Majibu kuhusu Utamaduni wa Amani
Prosper,
Nakubaliana na maoni yako, ndugu zetu wa Kenya hususani na Kibaki na Raila wanapaswa kuweka utaifa wao mbele na kutafuta suluhu ya mgogoro unaoendelea kufukuta huko. Na ni funzo kwetu wa Tanzania kwamba tufanye mabadiliko sasa kuhakikisha mifumo yetu ya uchaguzi na kisiasa inakuwa huru na inasimama mstari wa mbele katika kulinda haki na amani.
Huu ujumbe ameandika kaka Mwakatobe mwenyewe kwa mkono wake? Sitaki kuamini!Kila uhuru ana haki ya mawazo na fikra, lakini binadamu anapotoa mawazo tofauti na imani yake ambayo imezoeleka na wengi kuna haja ya kujiuliza maswali mengi sana. Nitaendelea kujiuliza. Ukipata wasaa wa kuonana naye naomba umwulize ana kwa ana kama ujumbe huu ameuandika yeye.
Sidhani kama mwakatobe ambaye tulikuwa naye NYF miaka mingi nyuma kabla ya kuingia kwenye siasa- wakati huo tukiwa kwenye harakati tu za kawaida za kuhamasisha mabadiliko ya kiraia nchini, sidhani kama alikuwa na mawazo kama haya. Na kwa kweli binafsi nimepata nafasi ya kubadilishana naye mawazo kirafiki kabisa maeneo mbalimbali hapa dsm na hata nje ya mkoa- kuanzia nyumbani kwake mpaka kwenye vikao vya ndani. Ukimweleza hivi najua atakumbuka mengi sana! Kama ujumbe umeandikwa mwenyewe- basi binadamu ni kiumbe cha pekee sana! Nitajaribu kuingia katika kumbukumbu zangu kuona kama nipata maandiko yake ya wakati huo, ikiwemo ile itikadi/falsafa aliyokuwa akiitetea. Je, ni wakati huo ndio alikuwa akiandika alichokuwa akiamini au ni sasa ndicho anachokiamini, Je, ataendelea kuamini hivyo? Nini asili ya uongofu huu? Kwa kweli, nikianza kuandika kwa undani kumbukumbu hizo za zamani, tukio hata tukio, hatua hata hatua- kwa kweli nitajikuta naandika mambo mengine binafsi kabisa! Sitafanya hivyo. Na wala si nia yangu kuandika makala ya gazetini, sitafanya hivyo pia. Kwa kuwa siamini kama makala haya uliyonitumia ni fikra huru za kaka Gwandumi Mwakatobe!
Nakubaliana na maandiko haya kwamba AMANI ni tunu ya muhimu sana, na inafaa kulindwa kwa gharama zozote. Nakubaliana pia kwamba Tanzania ina UTAMADUNI WA AMANI. Ila mwandishi alipaswa kujiuliza- Utamaduni nini? Je, utamaduni huweza kuzaliwa na kufa? Nini asili ya utamaduni wa amani katika Tanzania? Na yapi yanaweza kufanya utamaduni huo kutoweka?
Msimamo wa Kaka Gwandumi huko nyuma umekuwa ni kuwa Tanzania pamoja na kuwa tuna amani lakini kuna watanzania wengi hawana amani- na hali hii ya kukosa kwao amani inachangiwa pia na kukosa kwao haki, na wengine ni kutokana na hali mbaya ya maisha iliyozidi mipaka. Katika mazingira hayo msimamo wake wakati wote umekuwa kama ule wa Mwalimu Nyerere ambao pia ni msimamo ulioko kwenye Biblia ambayo Kaka Gwandumi amekuwa akiitumia kwa muda mrefu kwenye maandiko yake. Kwamba AMANI ni TUNDA la HAKI. Ndio maana sitaki kuamini kama msimamo huu mpya ni wa Kaka Gwandumi.
