Hoja zangu kuhusu mjadala wa "CCM kumbomoa Mbowe na CHADEMA" :
Mwanakijiji, Mkandara na Mzee Es,
Nadhani nikiendeleza ukimya na kusoma tu sitakuwa nimechagiza vizuri mjadala.
Naowaomba nirushe kidogo “chakula cha fikra”
Tuisome na kuijadili habari husika kwa ujumla- kichwa kinasema Mbowe lakini habari imedokeza kuwa CCM inataka kumharibu “Mbowe na chama chake”. Sijui kama mwandishi alitumia “chama chake” kama lugha ya picha au ulikuwa akimaanisha umiliki. Yote kwa yote, kwenye ‘chama chake’ tuweke “CHADEMA”. Utamaduni wa chadema ni kutoamini katika chama mtu bali chama taasisi.
Niweke bayana kwamba nitakayosema ni maoni yangu binafsi, si kauli ya chama kama.
Naamini ni kweli CCM ina mpango wa kubomoa upinzani, au niweke vizuri- “kundi fulani” ndani ya CCM. Wanajitahidi kupandikiza migogoro(Rejea mtiririko wa matukio ndani ya vyama), wanajitahidi kutaka kuhonga(vyeo, fadhila nk) baadhi ya viongozi wanaochipukia katika upinzani lakini kubwa kuliko yote wanajenga kupitia vyombo vya habari propaganda dhidi ya upinzani(kwa walio nyumbani rejea mtiririko wa habari na makala katika magazeti mbalimbali kuhusu upinzani, utajiuliza kwanini makala kuhusu masuala nyeti haziandikwi kwa wingi lakini kuna makala nyingi za namna hii tena katika hoja zisizo na mshiko). Huu ni mkakati.(media spin)
Ni kweli vyombo vya habari vilitumika wakati wa kura za maoni ndani ya CCM sasa nguvu imeelekezwa katika kuupamba utawala na kubomoa upinzani.
Lakini Rais Kikwete anajiweka mbali kabisa na haya, alianza kwa kusema upinzani usibezwe baada ya matokeo, akaendelea kusema katika hotuba yake ya kufungua bunge kuwa mwenye kuwepo CHADEMA ni haki yake, asibuguziwe, akaendelea kusema Moshi Mjini kwamba hata waliochagua upinzani hawatanyimwa maendeleo. Na kwamba hakutakuwa na ubaguzi wala kunyanyaswa. Haya ni maneno matamu! Lakini hali halisi ardhini ni tofauti. Je, rais kama kikwete mwenye kupenda kuwa karibu na watu hajui kinachoendelea?Je usalama wa Taifa hawamwambii?. Nini chanzo cha mgogoro wa CCM Tarime kama sio kuchukia upinzani? Wananchi wa Karagwe wanafanywa nini hivi sasa? Angalia mwenendo wa Tendwa katika sakata la TLP!. Ya Mahita je?Najua wengine mtasema, serikali iliomba msamaha kwa CUF, je kwa kiasi gani imesadia CUF kusafishika? Lakini mimi nasema, CCM ilianza kuua upinzani siku nyingi kabla ya uchaguzi na kwenye uchaguzi wenyewe. Hoja ninazo, ila si sehemu ya mjadala huu.
Mzee mwanakijiji, umekuja na nadharia kwamba Mbowe ndio kaua upinzani kwa kuamua kugombea urais. Hii si kweli. CHADEMA imefanya tathmini na kuona ni jinsi gani chama kimepata faida kwa kusimamisha mgombea urais. Macho ya wananchi, asasi mbalimbali, na hata vyombo vya habari yasingekuwepo kwa CHADEMA kama isingekuwa na mgombea urais. Uzito wa Mbowe wakati wa kampeni usingekuwa mkubwa kama angezunguka kama mwenyekiti( Waulize Mbatia na Mvungi). Kuna baadhi ya maeneo matokeo ya wagombea ubunge na udiwani yamebebwa na kampeni za urais kupitia mabango, vipeperushi na nguvu ya helikopta kuwafikia watu wengi. Na ingekuwa vigumu kuwianisha muda katika ya haja ya CHADEMA kuendelea kutawala Hai na siasa za nchi nzima. Kwa ujumla, CHADEMA iliwasha mwamko mpya katika siasa za Tanzania uchaguzi uliopita kwa kuamua kumsimamisha Mbowe kama mgombea urais.(Hili nalo ni suala pana linalohitaji makala ya peke yake yenye uchambuzi wa matokeo kwa kina).
