HOTUBA YA UFUNGUZI WA MKUTANO WA VIJANA WA SEKTA MBALIMBALI KUKUSANYA MAONI YA RASIMU YA MWONGOZO WA BARAZA LA VIJANA WA CHADEMA ILIYOTOLEWA NA MKURUGENZI WA VIJANA-JOHN MNYIKA KATIKA UWANJA WA MAKAO MAKUU YA CHAMA KINONDONI-DAR ES SALAAM
JUMAPILI 23 APRILI,2006
Waheshimiwa vijana wenzangu wa sekta mbalimbali,
Waheshimiwa wanachadema wenzangu,
Waheshimiwa wanahabari,
Waheshimiwa wageni waalikwa,mabibi na mabwana
Heshima yenu wote!
Wengine mtajiuliza ni vipi nimekuwa mtovu wa itifaki katika kulitumia neno “waheshimiwa”. Mimi imani yangu ni kama ile iliyo katika katiba ya nchi yetu kwamba kila mtu anastahili heshima. Sasa kwa kiswahili rahisi yoyote yule anayestahili heshima basi ni mheshimiwa. Sisi wote ni waheshimiwa.
Naomba nianze kwa kuwakaribisha na kuwashukuru kwa kuitikia kwenu mwetu wetu. Ninazo sababu mbili kubwa za kuwashukuru:
Mosi kwa uamuzi wenu kwa kuacha mapumziko na kuja kufanya kazi ya kujitolea. Kwa wengi jumapili ni siku ya mapumziko wakati mwingine huonekana hata kufanya kazi siku hii ni dhambi. Lakini Nabii Isa amefafanua vizuri-yu wapi ambaye mfugo wake ukiingia shimboni siku ya mapumziko ataacha kuutoa eti kwa kuwa anapaswa kupumzika?Kadhalika vijana wa CHADEMA leo tumewaiteni, nawashukuru kwa kuja kutusadia hii kazi iliyo mbele yetu.
Pili kwa kuitika mwito wa toka kwa vijana wa CHADEMA-chama cha upinzani. Katika jamii ya Tanzania ambapo mfumo huu wa vyama vingi bado ni mgeni na pengine kuna nguvu za utawala zinazouminya ni wazi kuwa upinzani kunaonekana kuwa jambo gumu na la hatari. Wakati mwingine watu wanaweza kukunyanyapaa kwa kuwa tu uko upinzani. Lakini nyinyi mmekubali mwito wetu kuja kutusikiliza na kutoa maoni yenu. Niwapongeze kwa kukomaa kisiasa. Siasa si uadui. Na nafurahi sasa kuna viongozi wa serekali wamenza kulitambua hili, kwamba kila mtu ana haki na uhuru wa kuwa katika chama anachokitaka na wananchi wana haki ya kuchagua chama wanachokitaka ama mwakilishi wampendae. Raisi Kikwete alisisitiza kauli hii hivi karibuni, mwito huu unapaswa kuitikiwa na wote wanaopenda demokrasia na maendeleo.
Ndugu washiriki:
Wajibu wangu hivi sasa ni mdogo tu, kufungua rasmi mkutano huu kama mwenyeji wenu. Huu ni wajibu wa sekunde chache. Lakini kabla sijautekeleza naomba kwa ruhusa yenu mniruhusu niseme maneno mawili matatu kwani fursa si mara kwa mara zinapatikana fursa kama hii ya kukutana na wadau mbalimbali wa vijana.
Leo tumewaalika ninyi vijana wa sekta mbalimbali baadhi yenu ni wanachadema na wengi wenu si wanachadema mje mtupe maoni yenu kuhusu rasimu ya mwongozo wa Baraza la Vijana wa CHADEMA. Hapa mpo vijana wenye ulemavu,mpo vijana wafanya biashara ndogo ndogo, mpo vijana wa vyuo vikuu, mpo vijana wa sekondari, mpo vijana wa Asasi Zisizo za Kiserekali, mpo vijana wa Jumuia za kidini, mpo vijana wa utamaduni nakadhalika.
Labda wengine mtajiuliza ni kwanini moja kwa moja tumeamua kuanza na vijana wa sekta mbalimbali. Kwa nini hatukuamua kujifungia na vijana wa CHADEMA kuandaa mwongozo na kuupitisha. CHADEMA tunaamini katika itikadi ya nguvu ya umma kwamba umma wa watanzania ndio unahaki ya kuamua kuhusu hatma ya nchi yao ikiwemo kufurahia matunda yake. Kadhalika, umma wa vijana una haki ya kuamua hatma ya baraza la vijana wa CHADEMA tuliloamua kuliunda. Chama cha siasa ni mali ya umma. Vyama vya upinzani ni mali ya umma. Vyama cha upinzani ni serekali inayosubiri kwa kiingereza wanasema “a government in waiting”. Hivyo kwa kuwa iko siku chama kitaingia madarakani na hivyo kutoa mwelekeo wa watanzania wote ni lazima tangu mwanzo kiruhusu ushiriki mpana. Tunawashukuru kwamba mmekubali kuja kuchangia maoni yenu kama sehemu ya kutekeleza lengo hili.