Nakubaliana na mwandishi katika utangulizi kwake kwamba njia za amani ndizo ambazo ni za kwanza kabisa, na za kistaarabu katika kufikia malengo ya kisiasa. Ila sikubaliani naye kwamba njia zingine ni njia ambazo madhara yake hayawezi kufutika milele. Naandika ujumbe huu leo Januari 12 ambapo Wazanzibar wameadhimisha mapinduzi ya umma yaliyomwaga damu kumng’oa sultani; Je, anataka kusema kwamba mapinduzi yale- yeye kama mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi, anayatangaza kuwa ni haramu na njia mbaya zaidi iliyowahi kutumika katika historia ya Taifa letu ambayo itasababisha visiwa vile visiwe na Amani milele? Afrika Kusini ilitumia muda mwingi mijadala na kujenga hoja huku makuburu wakitumia risasi za moto, ANC baadaye ikaazisha Umkotwo we Sizwe, jeshi lake hili ambalo lilifanya uharamia kwa serikali ya makuburu ikilenga miundo mbinu yao- ni harakati hizi ziliwarudisha makaburu kwenye meza ya majadiliano. Sisemi hivi kuhalalisha mapinduzi ya kijeshi; njia ambayo katika siasa za sasa za ustaraabu ni njia ya mbali kabisa. Nasema hivi kufuta hoja ya mwandishi, na mifano kwa kweli iko mingi sana duniani. Hawa wastaarabu wa demokrasia wa magharibi tunaowazungumzia leo, karibu kila taifa lao limepitia katika ushenzi usiomithilika kufikia katika ustawi walio nao sasa! Sisemi hivi kuhalalisha kwamba sasa tuwe washenzi, nasema hivi ili mwandishi wa makala haya ajaribu kutafakari kidogo- “Hivi kwa nini binadamu wanafikia hatua ya kuwa washenzi?”.
Mwandishi amejaribu kujenga hoja kwamba AMANI ndiyo kipeo cha yote. Na amani hiyo ndiyo ameiita URITHI MKUU WA UTAMADUNI WETU WA KISIASA. Kama nilivyosema, utamaduni huzaliwa, hukua na huweza hata kufa? Mwandishi ajiulize, ni mambo gani yanatishia kuua huu utamaduni? Niliwahi kuandika hapa baadhi ya mambo ambayo yanaweza kutishia kufa kwa utamaduni wetu wa amani, mambo ambayo baadhi hata Nyerere mwenyewe alishawahi kuyatabiri- bonyeza hapa kusoma andiko langu hilo:Jambo moja utabaini; http://www.chadema.net/makala/mnyika/mnyika_15.html HAKI( kwa maana ya JUSTICE ambayo ni zaidi ya RIGHT); ni roho ya AMANI. Bila haki amani iko shakani. Haki ikitoweka, amani haiwezi kuishi hata kwa kuandika makala elfu na maelfu za propaganda kuhusu umuhimu wa amani katika nchi yetu. Namna ya kuendeleza uhai wa amani hiyo ni kuchambua, kukemea na kuondoa mizizi inayotishia haki za wengi. Mwandishi amesema AMANI ni urithi mkuu; lakini mwandishi anajua kuwa urithi ni jambo jema lakini si kila mrithi anauwezo wa kutunza urithi kama mwenye mali mwenye ambaye aliichuma kwa tabu hatua kwa hatua. Kauli ya kwamba huu ni urithi pekee haiwezi kulinda urithi huo.
Ukiona viongozi wa serikali wanazomewa hadharani. Ukioana wananchi wanaanza kujichukulia sheria mikononi wenyewe. Huku viongozi na makada wakiendelea kuiamba AMANI,AMANI, AMANI! Wananchi wakiendelea kuimba HAKI, HAKI, HAKI!. Hizo ni alama za nyakati. Ni wakati wa viongozi na wananchi kukaa na kutafakari na kuzungumza lugha moja. Si wakati wa viongozi na kikundi cha watu wachache kuwahubiria kile wasioamini. Tembelea maeneo ya migodi, pata hisia za wananchi. Jaribu kaa vijiweni, sikiliza wananchi wanazungumza nini kuhusu ufisadi na watawala wao. Mambo haya yatahitaji mchambuzi kama huyu, aliyeandika kurasa zote hizi kuyafanyia kazi kwa manufaa ya taifa letu. Na ni kwa kuchukua hatua ndipo tutakuwa kweli walinzi wa AMANI. Ni kwa kuamka, na kukemea aina zote za UBAGUZI, zinazoanza kujitokeza katika nchi yetu, ndipo tutadumisha Taifa lenye AMANI.
