PROFESA MSOLLA : SULUHISHO LA MIGOMO NI KUTOA HAKI KWA WANAFUNZI
Na John Mnyika
Hivi karibuni, akiwa mkoani Mbeya katika majumuisho ya ziara yake ya vyuo vikuu. Waziri wa Sayansi teknolojia na elimu ya juu, Mh Prof-Peter Msolla, alinukuliwa na vyombo vya habari akitoa vitisho kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa madai kuwa wanafunzi wanaohusika na migomo vyuo vikuu wanajiandalia mikosi na kwamba hawatapata ajira baada ya masomo yao.
Prof Msolla ametoa kauli hiyo huku kukiwa na vuguvugu la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kupinga taratibu za sasa za utoaji mikopo ambapo kwa mujibu wa taratibu za sasa ambazo kimsingi zinakinzana na sheria halisi ya mikopo. Pamoja na mapungufu mengine ya msingi ni kwamba wanafunzi wanalazimika kuchangia asilimia 40 ya gharama za masomo. Na sasa vuguvugu hili huenda likasambaa zaidi wakati wowote kwani mpaka sasa kuna taarifa kuwa baadhi ya wanafunzi katika baadhi ya vyuo wanashinikizwa kuchangia pesa hizo ambazo ni kati ya laki 3 na zaidi ya laki 5 ili waruhusiwe kuingia darasani sambamba na kupewa huduma zingine za msingi.
Aidha, hivi karibuni, vyombo vya habari vimeandika kwamba wanafunzi wa Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA) waliendesha mgomo na kuja wizarani kutaka kuonana na waziri kupinga utaratibu wa kuchangia asilimia 40 ya mkopo. Pesa hizi ni takribani laki 5 ambazo walipaswa kuzilipa kabla ya kuanza masomo.
Imeelezwa kuwa serikali imewataarifu kuwa wasaini mikataba na kuendelea na masomo. Uamuzi huu unaweza kutafsiriwa kuwa tayari serikali imewasaidia wanafunzi hawa kuendelea na masomo.
Lakini ukweli ni kuwa huu ni mtego. Ni wazi kwamba serikali ama inasubiri kipindi cha karibu na mitihani ndipo iwabane wanafunzi kwa kuwataka kulipa hiyo asilimia 40 au inaweza kuwaruhusu wafanye mitihani na pindi watakapokwenda likizo ikatoa maelekezo kuwa wasiolipa wasirejee mpaka watakapopata pesa za kulipa.
Huu ni mkakati wa ‘wagawe uwatawale’ (divide and rule) ambao serikali imekuwa ikiutumia mara kwa mara kuvunja mshikamano wa wanafunzi. Na hii inathibitika kutokana na kauli ya Waziri wa Elimu ya Juu, Prof Msolla ambaye amenukuliwa na gazeti la Uhuru la Januari 17 akisema kwamba serikali haina mpango wa kulipa hiyo asilimia 40 kwa kuwa wanafunzi walikwishasaini fomu za mikopo na kwamba sharti hilo lilikuwa sehemu ya mkataba. Waziri anasahau kuwa fomu hizo zilishasainiwa na wanafunzi chini ya shinikizo la serikali pamoja na ahadi mbalimbali kwamba serikali iko mbioni kuandaa utaratibu mzuri zaidi. Tunachotaka ni serikali kutoa tamko kwamba itahakikisha kwamba utaratibu huu unafutwa kwa kutenga pesa katika bajeti ya mwaka huu ikiwemo za kulipia gharama za wanafunzi walioko masomoni hivi sasa.
Ni katika muktadha huo, tunapaswa kulijadili suala hili ili kuhakikisha serikali inafika mahala inakiri kuwa mikopo sio hisani , ni haki ya kila mtanzania anayepata udahili wa chuo kikuu kwa mujibu wa sheria inayounda bodi ya mikopo. Na kwa mantiki hiyo tunasisiza msimamo wetu katika misingi ifuatayo;
Migomo na Maandamano ni moja ya njia halali katika kudai haki.
Kauli ya Mh Waziri ni kama vitisho ambavyo vilikuwepo hata wakati wa serikali ya mkoloni wa kizungu kuwadhibiti wanafunzi wanao nyanyaswa na serikali yao wasipisisimamie haki yao kwa vigezo kwamba kufanya hivyo ni kujihatarishia mazingira ya ajira punde baada ya kumaliza masomo yao.