Ndugu washiriki:
Nyinyi ni wataalam na wazoefu wa masuala ya vijana katika sekta zenu. Wito wangu kwenu ni kutusaidia kwa kutoa maoni yenu ili kuboresha uundwaji wa baraza la vijana wa CHADEMA. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa malengo, muundo na masuala mengine kuhusu baraza la vijana wa CHADEMA vinazingatia matakwa ya vijana wa sekta mbalimbali na vigezo vya ushiriki wa vijana wenye kuleta ufanisi.
Lakini kwa kuwaita ninyi kutoa maoni haimaanishi kwamba tumewanyang’anya wajibu wao wa kikatiba vijana wa CHADEMA hususani vijijini. Baada ya mkutano huu tutasambaza rasimu hii katika wilaya zote nchini na kuwahimiza viongozi wetu katika ngazi hizo kukusanya maoni ya ngazi za chini zaidi na hatimaye kuyawasilisha makao makuu ya chama.
Kwa upande mwingine kwa kuwa sisi vijana ni “kizazi za TEKNOHAMA”, tutaitumia fursa hii vizuri. Tunawataarifu vijana wote na wadau wengine kwamba mnaweza kutembele tovuti ya chama www.chadema.net na kuchangia maoni au kuyatuma moja kwa moja kwa anuani pepe vijana@chadema.net.
Mwishowe kabla ya mkutano mkuu wa chama unaotarajiwa kufanyika mwezi wa nane tutaitisha mkutano wa kitaifa wa vijana wa CHADEMA ambao utapitisha rasimu iliyochanganya maoni yatakayokusanywa kabla ya kuthibitishwa na vikao vya juu vya chama.
Ndugu washiriki:
Labda pia nidokeze mambo machache ambayo ni vyema mkayatafakari wakati mnatakapotoa maoni yenu. Uamuzi wa kuunda Baraza la Vijana wa CHADEMA(BAVICHA) ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya vijana ya CHADEMA. Ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za chama za kutoa fursa kwa vijana kama chama mbadala kinachotambua mchango wa kizazi kipya katika kuchochea demokrasia na maendeleo. Uamuzi huu unalenga pia kutekeleza sera za kimataifa kuhusu vijana mathalani Mkakati wa vijana wa Dakar na Mpango wa vijana wa dunia kuanzia mwaka 2000 na kuendelea. Kwa upande mwingine msukumo ziada wa kuunda baraza la vijana kutokana na uzoefu wetu hususani katika uchaguzi mkuu 2005 kama vijana wa CHADEMA wa haja ya kuwa na chombo kipana zaidi cha kutuunganisha pamoja. Lakini pamoja na nia njema ya uhuru na kujitegemea mhakikishe kuwa maoni hayatupeleki kuwa na “chama ndani ya chama”.
Pamoja na malengo na majukumu ya kisiasa ambayo naamini hamtayasahau kwa kuwa hili ni baraza la chama cha siasa ni vyema maoni yenu yakawezesha baraza la vijana litakaloundwa kuwa na wajibu wa kutetea maendeleo ya vijana ikiwemo kuwasadia vijana wenye matatizo, kuunga mkono harakati makini za vijana na kushirikiana na vijana wa sekta mbalimbali. Wajibu huu ni muhimu sana hususani katika wakati wa sasa ambapo jumuia nyingi za vijana zipo kimya kutetea maslahi ya vijana na kuwahamasisha kutimiza wajibu wao. Pia baraza liweze kuwahamasisha vijana wa CHADEMA kushiriki shughuli za kisiasa na kijamii ikiwemo kuhamasisha vijana kujiunga katika vikundi vya michezo/kiuchumi na kudhibiti madawa la kulevya na UKIMWIVVU.
