha wote na kuamua mimi niliye mdogo katika Kristu niwe mgeni rasmi katika sikukuu, siku hii kubwa. Mmetimiza Maandiko! Palikuwa na wanawake wawili, mmoja akiitwa Elizabeti na mwingine Mariam. Mariamu alipokwenda kumtembelea Elizabeti aliposikia tu kuamkia kwake kitoto kichanga kilichokuwa tumboni mwake kikaruka. Baada ya kuelezwa maajabu haya Mariamu aliamua kumshukuru Mungu. Alimshukuru kwa mengi, lakini kubwa kuliko yote, alimshukuru Mungu kwa kuwakweza wanyonge na kuwashibisha mema wenye njaa. Nami nami nawashukuru kwa kunikweza maana mara nyingi maadhimisho kama haya hufunguliwa na viongozi wa juu, wafanyabiashara wakubwa na wazee wenye kutambulika . Lakini ninyi mmenialika kijana wenu, najua wengi mmenifahamu katika hekaheka za uchaguzi mkuu 2005 ambapo mimi niligombea Ubunge Jimbo hili la Ubungo. Mwaliko wenu umetimiza maandiko.

Maandiko matakatifu yanaeleza kuwa Nabii Samueli aliwahi kutumwa na Mungu kwenda nyumba ya Yese kumpaka mafuta mmoja wa watoto wake kuwa mfalme. Familia ya Yese ilikuwa na watoto mbalimbali wenye tambo na sifa kemu kemu. Walipitishwa wote, Samueli akasema HAKUNA. Alipouliza kama kuna mwingine wakamwambia “kapo katoto kengine kadogo sasa kanachunga kondoo”. Kalipoitwa kakaja, kakijana Daudi-mwenyezi Mungu akamwambia Samueli, “Huyu ndiye, mpake mafuta”. Nanyi leo ‘mmenipaka mafuta’, ndio maana narudia tena kuwashukuru kwa kutimiza maandiko.






Wapendwa wanawake wa Moravian, wageni waalikwa mabibi na mabwana:

Sasa niko mbele yenu hapa kijana wenu. Tuko katika maadhimisho. Na nisingependa niseme maneno mengi katika sikukuu. Raha ya sherehe ni kushereheka. Pengine wengine mnatarajia mimi kama mgeni rasmi nichochee hali hiyo. Ni wajibu mzito kuleta mambo yenye kusherehesha. Mnakumbuka kuhusu simulizi la harusi ya huko Kana mji wa Galilaya? Mamaye Yesu pamoja na wanawake wengine walikuwa harusini, Yesu naye alialikwa harusini pamoja na wanafunzi wake. Maria alipomfuata Yesu na kumweleza kwamba divai imewatindikia- Yesu akajibu kwa unyenyekevu-“Mama tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Lakini Mama akawaeleza watumishi wafanye kama walivyoelekezwa na hatimaye maji yakageuka kuwa divai. Mimi siyawezi haya, ni ya kimungu.

Pamoja na kuyashindwa haya, nawaomba nichukue fursa hii kabla ya kufungua rasmi niwape kidogo “divai”. Tofauti na ya Kana, mimi nawaomba niwape ‘kinywaji cha fikra’. Naomba niwaambie mambo mnayoyafahamu lakini pengine hamkupata wasaa wa kuyatafakari. Maadhimisho yetu ya leo yaambatane na tafakari.


Wapendwa wanawake wa Moravian, wageni waalikwa mabibi na mabwana:

Mosi, nawapongeza sana kwa utamaduni wenu huu wa kukutana kila mwaka na kuadhimisha sikukuu. Biblia inakumbusha kwamba walipo wawili au watatu kwa jina lake yeye yupo katikati, atakuwepo kwa kiasi gani katika kusanyiko hili kubwa? Kusanyiko kama hili ni kiungo cha kuunganisha nguvu za pamoja katika kukubiliana na changomoto za kiimani, kijamii na kadhalika. Maadhimisho haya yawe chachu ya wanawake wa Moravian kanda ya kusini kuwa pamoja katika mwaka mzima. Katika shida na raha, katika raha na karaha, katika huzuni na furaha. Ukiangalia historia za ujenzi wa nchi na maeneo mbalimbali, taasisi za kidini zina mchango wa pekee sana. Hii ni kwasababu zinaongozwa katika misingi ya utumishi, zina maadili yanayotaka kutumia raslimali bila ubadhirifu lakini pia zina mihimili ya kiimani inayotaka waumini na wote wenye mapenzi mema kuchangia raslimali. Wanawake wa Moravian, ni vyema kuitumia fursa hii. Kwa kuchochea mabadiliko ya kimaisha miongoni mwa wanawake, katika kata na kuendelea mbele zaidi. Maandiko yanatupa wajibu huu. Moja ya amri kubwa tunayopewa ni kumpenda jirani yetu. Ninyi nyote ni majirani katika Kristu. Tunaelezwa tunapaswa kuwavisha wenye njaa, kuwapa tumaini waliokata tamaa, kuwatetea wanaozulumiwa na mengine mengi ambayo ni sehemu ya agano jipya. Tukitekeleza haya hatutapungukiwa kitu-tutapata mahitaji yetu kama wanawake wa Moravian, tutachangia katika kuleta maendeleo katika taifa letu lakini kubwa zaidi tutakuwa tumejiwekea hazina isiyoharibika mbinguni.