Tunapaswa kutambua kuwa nguvu ya umma ni hatua ya mwisho katika kuhakikisha umma unapata haki yake stahiki kutoka kwa serikali isiyojali. Migomo na maandamano ni hatua ya mwisho inayorejesha wadau katika meza ya majadiliano baada ya hatua za awali za majadiliano kutokuzaa matunda.
Maandamano na mashinikizo ya hali ya juu kutoka kwa wanafunzi wenyewe dhidi ya serikali ni mambo yasiyoepukika kama hatua ya mwisho kwani serikali yetu imekuwa na tabia ya kutowatendea haki wanafunzi kila wanaponyanyaswa mpaka wanapoamua kusitisha masomo kwa migomo na maandamano.
Hivyo kwa kuwa serikali imejenga tabia ya kutowasikiliza wanafunzi wa elimu ya juu mpaka wagome na kuandamana, Na kwakuwa migomo na maandamano ni njia zinazoruhusiwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, katiba ya nchi na sheria za taasisi mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu kama moja ya njia ya kushinikiza haki kutendeka. Hivyo si ajabu kwa wanafunzi wa elimu ya juu kufanya kila linalowezekana ikiwa ni hata kugoma na kuandama kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha haki yao inapatikana, inalindwa na kuheshimiwa.
Jumuiya ya wasomi kama vyuo vikuu kuacha haki yao inyongwe kwa hofu ya kitambo, tena isiyo na ukweli wowote ni mfano mbaya wa namna wasomi wanaotarajiwa kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya msingi ili nchi hii ikombolewe wanavyoweza kudhulumiwa haki yao mbele ya umma unao watazama kama majemedari na wakombozi watarajiwa.! Ni usaliti wa hali ya juu.! Ni usaliti kwa nafsi zao, ni usaliti kwa taifa lao.
Ndio maana natoa rai kwa Mh Waziri kuacha vitisho, na badala yake ahakikishe wanafunzi wanapata haki yao kama kweli ni msomi mzalendo. Hakuna binadamu anayependa kugomagoma wala kuandamana. Serikali isiwaweke wanafunzi katika mazingira yanayowalazimisha kugoma na kuandamana.
Haiingii akilini kwa mwanafunzi kutishwa kuwa asigome na wala kuandamana kwa madai kuwa kufanya hivyo kunahatarisha ajira yake hapo baadae wakati ukweli ni kwamba mwanafunzi asipogoma hatopata mkopo, na asipopata mkopo atafukuzwa chuo, hatomaliza Chuo. Sasa kama hatopata mkopo na kushindwa kumaliza chuo, ni ajira gani ambayo Msola anasema wanafunzi wanahatarisha ?
Mapungufu ya sera na utekelezaji wa sera ya mikopo.
Utaratibu wa sasa wa mikopo una mapungufu mbalimbali ya kimsingi ambayo yanaleta mkanganyiko wa hali ya juu katika taifa hili, na zaidi unatishia mustakabali wa elimu hiyo kwa wanafunzi wa kitanzania wanao toka familia masikini.
Mosi ; Dhana ya uchangiaji wa gharama za elimu ya juu imegeuzwa kuwa mfumo wa kufanya elimu ya juu nchini kuwa bidhaa inayouzwa badala ya huduma (service). Dhana nzima ya uchangiaji gharama za masomo ya elimu ya juu imepotoshwa , Kwa mujibu wa sera ya serikali , Mwanafunzi anatakiwa kuchangia asilimia 40 na serikali kumchangia asilimia 60 ya mkopo wote.
Lakini kinachotokea ni kwamba, wanafunzi wanapewa mkopo wa asilimia 60 (huu ni mkopo sio mchango kwani watalipa), na baadae mwanafunzi anatakiwa kujilipia mwenyewe asilimi 40 ya gharama zinazobaki.
Hivi katika muktadha huu, serikali inawezaje kusema kuwa inawachangia wanafunzi kusoma elimu ya juu ? Hii ni cost sharing ya namna gani ? .Kilichopo hapa ni mwanafunzi kujilipia asilimia 100 za gharama za masomo yake (total cost bearing).