Ndugu washiriki:
Ni imani yangu uamuzi wa kuunda baraza la vijana wa CHADEMA utatoa changamoto kwa serekali kuharakisha mchakato wa uundwaji wa Baraza la Vijana la Taifa.(BAVITA). Mtakumbuka kuwa toka mwaka 1998 vijana wa sekta mbalimbali tumekuwa tukitaka kuundwe baraza huru la vijana la Taifa. Leo miaka nane imepita baraza limeendelea kuwa ahadi. Sisi vijana wa CHADEMA tunaunga mkono uanzishwaji wa baraza la vijana la Taifa ambalo litaunganisha vijana wote wa Tanzania bila kujali itikadi. Umoja ambao uliwekewa ufa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi na hivyo umoja wa vijana wa chama tawala kupoteza uhalali wa kuwa kiungo na kiwakikilishi cha vijana wote. Lakini katika mchakato huu lazima ukamilishwe kwa kuzingatia matakwa ya vijana. Kuna mambo kadhaa yanayopaswa kujadiliwa kuhusu mchakato huu lakini leo si mahali pake. Ila kwa vyovyote vile baraza la lazima liwe na uanachama mpana na wa aina mbalimbali utakaowakilisha maslahi ya vijana wa sekta mbalimbali. Kwa upande mwingine pamoja na kupata ruzuku serekalini kama ilivyo katika nchi nyingine ni vyema baraza likawa na uwezo wa kupata raslimali toka kwa wanachama wake na wadau wengine ili kuliepusha kupoteza uhuru wake kutokana na utegemezi. Kwa upande mwingine viongozi ni vyema wakatokana na vijana wenyewe kupitia mchakato wa kidemokrasia na watendaji wapatikane kupitia mfumo wa wazi wenye ushindani.
Ndugu washiriki:
Ninyi ni vijana toka sekta mbalimbali. Nadhani ni vyema nikawaeleza haya leo ili mtusadie katika kuleta mabadiliko ya kweli. Nakumbuka nilitembelea Accra-Ghana niliona sanamu ya Hayati Nkurumah chini yake palikuwa na nukuu yake, “Utafuteni ufalme wa siasa na yote mtaongezewa”. Siku elewa kwa kina ujumbe nyuma ya maneno hayo kwa wakati huo. Lakini nilipotafakari baada ya miaka kadhaa nilipata mang’amuzi mbalimbali ambayo leo nisingependa kuchukua muda kuyaelezea. Pengine niwape mifano kutoka katika uchaguzi mkuu 2005 labda nitaeleweka zaidi. Kabla ya uchaguzi huo vijana walikuwa wakiitwa taifa la kesho-lakini vijana walipoelekea kuutafuta ufalme wa siasa ama kwa kugombea au kwa kuunga mkono wagombea hali ilibadilika. Vijana wakaonekana watu wa muhimu kweli, wakaanza kuongezewa yote. Ghafla ajenda za ujana na ujana vikatawala katika uchaguzi, kizazi kipya kikaonekana ni funguo za kuelekea utawala. Kila mtu akapenda kuwa kijana. Ahadi zikatolewa kwa vijana kubwa zaidi ikawa ile ya ajira. Sasa uchaguzi umekisha, vijana waanze kuzitumia fursa zinazojitokeza na kutengeneza fursa za kujiendeleza kijamii na kiuchumi. Lakini narudia tena maneno ya Nkuruma, endeleeni kuutafuta ufalme wa siasa na yote mtaongezewa hii ni pamoja na kufuatilia ahadi zilizotolewa. Wapo vijana waliopata nafasi za kuwakilisha katika bunge, halmashauri na asasi nyinginezo-nyinyi mmeongezewa. Ni zamu yenu sasa kuwaongezea vijana wengine. Lakini idadi yao ni ndogo. Nambari yao inadhihirisha kwamba pamoja na hamasa kuhusu vijana na ujana zilizokuwepo katika uchaguzi uliopita vijana bado wanalitumika kama wapiga debe tu. Hivyo ninyi mnao wajibu wa kuibadili hali hii. Niwape mfano hai, katika bunge letu lenye wabunge 324 wabunge walio chini ya miaka 30 wako watano tu. Hii ni sawa na asilimia moja na nukta kadhaa tu. Haya ni matusi kwa demokrasia. Demokrasia ni utawala watu kwa ajili ya watu, iweje watanzania wenye umri chini ya miaka 30 ambao ni asilimia takribani 60 ya watanzania wote wakawakilishwa kwenye chombo kikuu cha maamuzi ya nchi kwa asilimia moja? Vijana bado tunasafari ndefu, nawaombeni vijana wa sekta mbalimbali twendeni sote tuimalize hiyo safari. Tunahitaji matanuru ya kuoka kuoka viongozi vijana-Baraza la vijana wa CHADEMA litakuwa ni tanuru mojawapo.
Hii itakayowasilishwa hapa ni rasimu sifuri ama kwa kimombo Zero draft, hivyo mko huru kuichambua na hata ‘kuichanachana’ kama ikibidi. Natangaza kuwa mkutano huu wa kukusanya maoni ya vijana wa sekta mbalimbali kuhusu rasimu ya baraza la vijana wa CHADEMA umefunguliwa rasmi na mchakato wa kupokea maoni ya vijana na wadau mbalimbali kuhusu BAVICHA umezinduliwa rasmi.
Mbarikiwe kwa kunisikiliza