Umemkweza lakini wakati huo huo umemtweza Kinjeketile; niliwahi kuandika, tunu ya yangu kwa shujaa huyu: http://www.chadema.net/makala/mnyika/mnyika_13.html mwandishi wa uchambuzi huu kama naamini anajua historia ya nchi yetu pamoja na upotofu wote wa kihistoria uliofanyika. Anajua kwamba Kinjekitile ni mtu ambaye anapaswa kujengewa Minara kama ambavyo wakina Nyerere wanabigiwa baragumu! Wajerumani wametumia muda mrefu katika nchi yao mwaka jana kukumbuka vita vya Maji Maji, wanajua ni mapambano ya namna gani yalifanyika. Na mara baada ya Vita hivi utawala wa Kijerumani haukuwa tena katika hali ya awali hapa nchini. Falsafa ya maji, ilikuwa ni falsafa ya mapambano tu; lakini mbele yake waliokuwepo machifu na viongozi wengine wa kiafrika na wapambanaji wao waliokamata silaha. Mataifa ya wenzetu, chimbuko la uzalendo wao- ni harakati za watu kama hao. Lakini sisi tunawabeza! Uzalendo utatoka wapi? Uzalendo huchachushwa kwa moyo za hisia za kutazama mambo makubwa yaliyofanyika katika Taifa!
Mwandishi anajua kwamba Wajerumani ndio walikokuwa wakoloni halisi, huku waingereza ambao Mwalimu aliwakimbiza kwa Harakati za Ndani na Zile hotuba za umoja wa Mataifa kwa kuwa walikuwa na wadhamini tu. Najua mwandishi anayajua haya yote! Mwandishi anajua kwamba kama waingereza wangekuwa walowezi Tanganyika kama ilivyokuwa kwa Kenya ni wazi baada ya Maji Maji ingezaliwa Mau Mau nyingine hapa kwetu. Mwandishi anajua haya! Anajua kwanini tulipeleka vikosi vyetu vijana wetu wakapoteza damu kuleta ukombozi kusini mwa Afrika- Msumbiji, Angola, Afrika Kusini nk! Anajua haya. Hata Nyerere aliyajua haya, ndio maana hakupeleka njia za Amani na Maelewano huko(Non Violence Method); Nyerere aliyekuwa kiongozi aliyejua falsafa ya mapambano. Alijua adui anayetumia mbinu gani akabiliwe kwa mbinu gani!. Ndio maana hakutaka kukaa meza moja ya majadiliano na maelewano na Iddi Amini Dada! Unadhani Nyerere hakuwa anajua “urithi mkuu na utamaduni wetu wa kisiasa” za AMANI?
Mwandishi ametumia muda mrefu kujenga hoja kwamba WAPINZANI wanachochea vurugu, uhasama, ugomvi, matusi, kejeli nk na kwamba ndio wanaoelekea kuvunja AMANI nchini. Lakini mwandishi ameshindwa kutaja mifano ya kauli au matukio hayo na yalihusu wapinzani gani! Ujumbe huu, ukisomwa juu juu, waweza kuaminika na kuviza imani ya watanzania kwa watanzania wenzao walioko kwenye upinzani. Lakini tukumbuke, Mandela alipopinga ubaguzi aliitwa mpinzani mwenye kuvunja amani. Nyerere aliitwa na serikali ya mkoloni, mpinzani mwenye kuvunja amani na akashtakiwa kwa uchochezi. Mchambuzi mahiri kama huyu, angetumia muda kuvitaka vyombo vya dola kuchukua hatua kwa wapinzani hao kama kweli wanavunja amani ya nchi!. Mwandishi akumbuke kwamba, kwa mpinzani Dr Slaa alipojitokeza hadharani kusema ufisadi wa Benki Kuu(BOT) aliitwa majina yote ambayo mwandishi huyu ametumia kueleza tabia ya upinzani. Leo hii baada ya Rais Kikwete kuona ukweli wa mambo tena katika sehemu ndogo tu ya ukaguzi wa EPA; wale wote waliosema maneno hayo sijui kama wanajisikia AMANI mioyoni mwao! Ndio maana sitaki kuamini kama ameandika Kaka Mwakatobe ujumbe huu, kwa kuwa najua yeye anajua , na huwa anapenda sana kutumia biblia- na ndani ya kitabu hicho kuna simulizi ya Yesu ambaye naye aliitwa majina kama hayo na watawala wa wakati huo. Lakini leo wakristu wote kote duniani wanamuita jina tofauti kabisa!