Pili ; Dhana ya kutoa mkopo kwa wanafunzi waliofaulu kwa daraja la kwanza wavulana, na la kwanza na la pili wasichana ina mapungufu ya msingi. Kwanza inapingana na sheria ya mkopo kuwa kila atakayekidhi vigezo vya mkopo ikiwa na maana ya kupata usajili/udahili wa chuo na kuhakikisha kuwa hana uwezo wa kujisomesha atapatiwa mkopo. Kinachozungumzwa hapa ni kufikia viwango vya kusajiliwa/kudahiliwa chuoni na sio utaratibu wa madaraja kama ulivyoelezwa hapo juu.
Baada ya upinzani kutoa msukumo katika suala hili, serikali ilirudi nyuma kidogo na kuamua kutoa mkopo kwa baadhi ya wanafunzi wa daraja la pili wavulana na la tatu wasichana ambao wengi wao walijiunga na ualimu. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mh Rais kuwa pamoja na serikali kuwaruhusu baadhi ya wanafunzi wa daraja la pili wavulana, na la tatu wasichana, lakini bado vigezo vilivyowekwa katika fani mbalimbali ni kikwazo kwa wanafunzi hawa kujiunga na vyuo husika.(mathalani katika fani za udaktari na uhandisi).
Vigezo vilivyowekwa vilizingatia uhaba wa fursa zilizopo kwa msingi wa ni kiwango gani serikali imepanga kutoa mkopo katika fani fulani. Kwa mantiki hiyo, serikali inapotoa tamko kuwa imewaruhusu wanafunzi wa daraja la pili wavulana na la tatu wasichana katika fani chache, bila kuhakikisha vigezo vinabadilishwa, ni sawa na kutoa haki ambayo haipo. Ni kuwafanyia ‘usanii’ vijana wake.
Ni vyema Mh Rais atambue hilo, lakini pia atafiti kuhusu ukweli wa kauli yake kuwa serikali inasomesha wanafunzi waliofaulu vizuri kabisa kwa madai kuwa serikali haiwezi kuwekeza kwa wanafunzi wasio na uwezo.
Nasema hivyo kwa sababu kuu mbili : Kwa upande mmoja, kuna wanafunzi wengi wanao faulu kwa kiwango cha chini kutokana na mazingira ya shule wanazosomea, mifano dhahiri ni shule za serikali na zile za umoja wa wazazi wa CCM, shule hizi nyingi hazina walimu wala vifaa, mwanafunzi anayepata daraja la tatu au la pili katika shule za aina hii anao uwezo mkubwa wa kujifunza kuliko wanafunzi wengi wanao soma katika shule za kimataifa, seminari na baadhi ya shule za sekondari chache za serikali ambazo zinafaulisha vizuri.
Kwa upande mwingine, Kauli hii imekuwa ikithibitishwa na maprofesa wanaofundisha vyuo vikuu kwa kubainisha wazi kuwa wanafunzi wengi wanaofanya vibaya vyuo vikuu ni wale wanaotoka shule zenye majina makubwa ambao waliingia kwa alama za juu. Kwa maana hiyo basi, hoja ya Mh. Rais kumchukulia kila mvulana aliyepata daraja la pili na kila msichana aliyepata daraja la tatu hawezi kufanya vizuri sana, ina mapungufu hayo ya msingi.
Tatu ; Dhana ya kwamba waliopata daraja pili wavulana, na la tatu wasichana kuwa ndio wenye uwezo wa chini kitaaluma, na kwa hiyo wataenda ualimu ni kielelezo kuwa , serikali yetu inaamini Ualimu ndio taaluma isiyohitaji utaalamu sana, na hivyo haihitaji watu wenye uwezo mkubwa. Kitu ambacho kimewahi kurudisha maendeleo ya taaluma nchini kwa miaka kadhaa sasa.
Nne ; Mwisho lakini kubwa zaidi ni kwamba chama tawala CCM katika ahadi zake wakati wa kampeni iliahidi kuhakikisha inawapatia mkopo wanafunzi 30,000 kwa mwaka. Hata hivyo waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza mpaka la tatu ni wanafuzi 21,000 tu. Hivyo kama serikali ingekuwa inatekeleza ahadi zake wanafunzi wote wangepata udhamini wa chuo kikuu. Hata hivyo zaidi ya nusu ya hao , ambao walikidhi vigezo vya mkopo hawakupata mkopo.