Yote kwa yote, mimi siamini kama upinzani ulishindwa kwa kiasi kile cha matokeo ya tume. Siamini kama zile ndio kura za Mbowe na wala siamini kama ndio kura za CUF kama ambavyo siamini ndio kura za hata Mrema pamoja na kushuka kwake kisiasa. Unayaamini matekeo ya Temeke, Karagwe, Bukoba mjini, Ubungo na kwingineko? CHADEMA imeeleza sababu za kwanini haidhani kama yale yalikuwa matokeo sahihi ya uchaguzi( rejea http://www.chadema.net/uchaguzi/ripoti1.php ). Hili nalo ni suala linalohitaji mjadala wa peke yake!
Mzee Es, si kweli kwamba gazeti la Tanzania Daima linamilikiwa na viongozi wa CCM wasiokuwa wanamtandao. Tena ukichambua kwa makini habari za magazeti utaona kuwa Tanzania Daima ni moja ya magazeti yanayoandika sana habari za wanamtandao likizidiwa kiasi na magazeti ya Habari Corporation. Kwa jinsi ninavyofahamu ulivyomjuzi wa mengi, naamini mkono uliteleza!
Sitaki kwa sasa kuingia kwenye mjadala wa Independent candidates na mwelekeo kwa siasa za Tanzania aliouchokonoa Mzee Es. Kuna maswali mengi ya kujiuliza: Utanufaisha CCM, upinzani ama wananchi? Tufanyeje? Nashauri tuweke kwenye mjadala wa peke yake ili tusipoteze mtiririko.
Mzee Es umesema Freeman ni CCM. Kama alivyosema Mwanasiasa-Tupe ushahidi. Kwa maoni yangu mimi siyo. Ilinichukua muda sana kuamua kuingia CHADEMA. Mimi napenda Utomaso!. Niliwachunguza sana viongozi wa CHADEMA kabla sijajiunga. Wengi nawaamini. Kama watabadilika huko mbele hiyo ni silika nyingine tofauti ya binadamu. Nimekaa karibu sana na Freeman, msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya maisha naufahamu. Kama watu wa jamii hiyo ni wanaendana na yanayofanyika CCM basi watanzania wengi ni CCM. Lakini siamini hivyo. Kumbuka Freeman ana mizizi katika CHADEMA kama mmoja wa waasisi miaka kumi na ushee nyuma. Unataka kusema toka wakati huo alikuwa CCM? Sitaki kuzungumza sana, labda niulizwe-maana ningependa kuzungumzia zaidi masuala, sio watu. Walau kidogo naweza kuzungumzia matukio. Nachelea kuingia katika mizani ya busara nyepesi, busara za kawaida na busara zilizotukuka.
Umeghafilika pia katika suala la wabunge. Habari imezungumzia ubunge wa Afrika(AU), umeingiza ubunge wa EAC. Lakini umeenda mbali zaidi kusema kwamba ubunge huu ulipaswa kupewa kwa chama cha upinzani chenye wabunge wengi..nk ..nk..nk. Kwanza rejea kwenye mjadala wa bunge la AU kwa kuwa wa EAC bado(hata ukija ni yoyote anaweza kugombea si lazima awe mbunge. Pili, hitaji ni mbunge wa upinzani bila kujali kama anatoka chama chenye wabunge wengi au la suala ni awe mbunge. Ukweli ni kwamba CCM walifanya vikao kabla wakakubaliana kwamba wasimchague Zitto Kabwe wa CHADEMA wala Fatma Maghimbi wa CUF na kumfuata Mzee Phares wa TLP agombee. Wakampa kura nyingi. Walitumia uhuru wao, lakini siamini kama walitumia busara zao-hawakutanguliza utaifa wala sifa za kiuongozi. Mmoja alisema kabisa hatumtaki Zitto kwa kuwa tutaipa nguvu CHADEMA. Hii ni ishara ya wazi ya kuwa CCM imedhamiria kubomoa upinzani!
Ya Sumaye, JM na umakamu mwenyekiti tuyaache kwa sasa. Sumaye alichafuliwa na alilamika wazi- “Anayeingia madarakani kwa kalamu atatawala kwa risasi”. Lakini walichofanya ni kutumia udhaifu wa Sumaye, kuuweka wazi. Utasemaje sasa ya Mwananchi, uarabu wa Salim Ahmed Salim na mauaji ya Karume? Haya yalitokea Mzee Es. Tusipingane na ukweli. Ni wazi baada ya kumaliza kazi hiyo sasa nguvu imehamishiwa kwa majukumu mawili niliyoyataja.