Siasa za kistaraabu za kujenga hoja naziunga mkono! Siasa safi, za sera na hoja. Na ndio ambazo upinzani umekuwa ukifanya. Dr Slaa alianzia bungeni, akajaribu kutoa hoja ya awali ikapuuzwa. Akaongeza ukali zaidi wa maneno, hakueleweka. Akaongeza uzito zaidi kwa kuandaa hoja binafsi, akaletewa mizegwe. Na hapo ndipo alipotumia lugha kali zaidi, kwamba ‘hawa ni wezi na mafisadi’. Leo mpaka Kikwete naye ameanza kutumia lugha kali! Lugha ambayo miezi michache nyuma, mawaziri waliikebehi kama ambayo makala hii inakebehi upinzani!. Wote kati yetu, mtu akichukua mali- tutazungumza kwa ‘urithi wa utadamuni wetu wa kisiasa’, “Naomba nirudishie”; asiporudisha lugha gani hufuata?
Mwandishi ameendelea mbele kuonyesha nia ya maandiko yake pale alianza kujenga hoja kwamba Nyerere alisema ‘kiongozi bora lazima atoke CCM”; mwandishi anasahau ni Mwalimu huyu huyu alisema “CCM sio Mama yangu”. Mwandishi akasome maandiko ya mwisho mwisho ya Mwalimu Nyerere kwenye “Uongozi wetu na hatma ya Tanzania”; hakika hii kansa ya uongozi Nyerere alishaitabiri, na unaweza kubashiri kama angekuweo sasa na ufisadi angefanyaje! Kama kweli Nyerere aliamini kwamba “Kiongozi bora lazima atoke CCM”; Mwandishi anaweza kutuelezaje yaliyotokea kule Musoma baada ya mfumo wa vyama Vingi kuanza ambapo Baba wa taifa alimnadi wazi mgombea wa Upinzani Balozi Ndobho kwa ubora wake na kumuacha wa chama chake CCM? Watanzania tunapaswa kuwa na siasa zilizo juu ya vyama, zinazotazama zaidi maslahi ya Taifa.
Mwandishi anajenga hoja kwamba dosari kuu ya upinzani ni kutaka wananchi wakichukie Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake! Mwandishi anajua kabisa kwamba wema ni sumu ya uovu. Kama CCM na serikali yake wanatenda mema, unadhani wananchi wanaweza kuchukia hata wapinzani wangesambaza chuki? Lakini kwa kuwa kuna UOVU unajaribu kufichwa ni wazi kwamba yoyote anayesema UKWELI, ataonekana ni mchonganishi na mchochea chuki. Wakina Dr Slaa, Zitto wote wanaitwa waongo, huku wakina Mbowe na wengine wakiitwa wachochezi, Wakina Kubenea wakimwagiwa Tindikali na wakina Ndimara Wakikatwa mapanga. Hiyo ndiyo AMANI! Bahati nzuri, watanzania wanaelewa, na ipo siku KITAELEWEKA!