Rai yangu kwa serikali, namuomba tena Mh Rais amshinikize waziri wa elimu ya juu , aufahamishe umma wa Tanzania ni kwa kiwango gani serikali yako imeshindwa kutimiza ahadi uliyoitoa wakati wa kampeni. Na pia serikali ieleze ni wanafunzi wangapi walistahili mkopo kwa mujibu wa sheria lakini wamekosa na sasa inaandaa utaratibu gani kuhakikisha walikosa mwaka 2006 watapewa haki yao mwaka 2007, na kwamba mwaka 2007 kosa halijirudii na kwamba ahadi ya Mh rais itatekelezwa. Ili serikali iweze kutekeleza ahadi yake inapaswa kutenga si chini ya bilioni 195 kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya mikopo. Hii inawezekana, kwani kama tunaweza kutenga bilioni 272 katika miradi yenye utata kama mkataba wa RICHMOND, inashindwaje kusikiliza matakwa ya wananchi ya kufanya suala la elimu kuwa kipaumbele ? Kama Mfanyabiashara mmoja wa kitanzania anaweza kutuhumiwa kupata shilingi bilioni 15 ambayo ni sawa na milioni elfu 15 kama ‘hongo ya asilimia 30’ kwenye ununuzi wa RADA tunaweza kweli kusema hatuna pesa za kusomesha wanafunzi elfu 15 wanaohitaji takribani shilingi milioni moja kwa mwaka ?
Mwelekeo wa elimu ya juu nchini.
Kwa ujumla kadri miaka inavyokwenda, na awamu za utawala wa CCM zinavyobadilika, ndivyo mwenendo wa elimu ya juu nchini unavyozidi kwenda kombo, na zaidi unaelekea kujenga matabaka ya masikini wasio na haki ya kupata elimu dhidi ya matajiri wenye uwezo wa kununua elimu.
Itakumbukwa kuwa katika awamu ya kwanza ya serikali ya TANU, na baadae CCM ya wakulima na wafanyakazi chini ya Hayati Baba wa Taifa. Mwl Julius Kambarage kwa mtazamo wa siasa ya ujamaa, wanafunzi wote walisomeshwa bure chuo kikuu. Walipewa mahitaji yote ya msingi kwa mwanafunzi kuweza kusoma. Mwalimu aliweza kuwapatia watoto wa wakulima na wafanya kazi masikini elimu ya bure bila hata ya kuuza migodi, hifadhi za wanyama makampuni na nyumba za serikali na mali zote za watanzania. Viongozi walioko madarakani hivi sasa wengi wao walisomeshwa na serikali, ni vipi wanashindwa kuweka utaratibu mzuri wa kizazi kipya kupata fursa ya elimu ya juu?
Serikali ya awamu ya pili ilijaribu kuwalazimisha wanafunzi wajilipie chuo kikuu, kwa sababu Mwalimu Nyerere alikuwepo, na wanafunzi walikuwa na uwezo mkubwa wa kujipanga na kupigania haki yao, serikali ilishindwa. Hata hivyo kadri Chama Cha Mapinduzi kilivyozidi kujipanga kuhakikisha kinamkandamiza mtoto wa kimasikini, ndivyo kilivyokaribia ushindi, hatimaye katika awamu ya tatu ya CCM kiliweza kushinikiza wanafunzi kujisomesha lakini kwa mkopo.
Baada ya serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani , tulitarajia mabadiliko ya msingi katika elimu ya juu. Lakini mbaya zaidi kilichotokea ni kwamba ni mwenendo mbaya na wa ukandamizaji zaidi kwa wanafunzi wanaotoka familia masikini.
Wakati serikali ya awamu ya kwanza iliweza kuwasomesha wanafunzi wote bila kulipa hata shilingi wala mkopo, serikali ya awamu ya pili na ya tatu pamoja na kuuza migodi makampuni na mbuga za wanyama ilishindwa kuwasomesha wanafunzi masikini. Ilifuta utaratibu huo na kuanza kuwasomesha wanafunzi masikini kwa mkopo huku yenyewe ikijivinjari kwa maisha ya anasa katikati ya dimbwi linalotoa harufu ya umasikni.