Sasa kwani nini CHADEMA ilengwe zaidi na sio chama kingine? Mwandishi ametoa sababu mbili- Mosi, Kampeni kali za CHADEMA uchaguzi uliopita(nakubaliana naye), Pili-Mbowe na kashfa ya Kikwete ya pesa Mererani(nakubaliana naye kidogo), Tatu, Hoja ya Mbowe kuhusu wanamtandao(Nakubaliana naye ingawa amefinya sana hoja hii- sababu hapa ni tamko la CHADEMA la siku mia za kikwete-ukitaka kuthibitisha rejea http://www.chadema.net/makala/mbowe/mbowe_10.html ). Mimi nasema, sababu kuu ni tatu: Moja, CHADEMA ilikuwa tishio kwa CCM uchaguzi uliopita(ndio maana CCM iliitaja sana CHADEMA). Pili, CHADEMA imekubalika sana kutokana na uchaguzi uliopita(sasa na wakati wa kubomoa kukubalika huku); tatu, CHADEMA ndio chama pekee cha upinzani kilichokuwa kisiasa na kuonyesha matumaini ya kuchukua dola chaguzi zijazo na Mbowe ndio tishio zaidi kwa Kikwete na mgombea ajaye wa CCM( rejea http://www.chadema.net/uchaguzi/ripoti1.php -hivyo CHADEMA itazamwa kuwa adui namba moja wa CCM na utawala wake). Lakini kwa nini haraka hivi? Ni kutokana na sababu ya tatu, Uamuzi wa CHADEMA na Mbowe kuukosoa utawala wa Kikwete-hivyo mtandao unaona umaarufu wa Kikwete unapunguzwa. Ndio maana utasikia kauli si tulidhani Mbowe ni mstaarabu kumbe sio. Tulitegemea CHADEMA isikosoe nk nk. Ndio maana tamko limetolewa siku nyingi lakini mpaka leo CCM wanaendelea kulikanusha( rejea http://www.chadema.net/ kwenye tamko la Vijana wa CHADEMA kuhusu UVCCM). Hivyo kwa mtu yoyote makini anajua pamoja na idadi ndogo ya wabunge, CHADEMA sio chama cha kupuuza. CCM wanajua kuwa idadi ndogo ya kura sio nguvu ya kweli ya CHADEMA, mashushu wao wanaujua ukweli uliopo nyuma ya matokeo ya uchaguzi 2005.
Sitaki kuingia katika mjadala na Mzee Es kuhusu rai yake ya kutaka magazeti ya IPP na Tanzania Daima yafungiwe.
Mzee Es,nawe heshima yako, nakumbuka. Nilikwambia Sumaye na Keenja hawataaniibia. Na ukweli ndio. Walioiba Ubungo ni system. Wala sio kwa nguvu ya Keenja. Yeye alisha-surrender. Mkurugenzi wa manispaa wakati huo ambaye ndiye alikuwa msimamizi wa uchaguzi alitamka kuwa alipewa maagizo toka juu( yeye alisema ikulu) atangaze matokeo. Na kweli mwishowe baada ya kumaliza kuhesabu za urais akatoka nje aliporudi akatangaza matokeo bila kujumlisha matokeo ya Ubunge kituo hadi kituo kama sheria inavyohitaji. So my heart is sober on this, I belief the residents and young people were the winners in Ubungo what ever the results. Anyway, huu ni mjadala tofauti.
Mzee Es, narudia tena. Matokeo ya uchaguzi hayawezi kunifanya niingie CCM. Kwa nini sikuingia in a first place. I differ in its leadership principles and policies!. Sijaingia kwenye siasa kwa ajili ya “Mkate na Jibini”. There is a vision and mission I am pursuing. Sorry for using strong language but as Shaban Robert puts it, ‘’ ‘’Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake nikipatwa na ajali kama hiyo sitawaonea wivu wale wanaodumu na marafiki zao siku zote. Siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo na kujinyima ushirika wa milele unaotarajiwa kutokea baada ya kushindwa kwa uongo”.
Mwanasiasa, nakubaliana na hoja zako.Asante.