Eti, kero ya wapinzani ni kuona CCM inazidi kuimarika na kukubalika! Ndio maana siamini kabisa kuwa haya ni maneno ya Kaka Mwakatobe. Mwandishi anasema watanzania hawafanyi utafiti kubaini ukweli huu, anasahau kuwa ni watanzania hawa hawa ndio wametoa maoni yao kwenye tafiti mbalimbali kwamba umaarufu wa CCM umeporomoka. Sio sababu ya chuki ya upinzani, ni kwa chama hicho kushindwa kutekeleza ahadi lukuki ilizotoa. Huu ni ukweli ambao mwanaCCM yoyote makini anaufahamu.
Mchambuzi huyu anarudia kauli ya mara kwa mara ya kwamba wapinzani hawana DIRA- lakini mchambuzi huyu huyu anajua hazina ya sera ambazo CCM imekuwa ikichota kutoka upinzani kuanzia enzi za kufuta kodi za manyanyaso mpaka kipindi hiki cha kupitia mikataba ya madini. Mchambuzi huyu anajua kuwa “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania” ni lengo tu la MKUKUTA ambao umeandaliwa na wananchi wote bila kujali itikadi na kuchukuliwa tu kwenye ilani ya Chama tawala. Mchambuzi amesahau kabisa kwa CCM imeshatelekeza falsafa na itikadi yake, na hata Mwalimu Nyerere amekiri hili kwenye kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania. Mwandishi angetueleza- DIRA YA CCM ni ipi? Mchambuzi mahiri kama huyu alipaswa awe anafahamu kabisa Dira na mwelekeo wa vyama vingine nchini. CHADEMA mathalani, mambo haya yamefafanuliwa Kwa CHADEMA falsafa na itikadi yake inapatikana hapa: http://www.chadema.net/maoni/kijue.php na ilani yake ambayo utangulizi wake ni dira ya “Tanzania tunayoitaka” inapatikana hapa: http://www.chadema.net/ilani/tanzania.php na popular manifesto 2005 inapatikana hapa http://www.chadema.net/maoni/ilani.php . Lakini Ndio maana sitaki kabisa kuamini kwamba aliyeandika ni Kaka Mwakatobe, kwa kuwa najua kabisa yeye alikuwa kwenye jopo la wataalamu waliofanya mapitio ya Sera na Katiba ya CHADEMA mwaka 2003/04. Wakati huo, mimi hata sikuwa mwachama wa CHADEMA. Kwa maneno mingine, najua Kaka Mwakatobe anafahamu vizuri asili ya Falfafa ya “Nguvu ya Umma”. Hivyo, sifikiri kabisa kwamba anaweza kusema upinzania hauna dira! Yeye anafahamu kwamba hata Mwalimu Nyerere aliwahi kusifia Sera za CHADEMA.
Bahati nzuri nilikuwepo CHADEMA mwaka 2005, na nilikuwa mgombea Ubunge wa Ubungo wakati huo; najua undani wa mambo. Mwandishi amezusha kwamba mwaka 2005 CHADEMA iliponzwa kwa kujipendekeza kwa wafadhili; wafadhili gani, kujipendekeza gani? Hapa mwandishi anataka kusheheneza hisia kwamba CHADEMA ilipewa mapesa kutoka nje na kuyatumia kwenye helikopta na kuwatelekeza wagombea wa ngazi nyingine. Bahati nzuri, ni CHADEMA pekee iliyotangaza wazi matumizi yake ya fedha katika kampeni. Rejea Tamko la Baraza Kuu la CHADEMA hapa: http://www.chadema.net/uchaguzi/ripoti1.php CCM mbona mpaka leo haijatangaza? Hapa imeelezwa wazi kiasi gani tulitumia, kiasi gani zilitumika kwenye helikopta. Lakini tulikwenda mbele zaidi kutangaza ni kiasi gani zilipatikana toka nje. Tuliweka wazi, kampeni zetu hajikuchangiwa kwa fedha toka nje- zimegharamiwa kwa ruzuku ya chama ni michango ya wanachama mbalimbali. Kitu pekee tulichopata toka kwa rafiki zetu wa nje ni ruzuku kidogo ya kuendesha warsha ya mafunzo kwa wagombea ubunge, na michango hii ya kiufundi haikutolewa kwa CHADEMA tu katika kipindi cha kuelekea uchaguzi. Mchambuzi huyu, angepaswa aandike uchambuzi wa kutaka CCM itangaze mapato na matumizi yake ya uchaguzi-na angeuliza vile vile, zile tuhuma za fedha za uchaguzi wa CCM kutoka nje ya nchi ambazo walisema wangelishitiki gazeti la nje lililofichua suala hilo zimefikia wapi? Kama mchambuzi huyu hafahamu tuhuma hizo- asome humu atazipata: http://www.chadema.net/habari/misc/misc_10.html .Baada ya kuchambua hapa, atajua ni chama kipi cha siasa ‘kinajipendekeza’ kwa wafadhili wake wa wakati wa uchaguzi!
