MNYIKA AENDA ZIARA MAREKANI
Mkurugenzi wa Vijana, Bwana John Mnyika anatarajiwa kuondoka leo kwa ziara ya wiki tatu nchini Marekani kwa mwaliko wa Idara ya Ikulu ya nchi hiyo. Anatarajiwa kushiriki kwenda kwenye ziara ya kujifunza inayohusu “ Uwezeshaji wa Vijana”.
Ziara yake ni sehemu ya mpango unaosifika wa Kiongozi Mgeni wa Kimataifa(International Visitor Leadership Program) ambao unawezesha mawasiliano ya kibinafsi na kitaaluma kati ya watu wa Marekani na Tanzania.
Malengo ya ziara hii ni: kutambulisha mfumo wa demokrasia wa Marekani, mfumo wa kisiasa wa Marekani na umuhimu wa ushiriki wa vijana kwenye siasa na uraia; kujifunza jinsi vijana wa Marekani wanavyopata stadi za kuathiri sera za umma katika ngazi za chini, majimbo, kitaifa na kimataifa na kuchambua asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala la vijana na kuhamasisha ubadilishanaji wa mikakati ya kiutawala na kimaendeleo.
Bwana Mnyika amealikwa kutokana na ushiriki wake katika mipango anuai ya maendeleo ya vijana nchini kupitia asasi mbalimbali hususani YouthNet Tanzania ambamo ni mjumbe wa kamati yake ya vijana. Amechaguliwa pia kutokana na mchango wake mkubwa katika harakati za vijana nchini na uwezo wake wa kiuongozi.
Ataanza ziara Washington, DC ambapo atashiriki katika kutahini wajibu wa serikali ya majimbo na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuunga mkono jitihada za kuhamasisha uongozi wa vijana na kutembelea Capitol Hill pamoja na mahakama kuu. Atakutana na maafisa wa asasi mbalimbali za kisiasa ikiwemo Baraza la Viongozi Vijana wa Kisiasa Marekani na kamati za kitaifa za Republican na Democratic.
Atatembelea Seattle ambapo atakutana na viongozi wa wanafunzi na kushiriki katika mafungo katika kambi ya YMCA ya Seymor ambayo yatahusisha shughuli za nje zenye shabaha ya kuendeleza stadi za uongozi na kufanya kazi kwa timu. Hapa Tanzania Bwana Mnyika ni mjumbe wa Baraza Kuu la chama cha vijana wa kiume wa kikristu Tanzania (YMCA).
Bwana Mnyika atasafiri kwenda St. Louis, Missouri kwa programu nyingine ambayo itahusisha mkutano na wanachama wa kamati ya Uongozi wa Watu Weusi kuhusu Elimu ambayo inafanya kazi kuondoa ombwe la kitaaluma kati ya vijana wa Kimarekani wenye asili ya Kiafrika. Atakutana pia na wawakilishi wa programu ya Raslimali za UKIMWI kwa watoto(AIDS resource for KIDS) ambayo inatoa huduma za kukinga VVU/UKIMWI miongoni mwa vijana ambazo kitovu chake ni familia.
Baada ya hapo atajumuika Portaland, Maine ambapo anatarajiwa kushirikiana na wawakilishi wa asasi mbalimbali mathalani Mfuko wa Uongozi wa Raia na Tuongee America. Atakutana pia na maafisa wa Rising Tide, kikundi kisicho na mrengo na chama chochote cha siasa kinachojihusisha na kutoa mafunzo na maendeleo kwa viongozi wa baadaye wa kati ya miaka 16 mpaka 35 ambao wameonyesha nia ya kisiasa na uthabiti wa kijamii na wana malengo ya kuendeleza stadi zao katika stadi za kampeni, harakati, na ushawishi. Bwana Mnyika amepanga kutoa uzoefu wa ushiriki wake katika uchaguzi Mkuu 2005 ambapo alikuwa mgombea Ubunge katika jimbo la Ubungo akiwa na miaka 25.
Halafu ataondoka Portland pamoja na washiriki wengine kuelekea “Big Apple” ambapo watapata ziara ya utambulisho wa Jiji na New York ambayo itawapa picha kuhusu utajiri, historia, idadi ya watu na nafasi yake kama makao makuu ya kiuchumi ya Marekani. Atashiriki pia katika ziara ya kutembelea umoja wa Mataifa. Watakutana pia na Youth Venture ambayo ni taasisi ya kijamii inayowawezesha vijana kuunda na kuzindua miradi yao na kuwahamasisha kuchukua wajibu wa ziada wa maisha yao na ya jumuia.
Mnyika anatarajiwa kurejea kutoka New York tarehe 23 June, 2006 na kufanya mkutano wa kutoa mrejesho kwa ofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini.
Imetolewa tarehe 29 Mei, 2006 na Idara ya Vijana CHADEMA.

0 Comments:
Post a Comment
<< Home