Jasusi, yafungulie mjadala hayo maswali- Masha, Kikwete na Madini ya Mererani. Tujadili humu, kutoka Afgem mpaka TanzaniaOne. Kutoka IMMA mpaka kauli za Tundu Lissu. Yapo mengi. And Let them respond!. There are issues on minerals, let me reserve them for now.
Mkira, naendeleza ulipoishia..as Bob says…but now you see z light..STAND UP FOR YOUR RIGHT.
Mwanakijiji-maswali yako kuhusu loyalty ya wabunge naomba uyafungulie mjadala wa pekee. Kuna masuala nyeti humo! Ila Mimi naamini katika kuishi beyond partisan politics. Vyama mbalimbali ni muhimu, muhumu sana. Ndio maana namshangaa yoyote mwenye kutaka kuua upinzani. I know politics is about power, but a good politician or citizens must know absolute power corrupts absolute. Ndio maana nataka kwa pamoja tuvilee vyama lakini kulea kwetu vyama kusitufanye tupoteze utaifa.
Mkandara, ni kweli kuwa JK hakuvunja sheria. Na wala Free hakusema alivunja sheria. Alichosema ni kuwa Kikwete hawezi kuwatetea wana Appolo akiwa rais kwa kuwa amechangiwa na wale wale waonaowanyanyasha wanamerereni. This was a policy attack. But CCM took it as a personality assault which is tantamount to cropping enemity!
Ya takrima nakubaliana nawe. We profaned the essence of our traditional hospitality and even abused the dictationary meaning on the word “Takrima”.
Nakubaliana nawe kuwa tumeipokea demokrasia kichwa kichwa. We the new generation have the role to change this trend!
Mkandara, Free wa mwaka juzi si wa mwaka jana na si wa leo. He is one of the everyday readers and learners I have seen. Perhaps sasa umuandikie kwa kirefu. You may send him direct your plans or through me. Anapokea sana mawazo.
Ila narudia tena, CHADEMA ilifanya vizuri sana kumsimamisha kugombea. Nakubaliana nawe kuwa CHADEMA inahitaji kujipanga, na ndicho tunachofanya hivi sasa. Tulianza kwa kutengeneza Mpango Mkakati wa Miaka mitano na Mpango kazi wa Mwaka. Sasa tumeanza kutekeleza. Tuko kwenye mchakato wa kubadili katiba, mwezi wa nane tutafanya mkutano mkuu. Mwakani tunafanya uchaguzi. Viongozi wote wa chama wamefupisha muda wao wa uongozi kupata fursa ya kukipanga chama vizuri ikiwemo kuweka muundo thabiti kwa mapambano.
Mkandara, sikubaliani sana na dhana ya kutoa viongozi toka CCM. Mko vijana makini wengi na watanzania wengi mahiri ambao hawana vyama. Karibuni tujenge upinzani wenye manufaa kwa taifa. Somo la Njelu Kasaka na wengine linafundisha mengi kuhusu watokao CCM. But I don’t close my door. There are some good people the likes of Dr. Slaa, Balozi Ngaiza, Pesha etc.
Mkandara, Mbowe kuwa na ndoto ya kwenda ikulu sio nongwa. Ni fursa. As JF. Kenedy said- mwanasiasa yoyote lazima autake uongozi ndipo ataweza kupata uongozi na kuongoza. But what is important is shunning away from Machavellianism!. Suala la msingi ni unataka kwenda ikulu kwa nia gani? Is Ikulu a means or an end?. Kiongozi yoyote anayetaka kwenda ikulu kwa nia njema atajenga taasisi. Naamini ndicho Mbowe anajitahidi kufanya CHADEMA. Na katika hatua kilipofika hivi sasa CHADEMA sio Mbowe, CHADEMA ni taasisi. Katika hatua hii maamuzi ya mwachama mmoja hayawezi kubomoa chama. Hii ndio CHADEMA inayopaswa kulindwa dhidi ya hujuma za chama tawala ambacho ni chama dola ili Tanzania tuendelee kuwa na upinzani wenye maslahi kwa wote.
Mungu atubariki tuendelee kutofautiana bila kugombana. Kama nilivyosema mwaka jana SIASA sio UADUI

1 Comments:
Mnyika, naona umekuja kwa nguvu zote. Karibu sana. Hatua nzuri hii ya wanasiasa kuanza kutumia blogu.
2:17 PM
Post a Comment
<< Home