Inasikitisha kwamba mchambuzi kama huyu, anadiriki kudanganya kuwa CHADEMA ilikuwa ikitumia milioni 10 kwa siku kwa ajili ya helikopta! Huu ni uzushi kabisa. CHADEMA haijawahi kutumia milioni 10 kwa siku kwa ajili ya kukodi helikopta. Niliwahi kuchambua gharama za matumizi ya helikopta katika makala yangu iliyotoka katika vyombo vya habari vya nyumbani- makala hiyo inapatikana pia hapa: http://www.chadema.net/blogu/mnyika/2008/01/helikopta-ya-chadema-raha-karaha-au.html .Ni vyema akajiridhisha na kusema ukweli.
Mchambuzi huyu, anataka kujenga picha kwamba upinzani unapokea mabilioni mengi ambayo ingeweza kabisa kujenga zahanati, shule, hospitali nk ili kuonyesha kwa vitendo. Mchambuzi anataka kujenga picha kwamba vyama vya upinzani vinatapanya fedha! Mwandishi anashindwa kujua kwamba ruzuku ya vyama inatolewa kwa kazi maalumu za kisiasa ambazo sheria ya vyama vya siasa imeelekeza. Mwandishi anashindwa kujua kwamba michango mahususi inayotolewa inatolewa kwa kazi mahususi. Mchambuzi anashindwa kujua kabisa kwamba huwezi kupewa mchango wa kuendesha mafunzo wa viongozi ukapeleka kwenye kujenga zahanati pamoja na umuhimu wake. Kubwa kuliko yote, mwandishi anaashindwa kuelewa kazi ya vyama vya siasa- anashindwa kujua kwamba vyama vya siasa vinatoa sera na viongozi ili watumie vizuri rasilimali kuleta barabara, zahanati nk. Mwandishi anashindwa kujua kwamba michango ya wafadhili mbalimbali inapitia serikalini kutoa huduma za kijamii na kutekeleza miradi ya kimaendeleo- kazi ya upinzani ni kuiwajibisha serikali iliyoko madarakani na kutoa mwelekeo mbadala! Mwandishi anashindwa kujiuliza mbona CCM inapokea ruzuku ya takribani bilioni mbili(milioni 2000) kila mwezi kutokana na fedha za walipa kodi, wakati CHADEMA inapokea milioni 56 tu kwa mwezi lakini CCM haijengi barabara, zahanati kutokana na ruzuku hiyo? Badala yake madarasa, zahanati nk zinajengwa kwa kodi za wananchi kupitia bajeti ya nchi, michango ya wananchi na fedha toka kwa wadau wa maendeleo? Ni kutokujua au kupotosha?