Serikali ya awamu ya nne iliyoingia madarakani kwa ahadi kemkem na kujifanya yenyewe ndio mkombozi. Ndani ya mwaka mmoja tu, mwenendo na kasi yake mpya, unaelekea kummaliza mkulima na mfanyakazi ambaye ambae pamoja na ukweli kuwa ndio aliyepigania uhuru wa nchi hii ndio masikini wa kutupwa katika nchi hii
Wakati serikali ya awamu ya pili na tatu pamoja na uozo uliofanyika lakini iliweza kutoa mikopo. Serikali ya awamu ya nne kwasababu ya kuendekeza mikataba yenye mazingira ya rushwa na matumizi ya anasa sambamba na kukosa dira madhubuti ya uchumi, imeshindwa kutoa mikopo kwa wanafunzi masikini ambao ni watoto wa wakulima na wafanyakazi, na sasa inawataka waanze kujilipia.
Naona hatari kubwa huko tuendako, na bila wanafunzi na asasi za kiraia kushika bango, serikali itaturejesha kwenye utumwa mkongwe wa wageni, maana mali zote zinasombwa na wageni, huku viongozi wetu wakiingia mikataba yenye utata kila kukicha. Bila wanafunzi na asasi hizo kusimama wima kudai haki hii, nchi yetu inaelekea rasmi kuingia kwenye ukoloni mamboleo.
Hakuna nchi iliyofanya mapinduzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii bila ya kuwekeza zaidi kwenye elimu. Chama Cha Mapinduzi kinaposhindwa kufanya mapinduzi katika elimu maana yake hakiwezi kufanya mapinduzi katika maendeleo ya watu kama dhana ya mapinduzi ni katika maendeleo ya watu, labda kama maana yake ni vinginevyo.
RAI YANGU KWA VIJANA
Naomba na kusisitiza kuwa, vijana tusitishwe wala tusirubuniwe. Tunataarifa kuwa CCM kimeanza kupita vyuoni na mbaya zaidi kinavunja sheria kiliyoipigania chenyewe ya kukataza siasa vyuoni, lakini sasa kinawatumia viongozi wa vyuo kufanya mkakati wa kuwaingiza vijana CCM, siwazuii vijana kuingia CCM lakini CCM izingatie sheria za nchi kwa upande mmoja,
Na kwa upande wa pili, nawaomba vijana mtazame mbele zaidi , na kujiuliza mara mbili mara tatu juu ya ni nani atasimamia haki zenu ? Je sheria hizi zinamruhusu mdogo wako, ndugu yako, na hata mtoto wa jirani yako aliyeko kijijini kupata elimu ya juu?.Je unaweza kutetea na kuleta mabadiliko kwa mfumo uliopo kazi ambayo ilimshinda hata mwasisi wa CCM yenyewe, Hayati Baba wa Taifa letu, Mwl JK Nyerere ?
Muda wa kustarehe vijana bado !, nchi ipo kwenye lindi la tope la umasikini , tusichelee kudai haki yetu na kuisimamia nchi yetu ikae kwenye mstari mnyoofu kwa hofu potofu ya kunyimwa kazi, au ahadi za kupewa ukuu wa wilaya, ubunge, ukurugenzi, nk.
Tusimame pamoja tudai mabadiliko ya kweli mpaka serikali tuiweke kwenye kona yenye mwanga iweze kuona kuwa kupewa uongozi wa nchi ni kupewa dhamana na wananchi, na haina maana ya kuwa juu ya vichwa vya wananchi.
Na nawataka wanafunzi wa vyuo vikuu wasiwe wabinafsi na kusimama kidete kwenye migomo na maandamano wakati wa kudai haki zao za mikopo tu bali watazame maslahi ya umma kwa ujumla ikiwemo masuala ya kupinga mikataba mibovu kama IPTL, RICHMOND, kwenye madini, ununuzi wa RADA na ndege ya rais. Huku kuna mabilioni ambayo yalipaswa kuelekezwa kwenye elimu.
Profesa Msolla akumbuke maneno ya Mwanamuziki Bob Marley kwamba unaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa muda mchache lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote, na kama Mwalimu alivyowahi kusema haki haiwezi kupewa kwenye kisahani cha chai kama zawadi. Haki inatafutwa. Hakuna kulala, Mpaka kieleweke!
Mwandishi wa makala hii ni mwanaharakati na mwanasiasa kijana anayepatikana kupitia 0754 694 553, mnyika@chadema.net

1 Comments:
Tovuti yako ina habari za nyuma sana. Kuna mambo mengi yamefanyika na we umeshiriki, lakini hujayaweka kwenye blogu. naona hata kwenye tovuti yako ya chama vivyo hivyo. Hakuna habari mpya. Imelala!
4:31 PM
Post a Comment
<< Home