Wapendwa wanawake wa Moravian, wageni waalikwa mabibi na mabwana:

Baadhi wanaweza kuwa na umaskini wa kipato, lakini hatupaswi kwa namna yoyote kujiruhusu ama kuruhusu tukawa na umaskini wa kimaadili. Maadili hayauzwi. Maadili ni bidhaa ya bure. Tunaweza tukawa na matabaka ya kiuchumi katika jamii yetu, lakini maadili ni chanzo cha heshima kwa wote. Maadili mema ni uwezo wa kutambua mema na mabaya na kuchagua yaliyo mazuri. Hatuhitaji fedha kuwa na maadili mema, hatuhitaji elimu ya chuo kikuu kuwa na maadili mema. Tunahitaji utashi. Maadili ni kinga dhidi ya matatizo mengi katika jamii. Maadili ni kinga dhidi ya kusambaa kwa UKIMWI, ngao dhidi ya rushwa na ubadhirifu, kinga dhidi ya matatizo ya kifamilia yanayopelea nyumba ndogo na kuvunjika kwa ndoa, ni ngao dhidi ya madawa ya kulevya na mapungufu mengi katika jamii. Kwa lugha ya mtaani tunaweza kusema maadili ni ‘dili’. Nyinyi mnayo nafasi ya pekee kwa kuwa mmejiunga pamoja chini ya mwamvuli wa wanawake wa Moravian-taasisi ya kidini. Dini zinahimiza upendo na kujitawala. Dini zinahimiza maadili. Tuyaweke mafunzo haya katika vitendo lakini twende mbele zaidi kwa kuhimiza maadili katika jamii kwa ujumla. Hiki ni ‘kinywaji cha pili cha fikra’.

Wapendwa wanawake wa Moravian, wageni waalikwa mabibi na mabwana:

Suala la tatu ambalo ningependa tulitafakari ni “ukombozi wa kifikra”. Mtu anaweza kuwa fukara lakini hatupaswi kukosa fikra. Ukombozi wa fikra unajumuisha kufikiri na kutenda. Ni kuthubutu kufikiri na kufikiri kuthubutu. Kwa nini nazungumza hizi falsafa leo? Sipendi kuwatoa katika maadhimisho na kuwatumbukiza katika maudhi. Lakini leo ni sikukuu yenu wanawake wa Moravian , imani yangu ni kwamba nyinyi wakina mama ndio ‘wazazi wa fikra’. Mathalani, tabia yangu na silika yangu binafsi ikiwemo kujiamini na kuthubutu ni matokeo ya malezi ambayo kwa kiasi kikubwa yametokana na mama yangu. Tujiulize vichwani mwetu, ni wangapi tumewakomboa kifikra, kwa namna gani? Kama bado tuanze sasa. Wajibu huu hauhitaji elimu darasani. Unahitaji elimu ya nyumbani. Ukichambua kwa kina mataifa yaliyoendelea ama watu binafsi walioendelea utakuta kuna tabia fulani fulani zinazofanana: kupenda kazi/kujituma, kuthubutu, kuwa na malengo/dira na kuyasimamia, kufahamu haki na kutimiza wajibu, kuheshimu muda/wakati na hulka nyingine za kijasiriamali. Tabia hizi wameziweka kuwa sehemu ya utamaduni wao wa kila siku. Lakini chanzo cha kuwa na yote haya ni ukombozi wa fikra. Kitalu cha ukombozi huu ni elimu ya nyumbani ambayo mwalimu wake mkuu ni “mwanamke”. Kwa hiyo nyinyi ndio wenye funguo wa ama jamii ibaki ilipo au ibadilike. Kama Margaret Mead alivyowahi kusema, tusihofu kuwa kikundi cha watu wachache chenye dhamira kinaweza kuleta mabadiliko, ukweli ndio kitu cha pekee kilichowahi kuleta mabadiliko. Hii ni changamoto yangu kwa wanawake wa Moravian kanda ya kusini. Hatupaswi kushindwa kugharamia ukombozi wa kifikra kwa sababu gharama yake ni bure.