Hili la kusaidia miradi ya kuthibiti umaskikini: Linahitaji mjadala zaidi, tujiulize- duniani kote, kazi ya vyama vya siasa ni nini? Imani yangu ni kuwa CHADEMA tumeweza kufanya vizuri katika miradi mbalimbali katika halmashauri ambazo tumeongoza Kigoma Ujiji, Hai na Karatu; na tuendelea katika halmashauri ambazo tumeanza kuongoza baada ya 2005, sasa tunaoongoza pia Halmashauri mpya moja ya Tarime. Sidhani kama upinzani unatakiwa kugawa fedha za miradi ya kuondoa umasikin- kufanya hivyo, kuna vikwazo vifuatavyo: Mosi, tutakuwa tunatoa takrima ya maendeleo kwa wananchi toka mifukoni mwa chama ambayo kimsingi ni rushwa, Pili, tutatoa fursa kwa mafisadi nao kuanza kutoa michango hiyo kupitia vyama vyao- sasa mwenye kisu kikali ndio atakula nyama. Tatu, tutakuwa tumetoka katika malengo ya msingi ya chama cha siasa. Kwa maoni yangu, chama cha siasa ni muunganiko wa watu wenye mawazo yanayoshabihiana kwa lengo la kuchukua dola ili kutekeleza mawazo hayo, na kabla ya kuchukua dola kuiwajibisha dola iliyoko madarakani kwa misingi ya mawazo hayo! Kwa hiyo bidhaa za vyama vya siasa ni 'uongozi', 'sera' na 'oganizesheni'. Kwa hiyo, tunaondoa umasikini kwa kutoa viongozi bora, sera bora na oganizesheni bora. Kwa sasa pamoja na kuwa upinzani tumewatoa wakina Dr Slaa, Zitto nk ambao wanaiwajibisha serikali kwa sera zinazopinga ufisadi na kutetetea rasilimali za taifa, kwa kweli matokeo ya harakati zao ni fedha zetu za kodi kutumika vizuri zaidi katika miradi ya kuondoa umaskini. Naamini kabisa, serikali ya sasa(pamoja na ufisadi unaoendelea) kwa staili hii ya Orodha ya mafisadi kila mmoja yuko tumbo joto- hivyo, sidhani kama watakuwa na ari, nguvu na kasi mpya ya kufuja fedha za miradi ya kuondoa umaskini kama ilivyokuwa wakati wa Mkapa- sasa kama hali ikiwa nzuri kiasi nani atanufaika kama sio mwananchi? Nani amesababisha manufaa hayo kama si upinzani? Na ikifika 2009 na 2010 changamoto kwetu ni kuwafanya watu waelewe kwamba wakituchagua sisi tutaingia wenyewe kutekeleza sera hizo vizuri zaidi tofauti na CCM inayofanya mambo machache tena baada ya shinikizo. Kama ni kutokujua, niliwahi kuandika hapa kazi chama cha siasa- na ni kwa vipi upinzani unasaidia maendeleo nchini: “Huduma za Kijamii zinazotolewa na Vyama Vya Siasa vya Upinzani. Akitaka naweza kumtumia hilo andiko. .Leo upinzani ukiwezesha bilioni 133 zilizofujwa BOT zikapatikana unajua ni madarasa, barabara na zahanati ngapi? Kati ya chama kutumia milioni 56 kufanya harakati za kisiasa za kupambana na ufisadi na kuokoa bilioni 133 na chama kutumia milioni 56 kujenga matundu ya choo nyumbani kwa wananchi wachache kipi bora?
Ndio maana siamini kama ujumbe huu umeandikwa na kaka Mwakatobe; najua anaujue Ukweli huu, na anajua kuwa UKWELI ni UHURU. Na anajua kwamba utumwa wowote unaosababishwa na jitihada ya kulinda maslahi binafsi na ni suala baya. Lakini anajua zaidi, kujaribu kuambikiza utumwa huo kwa kizazi cha baadaye cha Taifa hili ni DHAMBI. Na Ole wake yule ayakayesababisha mmoja wapo wa watoto hawa kutenda dhambi...................
JJ
Ps: Unaweza kuutuma ujumbe huu kwa Kaka Mwakatobe na marafiki zetu wengine, lakini usiupeleke kama makala ya kwenye gazeti kwa kweli. Sijafanya uhariri wowote wala kuweka mpangilio, nimeandika mawazo kwa kadiri yalivyokuwa yakitiririka. Heri ya Mwaka Mpya na wasalimie Kigoma.

0 Comments:
Post a Comment
<< Home