Wapendwa wanawake wa Moravian, wageni waalikwa mabibi na mabwana:

Pamoja na kuweka mkazo katika elimu ya nyumbani kama nilivyodokeza hatupaswi kuweka pembeni elimu ya darasani. Elimu ya darasani ni mkunga wa taarifa na maarifa. Wote tunafahamu matokeo ya elimu nzuri ya darasani kwa maisha ya binadamu. Kwa hiyo hatupaswi kabisa kuwaza ‘kumchinja huyu kuku anayetuzalia mayai ya almasi’. Lakini kwa wanawake wengi kikwazo kikubwa ni gharama za elimu. Nakiri kuwa ni sehemu ya kikwazo lakini niweke bayana kuwa ziko fursa za kielimu ama za kupunguza gharama za kielimu ambazo hazitumiki na mara nyingi ni kutokana na kukosekana ama uthubutu ama taarifa. Linapokuja suala la elimu kurudi nyuma ni dhambi. Bisha hodi mpaka ufunguliwe! Kwa pamoja tuitazame elimu kama urithi wa lazima kwa watoto. Mfano wa mwanamke mjane akidai haki bila kuchoka uliomo katika biblia Injili ya luka(18:2-7) uwe kichocheo kwa wanawake wote kuwa mstari wa mbele kudai haki ya elimu.

Wapendwa wanawake wa Moravian, wageni waalikwa mabibi na mabwana:

Mwisho, matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno. Nimesema mengi. Ili haya yaweze kutekelezwa na wanawake wa Moravian nguvu za pamoja zinahitajika ikiwemo na raslimali. Na tuanze sasa, maadhimisho yetu yaende sambamba na harambee. Kama watu wanachangia harusi, kama watu wanachangia ‘kitchen party’, kwa nini tushindwe kuchangia kazi ya Mungu kupitia umoja wa wanawake wa Moravian? Kwa nini tushindwe kuchangia maendeleo kupitia asasi hii ya dini? Inawezekana, na tuanze sasa. Tunaweza kudhani hatuwezi. Tukumbuke sadaka wa mwanamke mjane, alitoa kidogo kilichochake ndani ya hazina yake lakini matokeo ya tendo lake yalikuwa makubwa. Tuanze sasa. Mimi nianze kutoa “sadaka ya mwanamke mjane”, natoa shilingi laki moja taslimu. Huu ni mwanzo, tuanze sasa. Viongozi wachukue nafasi, waongoze watu wengine hapa kuchangia na kutoa ahadi kwa namna mbalimbali. Tuanze sasa, huu ni mnyororo. Haupaswi kuishia hapa. Nilisema wapo waumini wengine ambao hawakufika na watu wengine wenye mapenzi mema ambao sio sehemu ya umoja huu. Huu ni mwanzo, muwatambue na kuwafuata. Mnyororo huu wa michango ya hali na mali uendelezwe mpaka malengo ya wanawake wa Moravian yapate raslimali za kuyatekeleza. Kama ambavyo bahari ni muunganiko wa matone madogo ya maji, raslimali zinazohitajika ni mkusanyiko wa michango kidogo kidogo kutoka vyanzo mbalimbali. Waswahili husema, haba na haba hujaza kibaba. Biblia inaeleza ukombozi ulizaliwa kupitia kwa mwanamke, wanawake walikuwa pamoja Yesu katika hatua zote za mateso na wanawake ndio wa kwanza kupokea habari za ukombozi. Maadhimisho ya sikukuu ya wanawake hapa Moravian kanda ya kusini hapa mabibo yalete mwamko huu katika kutimiza wajibu kama huu katika jamii yetu ya leo. Naamini sijawalevya kwa ‘divai hii ya maneno’, natumaini nimewapa ‘kinywaji ya fikra’ na sasa maadhimisho haya yamefunguliwa rasmi.


Mungu awabariki kwa kunisikiliza.